
Unguja. Benki ya Dunia (WB) imeitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kuongeza kasi kutekeleza mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia, Tanzania (Pamoja) ili kuleta matokeo chanya ambayo yanaonesha mabadiliko ya maisha ya wananchi kupita mradi huo.
Pia, imesisitiza matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa kama ilivyopangwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Mradi wa Pamoja unafadhiliwa na WB kwa kipindi cha miaka mitano (2024/29) na utagharimu Sh33 bilioni.
Kauli hiyo imetolewa Mei 11, 2026 na Mkurugenzi wa Uendelevu wa Kijamii na Ujumuishi wa WB, Valarakshmi Vemuru baada ya kumaliza kikao kifupi kilichofanyika ofisi za wizara hiyo kati ya benki hiyo, wizara na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA).
Katika kikao hicho ujio wa WB pia ulilenga kuona umefikia hatua gani katika utekelezaji na kushauriana njia sahihi za kuendeleza mradi huo.
“Lengo ni kupata matokeo chanya, hivyo wizara inapaswa kwenda kasi ya utekelezaji wa mradi na kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha hizi kama ilivyopangwa,” amesema.
Vemuru amesema mradi huo unalenga zaidi katika masuala ya fursa za kiuchumi na kuwanusuru wanawake katika unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto (ECD) ili wanawake wapate muda mzuri wa kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wizara hiyo, Abeida Rashid Abdalla ameahidi kutekeleza ushauri uliotolewa kuhakikisha unaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Amesema kikao hicho kimetoa fursa ya kushauriana na kuelekezana utekelezaji wa mradi huo, hivyo wizara imepokea ushauri uliotolewa ikiwemo kuwashirikisha jamii ili kuwajengea uelewa na kuongeza kasi ya kiutendaji.
Benki ya Dunia imetoa Sh33 bilioni kwa ajili ya mradi huo ambao una lengo la kuwainua wanawake kiuchumi na kupunguza vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto.
Abeida amesema katika mazungumzo yao pia wamekubaliana kuishirikisha zaidi jamii katika ngazi za chini ili kuwajengea uelewa kuhusiana na mradi huo utakavyowanufaisha wanawake kiuchumi kupitia fursa za mikopo na masuala ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji (GBV).
“Mradi huo utawainua kiuchumi vijana na wanawake kwa sifa ambazo zitakidhi vigezo vya kuwezesha kupata mikopo. Pia utajenga nyumba salama mbili moja Unguja na moja Pemba zitakazotumika kuwahifadhi waathirika wa vitendo vya ukatili udhalilishaji wa kijinsia” amesema Abeida.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhani Mohamed amesema kuwa mradi huo hautowasaidia wanawake pekee bali na wanaume watawezeshwa ili kuwa na jamii yenye mtazamo wa kiuchumi na kubadilisha maisha ya wananchi.
Mradi kwa Kukuza Usawa wa Kijinsi Tanzania (Pamoja) ni wa miaka mitano unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unatekelezwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na ZEEA, ukilenga kuwainua wanawake kupitia fursa za mikopo na kupinga vitendo vya udhalilishaji.