Mabao mawili ya Maabad Maulid na Saad Mwanza wa Coastal Union, yametosha kuizamisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kuendeleza presha kwa vijana hao wa Kocha Salum Mayanga.
Maabad ndiye alianza kuzitikisa nyavu za wapinzani kwa mpira wa penalti dakika ya 32, kisha Mwanza kuhitimisha karamu ya mabao kwa shuti kali nje ya eneo la hatari na kumpa tuzo ya mchezaji bora wa mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo Mei 13, 2026.
Ushindi huo unakuwa wa pili kwa ‘Wagosi’ hao na wa kwanza kwa Kocha Fikiri Elias katika mechi za ugenini na kufikisha pointi 25 ikikamata nafasi ya 10.
Katika mchezo huo, Mbeya City ilionekana kutumia nguvu nyingi ikilazimisha mashambulizi lakini kipa wa Coastal Union na mabeki wake walikuwa imara kuzuia hatari zote.
Matokeo hayo yanaifanya Mbeya City kubaki nafasi ya 14 kwa pointi 21 ikibakiza mechi saba sawa na wapinzani wao hao na mchezo ujao itakuwa ugenini dhidi ya Namungo.
Akizungumzia matokeo hayo, Mayanga amekiri kuwaweka katika hali mbaya akieleza kuwa walihitaji sana pointi tatu ili kujikwamua nafasi za chini huku akitaja uzembe na makosa binafsi kuwagharimu.
“Ni matokeo mabaya sana kwetu, vijana walijaribu lakini tumeruhusu mabao mepesi sana, tutaenda kujisahihisha ili kuona tunamalizaje ligi lakini haitakuwa kazi ndogo,” amesema Mayanga.
Kocha wa Coastal Union, Fikiri Elias amewapongeza nyota wake kwa kazi nzuri akieleza kuwa kabla ya mchezo huo walijiandaa kisaikolojia baada ya kupoteza mechi iliyopita ikiwamo hali ya hewa ya jijini Mbeya.
Hata hivyo, amesema licha ya ushindi huo kuongeza nguvu na matumaini, lakini vita ya kukwepa kushuka daraja haswa kwa timu zilizopo chini ni ngumu akiomba wadau na mashabiki wa soka kutazama zaidi ‘battle’ hiyo.
“Ni matokeo mazuri kwetu lazima niwapongeze wachezaji kwa kazi nzuri, lakini bado hatuko salama sana na tunahitaji ushindi zaidi, ukiangalia huko katikati ya msimamo na chini kuna ligi nyingine hata waandishi wa habari angalieni zaidi huko,” amesema Kocha huyo.