Shughuli za umma na zile za binafsi nchini Kenya, hivi leo zimesimama kwenye miji kadhaa nchini Kenya ikiwemo jiji kuu la Nairobi, ambalo limeshuhudia baadhi ya wanasiasa, wanaharakati wa haki za binadamu na baadhi ya wazazi waliopoteza watoto wao katika vurugu za mwaka 2024, wakiandamana kuelekea ofisi za bunge.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Licha ya njia nyingi za kuingia katikati ya jiji kuwa na vizuizi, baadhi ya wanasiasa wa upinzani akiwemo aliyewahi kuwa makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, aliyewahi kuwa jaji mkuu wa Kenya, David Maraga na waziri wa zamani wa sheria Martha Karua waliandamana kutokea hoteli ya Serena.

Hata hivyo kabla ya kufika ofisi za bunge, walizuiliwa na kuondoka na kuwaacha baadhi ya wazazi waliopoteza vijana wao pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu kuendelea na maandamano yao hadi nje ya lango la kuingia viwanja vya bunge ambapo walizuiliwa.

Tofauti na tangazo lililotolewa hapo jana na waziri wa mambo ya ndani ya nchi Kipchumba Murkomen, kuwa waandamanaji wangelindwa na kwamba shughuli za kawaida ziendelee, hali imekuwa tofauti katika jiji la Nairobi, ambalo limeshuhudia shughuli zikisimama.

Waandishi wa RFI Kiswahili walioko katikati ya jiji, wameripoti kushuhudia maduka yakiwa yamefungwa huku shughuli za uchukuzi zikiendelea kwenye baadhi ya mitaa ingawa ni tofauti na ilivyozoeleka.

Ulinzi uliimarishwa katikati ya jiji, ambapo baadhi ya raia waliojaribu kuandamana kwa amani walikamatwa na pilisi licha ya kuwa jana walitoa notisi ambayo idara ya polisi ilikiri kupokea kuhusu uwepo wa maandamano ya kuwakumbuka waliopoteza maisha mwaka 2024.

Awali kulikuwa na wasiwasi wa kutokea vurugu kutokana na madai ya uwepo wa makundi ya vijana wenye silaha waliolipwa na wanasiasa kuingilia maandamano ya leo, madai ambayo pia yalielekezwa kwa serikali kuwa iliandaa vijana kufanya vurugu.

Maadhimisho ya hivi leo yanafanyika kuwakumbuka raia zaidi ya 60 walioripotiwa kuuawa wakati wa maandamano ya mwaka 2024 ya kupinga serikali pamoja na muswada tata wa fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *