
Dar es Salaam. Wakati juhudi za kuwaunganisha watanzania wengi na huduma rasmi za kifedha zikiendelea kuongezeka, NCBA Bank Tanzania imesema matumizi ya teknolojia na ushirikiano na kampuni za simu yamekuwa nguzo muhimu katika kupanua ujumuishaji wa kifedha nchini.
Benki hiyo yenye matawi manane yaliyopo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Zanzibar inajivunia kufikia zaidi ya Watanzania milioni nane kupitia huduma ya M-Pawa inayowawezesha wateja kuweka akiba na kukopa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Alex Mziray wakati akizungumza na waandishi na viongozi wa Mwananchi Communications Limited (MCL) walipofanya mazungumzo katika makao makuu yaliyopo Tabata jijini hapa.
Amesema kupita huduma ya M-Pawa kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania wamefanikiwa kufikia mamilioni ya Watanzania wanaotumia simu za mkononi hatua inayorahisisha upatikanaji wa mikopo midogo, kuweka akiba na huduma nyingine.
“Hii inawezesha pia upatikanaji wa huduma nyingine za kifedha bila kulazimika kufika tawi la benki,” amesema.
Amesema hii ni ishara kuwa sekta ya benki imebadilika kwa kasi, na sasa ushindani mkubwa upo katika namna taasisi zinavyoweza kumfikia mwananchi wa kawaida kwa njia rahisi na ya haraka.
NCBA ilizaliwa baada ya muunganiko wa benki mbili ambazo ni NIC na Commercial Bank of Africa.
“Tunataka kujulikana zaidi kwa kile tunachofanya na namna tunavyoweza kusaidia wananchi. Siyo lazima uwe na uwezo mkubwa ndipo upate huduma za benki, hata mtu wa kawaida ana ndoto zake na sisi tunataka kumwezesha kuzifikia,” amesema Mziray.
Mbali na huduma za kifedha benki hiyo imekuwa ikitekeleza programu ya mafunzo kwa wahitimu wa vyuo vikuu ambapo huchukuliwa vijana 20 kila mwaka.
“Hatua hiyo inalenga kuwapa uzoefu wa kazi vijana wanaokabiliwa na changamoto ya kuhitaji kuwa na uzoefu kabla ya kuajiriwa. Programu hii inaweza kuwasaidia wahitimu kupata ajira au hata kujiajiri baada ya kujifunza namna mifumo ya biashara inavyofanya kazi,” amesema.
Haya yanasemwa wakati ambao taarifa ya robo ya kwanza ya mwaka ya benki hii inaonyesha kuwapo kwa ukuaji wa huduma za kifedha ikiwemo amana za wateja ambazo zilifikia Sh328.91 bilioni ikilinganishwa na Sh286.5 bilioni iliyokuwapo katika robo iliyoishia Desemba 31, 2025.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko kutoka NCBA Kenya, Hellen Wainaina amesema ongezeko la amana za wateja ni ishara kuwa wananchi wanaendelea kuiamini benki na huduma zake.
“Katika sekta ya fedha, amana za wateja si takwimu za kawaida bali ni kipimo cha imani ambayo wananchi wameiweka kwa taasisi husika kwa kukabidhi fedha zao,” amesema.
Amesema kuongezeka kwa amana kunaonyesha kuwa jamii imeendelea kuona benki kama sehemu salama ya kuhifadhi fedha, kufanya miamala na kupata suluhisho la kifedha.
“Mara zote ukuaji wa uchumi wa nchi huenda sambamba na uimara wa taasisi za kifedha kwani husisimua shughuli za biashara kuongezeka, ndivyo mahitaji ya mikopo, huduma za malipo na uwekezaji yanavyoongezeka,” amesema.
Kwa upande wake Meneja Rasilimali Fedha kutoka MCL, Amos Simiyu aliikaribisha benki ya NCBA kufanya kazi na Mwananchi kupitia huduma mbalimbali zinazotolewa ikiwemo usafirishaji mizigo, uchapishaji na utangazaji bidhaa zao.