Bahi. Miaka 27 ni umri mrefu kwa mwanadamu. Mtu mwenye umri huo atakuwa amesoma na tayari ameanza kulitumikia Taifa na familia yake.

Umri huo unatosha kuelewa simulizi ya Rehema Ndoje, mkazi wa Kijiji cha Mwitikila katika Wilaya ya Bahi, ambaye ametumia miaka 27 ndani ya kuta za magereza ya Isanga, Segerea, Keko na Mbeya akisubiri kitanzi kutokana na hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyopewa na mahakama.

Rehema aliingia gerezani Mei 24, 1999 akiwa na mashtaka ya mauaji ya mtoto wake aliyekuwa na umri wa miezi minane, kosa alilodaiwa kulitenda kwa kushirikiana na mpenzi wake ambaye hata hivyo alitoroka na hajawahi kupatikana.

“Mimi nilikamatwa kwa sababu moja tu, sikuwa nimeripoti tukio hilo na lilipotokea alinibembeleza ninyamaze nami nikakubali, lakini nani aliyetenda anajua Mungu, sitaki kueleza zaidi. Uzembe na huruma yangu kwa mtu wangu vingeniua…,” anasema huku akifuta machozi.

Rehema Ndoje akiwa mlangoni katika nyumba ya mama yake kijijini Mwitikila Wilaya ya Bahi.

Rehema (48) alikutwa na madhira hayo akiwa jijini Dar es Salaam na wakati huo alikuwa mama wa nyumbani, huku mchumba wake huyo ambaye hakuwa mzazi mwenza wake, akijishughulisha na kazi ndogondogo.

“Niliyezaa naye huyo mtoto sikuwa naishi naye na kama mnavyojua umri wa ujana, kumbuka nilikuwa na miaka 21. Sasa huyo niliyempata akawa hapendi niwe na mtoto. Yalitokea mambo mengi hapo katikati lakini nikaambiwa nisitoe taarifa, mwisho yakatokea yaliyotokea,” anasema.

Anasema mara baada ya kukamatwa, jambo kubwa walilolitaka Polisi ni aeleze mpenzi wake yuko wapi, ndugu zake na historia ya mhusika, lakini alishindwa kutoa maelezo zaidi kwa sababu hakuwa amemfahamu kwa undani kutokana na kukutana mjini kwa muda mfupi.

Kwa mujibu wa Rehema, baada ya mahojiano ya kina na Polisi, ilibainika kuwa alikuwa amefanya uzembe uliosababisha tukio hilo, hivyo akafunguliwa mashitaka ya mauaji, kutiwa hatiani na baadaye Novemba 11, 2007 kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuhusu hilo, lakini anaeleza kuwa kigugumizi, kulia mahakamani kila alipofikishwa na kutotoa ushirikiano wa moja kwa moja ili mpenzi wake apatikane, vilikuwa miongoni mwa sababu zilizomfanya Jaji amtie hatiani.

Rehema anasema hukumu hiyo ilimchanganya na hakujua aanzie wapi zaidi ya kusubiri siku yake ya kunyongwa, lakini anamtaja aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Segerea ambaye, mara baada ya kupokea hukumu hiyo, hakuridhishwa nayo ndipo akamtafutia wanasheria waliokata rufaa.

Rehema Ndoje akiwa mlangoni katika nyumba ya mama yake Kijijini Mwitikila Wilaya ya Bahi.

Kwenye kumbukumbu za mahakama, inaonyesha alikata rufaa Novemba 9, 2007 kupinga hukumu hiyo, ambapo walijitokeza watu wa kumsaidia baada ya kupata historia kamili kuhusu kesi hiyo ya jinai namba 40 ya mwaka 2001.

Anaeleza kuwa rufaa yake haikuweza kusikilizwa isipokuwa aliitwa na Mkuu wa Gereza na kuelezwa kuwa anatakiwa mahakamani Februari 13, 2026. Alipopelekwa huko, majaji walieleza namna alivyozungushwa lakini wakasema viapo vya kukiri kutokuwepo kwa nyaraka vilitosha kumwachia huru.

Maisha ya gerezani

Rehema anasema maisha ya gerezani ni magumu, yanahitaji moyo wa uvumilivu na hayahitaji mtu kuwa na mawazo mengi, ingawa anakiri miaka aliyoingia maisha yalikuwa magumu zaidi ukilinganisha na sasa.

Anasema mfungwa wa kunyongwa siku zote haoni kama kuna kitu mbele yake zaidi ya kuwaza kaburi lake litakuwa wapi na atazikwaje, licha ya ukweli kuwa aliwahi kuota zaidi ya mara tatu kuwa ameachiwa huru.

“Tangu nimeingia gerezani sijawahi kusikia mfungwa yeyote amenyongwa. Niliowakuta hadi niliwaacha wakiishi na hukumu za kunyongwa, lakini hawajawahi kunyongwa. Wanaishi kwa mateso na mawazo. Nashauri adhabu hii iondolewe kwa sababu si rafiki kabisa,” anasema Rehema.

Faili halikuonekana

Rehema amepambana kutafuta kumbukumbu za jalada lake kwa miaka 19 bila mafanikio kwani halikuwahi kuonekana na hata sasa hajui mwenendo mzima wa kesi yake. Hata alipotolewa aliachiwa bila kurejea kesi wala hukumu.

Mawakili waliandika barua nyingi kutafuta jalada lakini watunza kumbukumbu walisema hawalioni jalada hilo, ambapo zaidi ya barua tisa zinaonyesha viapo pekee vya kukiri kutokuliona jalada wala nyaraka.

“Wakuu wa magereza ambayo nilipitia walikuwa wanashangaa. Tukiandika barua wanasema hakuna jalada. Kila mtu alijiuliza nimefungwa kwa namna ipi, kwa nini nyaraka hazionekani na jambo hilo lilinichanganya sana,” anasema.

Hata hivyo, anasema akiwa amekata tamaa, maofisa Magereza waliendelea kumtia moyo na kumtafutia watu wa kumsaidia kwani kila aliyemsikiliza aliona upo mlango wa kutokea isipokuwa kulikuwa na ukwamishaji upande wa nyaraka.

Apata msaada zaidi

Mapambano ya kufuatilia nyaraka yalichagizwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Ex-Prisoners Foundation (TEPF) iliyotoa taarifa kuhusu mfungwa huyo kwa jinsi alivyokuwa akipambana kutafuta haki yake lakini akikwamishwa.

Mkurugenzi wa TEPF, Rose Malle anasema ucheleweshaji wa rufaa umekuwa tatizo kwa wafungwa wengi, kiasi kwamba baadhi hufikia hatua ya kukata tamaa na kuishia kusema, “Mungu anajua.”

“Mimi nimeyaishi haya. Nilimkuta Rehema akiwa na miaka 10 gerezani. Nilihukumiwa kunyongwa, nilikata rufaa na kuachiwa, mwenzangu alikuwa bado anahangaikia nyaraka. Changamoto alizopitia huyu dada ni kubwa. Ndipo nilipokwenda Gereza la Isanga nikakuta bado yupo, niliumia,” anasema Rose.

Rose anasema alichukua hatua kwa kuwasiliana na taasisi nyingine ili waunganishe nguvu, ambapo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) walijitokeza na safari ya kutafuta nyaraka ikaanza.

Rose anasema kutafuta haki ukiwa gerezani ni vigumu kama hakuna wa kukushika mkono, lakini pia kuna ugumu kwa mfungwa anapotoka gerezani na kurejea uraiani.

“Changamoto pia wanapotoka baada ya vifungo vyao kwani wanakutana na kutengwa na jamii na kunyooshewa vidole kwa unyanyapaa. Wanatoka hawana mitaji. Nashauri wafungwa wanapotoka magerezani wapewe kitu cha kuanzia maisha kulingana na ujuzi wanaoupata,” amesema Rose.

Wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hidaya Haonga na Meneja Uchechemuzi wa kituo hicho, Raymond Kenegene, wanasema kesi hiyo iliwapa ugumu licha ya nia ya kutaka kumsaidia apate haki yake.

Hidaya anasema ushirikiano wa Msajili wa Mahakama Kuu ulisababisha wabadili mkakati wa kesi hiyo na kuomba Ofisi ya Mwendesha Mashtaka iandike viapo kwa kila hatua, jambo lililosaidia majaji kumwachia huru bila kupitia nyaraka nyingine.

“Tulikwama kufanya follow-up kwa kukosa nyaraka. Msajili wa Mahakama na Mahakama Kuu wote tuliungana lakini hatukufanikiwa kuzipata. Ndipo ikaamuliwa viandikwe viapo ambavyo vilisaidia hatimaye ametoka,” amesema Hidaya.

Mama mzazi wa Rehema, Phoibe Mkundya anasema hana shida na binti yake huyo kwani wanafahamu kila kilichotokea, ingawa baada ya hukumu walikata tamaa kwamba ipo siku angerudi tena nyumbani.

Rehema Ndoje akiwa na Mama yake, Phoibe Mkundya

“Rehema aliondoka hapa akaniachia mtoto mdogo wa kike. Amerudi amemkuta binti yake tayari amezaa na hata mjukuu wake yupo kidato cha kwanza. Sisi tumempokea na tumefanya sherehe kubwa lakini tutakwenda kufanya ibada kanisani. Asante Mungu,” anasema Phoibe.

Phoibe anaiomba jamii kumsaidia mwanawe kwani amejirekebisha na amejutia makosa yake ya uzembe, hivyo anahitaji kuishi kama wengine ingawa kwa sasa hana kitu cha kufanya kutokana na mazingira aliyoyaacha na jinsi alivyoyakuta.

Kwa mujibu wa mama huyo, mara ya mwisho Rehema aliondoka kijijini hapo Novemba 22, 1998 na akarudi Februari 14, 2026 baada ya Mahakama kumuachia huru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *