
Kwa mujibu wa tathmini mpya ya upatikanaji wa chakula IPC iliyotolewa leo, zaidi ya watu milioni 3.6 wako katika kiwango cha dharura cha njaa, huku wengine milioni 22.9 wakiwa kwenye hali ya mgogoro wa chakula kati ya mwezi Januari na Juni 2026.
Mikoa ya mashariki ya North Kivu, South Kivu, Ituri na Tanganyika ndiyo imeathirika zaidi, ambapo zaidi ya watu milioni 9.9 wanatarajiwa kuendelea kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula katika kipindi hicho.
Mashirika ya misaada yanasema msaada wa chakula hauwafikii watu wengi wanaouhitaji, hali inayosababisha familia nyingi kushindwa kupata chakula na kujikwamua kiuchumi.
Ingawa hali imeonesha nafuu ndogo ikilinganishwa na makadirio ya mwezi Septemba 2025, bado kiwango cha uhaba wa chakula kinaendelea kuwa cha kutisha mashariki mwa DRC.
Muarobaini wa tatizo
Ndani ya ripoti hiyo mapendekezo kadhaa ya nini kifanyike yametolewa ikiwemo
• Kuongeza kwa haraka misaada ya chakula na lishe kwa watu walioathirika zaidi.
• Kuboresha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu katika maeneo yenye mapigano.
• Kusaidia wakulima na familia kurejesha maisha yao kupitia mbegu, zana za kilimo na msaada wa kujikwamua kiuchumi.
• Kuimarisha ulinzi na usalama kwa raia waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita.
• Kuongeza uwekezaji katika huduma za lishe kwa watoto na wanawake wajawazito ili kupunguza utapiamlo.
• Kuimarisha uratibu kati ya serikali, mashirika ya misaada na wadau wa kimataifa ili kukabiliana na ongezeko la njaa.
• Kuchukua hatua za muda mrefu za kuimarisha uzalishaji wa chakula na uthabiti wa jamii dhidi ya migogoro na majanga.
Kwa undani zaidi kuhusu ripoti hiyo soma hapa: Kwa lugha ya kiingereza Download snapshot (English) na kwa lugha ya kifaransa hapa Download report (French)