Dodoma. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema uwekezaji katika ujasiriamali wa vijana, matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo na mifumo ya tahadhari za mapema ni muhimu katika kuimarisha usalama wa chakula na ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo imetolewa leo, Jumanne Mei 12, 2026 na Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini, Christine Mendes, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya kuanzishia biashara kwa vijana kupitia mradi wa Vijana Kilimo Biashara (VKB).

Amesema vifaa hivyo vitasaidia vijana kuingia katika biashara za kilimo, kuongeza ajira na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno huku mifumo ya Tehama ikiimarisha utoaji wa tahadhari za mapema.

Baadhi ya wakulima wakiangalia mashine za kupuria zao la mtama zilizotolewa na shirika la chakula Duniani (WFP) mkoani Dodoma leo Mei 12, 2026 Jijini Dodoma. Picha na Rachel Chibwete

Tangu mwaka 2019, amesema WFP kwa kushirikiana na Tanzania Breweries Limited (TBL) imekuwa ikitekeleza miradi ya kuimarisha zao la mtama katika Mkoa wa Dodoma.

Mradi huo, amesema ulianza na wakulima 1,300 katika Wilaya za Kongwa na Mpwapwa, sasa umeongezeka hadi Chamwino na kuwafikia zaidi ya wakulima 3,000.

Kwa mujibu wa Mendes, usambazaji wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 20 hadi 40 na kuwawezesha zaidi ya wakulima 4,300 kulima ekari 7,400 katika vijiji 70 kwa msimu wa 2025/2026.

Katika kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kilimo, amesema wamekabidhi mashine 71 za kupuria mazao zenye thamani ya Sh251.3 milioni kwa wakulima wadogo wa Mkoa wa Dodoma.

Amesema mashine hizo zitasaidia kupunguza upotevu wa mazao na pia kuwa chanzo cha ajira kwa vijana.

Aidha, amesema kupitia mradi wa kilimo himilivu kwa mabadiliko ya tabianchi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland, WFP itanunua mashine nyingine 18 kwa wakulima wa Bahi, Chemba na Kondoa, hatua itakayofikisha uwekezaji wa mashine hizo hadi Sh315 milioni mwaka 2026.

Amesema WFP pia inatekeleza mpango wa miaka mitano wa Vijana Kilimo Biashara unaofadhiliwa na Mastercard Foundation katika mikoa minane nchini, ukiwalenga zaidi ya washiriki 100,000 wakiwemo vijana 26,000 kutoka Dodoma na Singida.

Amesema vijana 423 waliomba kushiriki katika programu ya Generation Food Accelerator, kati yao 100 walipata mafunzo na biashara 30 bora zitapewa ruzuku na msaada wa kitaalamu.

Baadhi ya wakulima wakiangalia mashine za kupuria zao la mtama zilizotolewa na shirika la chakula Duniani (WFP) mkoani Dodoma leo Mei 12, 2026 Jijini Dodoma. Picha na Rachel Chibwete

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amezitaka Halmashauri za Mkoa huo kununua mashine za kupuria mtama ili kusaidia wakulima kuvuna kwa urahisi na kupunguza upotevu wa mazao.

“Nimeambiwa mashine hizi zinapepeta mtama kwa zaidi ya asilimia 90 na mazao yake yanakuwa safi kuliko yanayopepetwa kwa mikono,” amesema Senyamule.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Selestine Masalamado, amesema vifaa vya Tehama vyenye thamani ya Sh121 milioni vitasaidia kuboresha ufuatiliaji wa majanga, utoaji wa tahadhari za mapema na uratibu wa taarifa kwa wakati.

Amesema kupitia mfumo huo wakulima watapata taarifa mapema kuhusu mvua, ukame na milipuko ya wadudu waharibifu ili kuchukua hatua za kulinda mazao na maisha yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *