
“Tunaona mashambulizi yakizidi kuratibiwa,” msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, James Elder, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva. “Matukio yaliyorekodiwa yanahusisha watoto kupigwa risasi, kuchomwa visu, kupigwa na hata kunyunyiziwa pilipili.”
Kwa mujibu wa UNICEF, watoto wapatao 70 wameuawa tangu Januari 2025 wastani wa angalau mtoto mmoja kila wiki huku wengine 850 wakijeruhiwa, wengi wao kwa risasi za moto.
“Haya yote yanatokea wakati mashambulizi ya walowezi yakifikia viwango vya kihistoria,” Elder ameendelea, akieleza kuwa Machi 2026 ilishuhudia idadi kubwa zaidi ya Wapalestina waliojeruhiwa na mashambulizi ya walowezi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Watoto washambuliwa kwa vipigo
Baada ya ziara ya hivi karibuni katika Ukingo wa Magharibi, msemaji huyo wa UNICEF amesimulia kukutana na mtoto wa umri wa miaka minane aliyepigwa kwa kipande cha mbao katika shambulizi la walowezi na kulazwa hospitalini kutokana na majeraha ya kichwani.
Mama wa mtoto huyo “alivunjwa mikono yote miwili alipojaribu kumlinda mtoto wake wa miezi minne kwa kuweka mikono yake kati ya mtoto na rungu la mshambuliaji.”
Elder pia amezungumzia ongezeko la mashambulizi yanayohusiana na elimu, yakiwemo mauaji, majeraha na kukamatwa kwa wanafunzi pamoja na kubomolewa kwa shule.
“Shule, ambazo zinapaswa kuwa maeneo ya usalama na utulivu, zinazidi kuwa maeneo ya hofu,” amesisitiza.
“Nilitembea pamoja na watoto wa shule katika Ukingo wa Magharibi ili kuwasaidia kuepuka mashambulizi,” amesema. “Inasikitisha kuwaona wakitembea. Hawatembei moja kwa moja kwa sababu kila wakati wanaangalia nyuma yao. Hii ni safari ya kwenda shule. Imekuwa safari ya kupitia katika hofu,” ameongeza.
Idadi ya watoto wanaozuiliwa yavunja rekodi
Elder pia ameripoti “ongezeko kubwa la kukamatwa na kuzuiliwa kwa watoto wa Kipalestina kutoka eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu na Israel”, akisema watoto 347 wanashikiliwa katika magereza ya kijeshi ya Israel “kwa madai ya makosa yanayohusiana na usalama” idadi kubwa zaidi katika miaka minane.
“Kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba zaidi ya nusu ya watoto hawa, 180, wanazuiliwa chini ya mfumo wa kizuizi cha kiutawala bila ulinzi wa kawaida wa kisheria, ikiwemo kutokuwa na fursa ya mara kwa mara ya kupata ushauri wa kisheria na haki ya kupinga kuzuiliwa kwao,” amesema.
Watoto wa Gaza wauawa na kujeruhiwa vibaya
Wakati huo huo huko Gaza, Elder amesema kuwa tangu usitishaji vita wa Oktoba 2025, Umoja wa Mataifa umerekodi angalau watoto 229 waliouawa na wengine 260 kujeruhiwa.
Dkt. Reinhilde Van de Weerdt, mwakilishi wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, katika Maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, amewaambia waandishi wa habari kuwa watoto wapatao 10,000 katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa wanaishi na majeraha yanayobadilisha maisha yao kabisa.
Kwa ujumla, inakadiriwa kuwa watu 43,000 kati ya 172,000 waliojeruhiwa Gaza tangu Oktoba 2023 wamepata majeraha makubwa yanayoathiri viungo vya mwili, uti wa mgongo au ubongo. Karibu watu 2,500 wamejeruhiwa tangu usitishaji vita wa Oktoba 2025.
“Kati ya watu 2,277 waliokatwa viungo vya mwili, chini ya asilimia 25 wamepatiwa viungo bandia vya kudumu,” amesema Dkt. Van de Weerdt, akieleza kuwa Gaza inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa hivyo.
Waliokatwa viungo wakosa msaada
Akizungumza kutoka Yerusalem, mwakilishi huyo wa WHO amesema takriban mizigo 18 ya vifaa vya ukarabati kama vile viti mwendo na viungo bandia bado inasubiri kibali cha kuingia Gaza, huku muda wa kusubiri ukiwa kati ya siku 130 hadi zaidi ya mwaka mmoja.
Kwa jumla, zaidi ya majeraha 50,000 yanayohusiana na vita yanahitaji huduma za muda mrefu za ukarabati, lakini hakuna kituo chochote cha ukarabati kinachofanya kazi katika eneo hilo.
“Kila siku ambayo huduma za ukarabati Gaza zinaendelea kukosa rasilimali za kutosha ni siku ambayo hatari ya ulemavu unaoweza kuzuilika inakuwa ya kudumu,” amehitimisha Weerdt.