Mwanza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka wasomi nchini kusimamia mabadiliko katika maeneo sita muhimu, yakiwamo ya utawala bora, usimamizi wa rasilimali za Taifa pamoja na kudai haki kwa sauti moja.
Akizungumza leo Jumatano Mei 13, 2026 katika kongamano la wasomi lililofanyika jijini Mwanza, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, amesema kila Mtanzania ana wajibu wa kupigania haki na kusimama pamoja na wanaoonewa, akieleza kuwa ukimya wa jamii unaweza kusababisha kila mmoja kuathirika baadaye.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) John Heche akiwasili kwenye Kongamano la Wasomi Jijini Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba
Heche amewataka wasomi kote nchini kutokaa kimya wanapoona watu wakionewa, kwa sababu ipo siku hali hiyo inaweza kuwageukia wao wenyewe.
“Mkikubali hali hii iendelee kwa kufikiria anayeumizwa au kuonewa, pengine ningepigana kama angekuwa ndugu yangu. Kesho yatamkuta mwingine naye atasema siyo mimi, siyo ndugu yangu wala baba yangu. Mwisho wa siku kila mmoja ataathirika kwa namna yake,” amesema Heche.
Wasomi wakisubiri kumpokea Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) John Heche kwa ajili ya Kongamano la Wasomi Jijini Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba
Ameongeza kuwa nchi ni ya Watanzania wote, hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha kila mtu anaheshimiwa na kupata haki zake bila ubaguzi.
“Hii nchi ni yetu sote, lazima tuiweke kwenye msingi ambao kila mtu anaheshimika. Vijana na wanafunzi wa vyuo vikuu wanapaswa kuelewa wajibu wao katika kuleta mabadiliko ya kweli nchini,” amesema.
Katika hotuba yake, Heche pia amewataka vijana na wasomi kupigania kupatikana kwa Katiba mpya, akisema suala hilo limekuwa likidaiwa tangu mwaka 1992.
Amesema kuchelewa kupatikana kwa Katiba mpya kumewafanya baadhi ya wananchi kupoteza imani na mchakato wa uchaguzi, hali iliyosababisha wengine kutoshiriki kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku wengine wakishiriki maandamano yaliyokuja kutafsiriwa kama vurugu.
“Tangu mwaka 1992 Watanzania wamekuwa wakihitaji Katiba mpya. Imefika hatua baadhi ya watu wanasema hawatakwenda kupiga kura kutokana na kukosa imani na mfumo uliopo,” amesema Heche.
Akizungumzia tume ya uchunguzi wa matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba, 2025, Heche amesema zama za sasa si za kuficha ukweli wala taarifa muhimu kwa wananchi, akisisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika uongozi wa nchi.
Kuhusu usimamizi wa rasilimali za Taifa, hususan sekta ya madini, kiongozi huyo amesema Tanzania bado haijanufaika ipasavyo na utajiri wake wa asili licha ya kuwa na madini ya aina mbalimbali.
“Botswana wana almasi pekee lakini wanaingiza takribani Sh10 trilioni kwa mwaka, wakati Tanzania yenye Tanzanite, almasi na madini mengine mengi inaingiza takribani Sh1 trilioni pekee. Sekta ya madini inachangia asilimia 11 ya pato la Taifa,” amesema Heche.
Aidha, amesema Chadema inataka kushika madaraka kwa njia ya kidemokrasia ili kuleta mabadiliko ya mfumo wa uongozi unaodaiwa kuwabagua vijana na watu wenye uwezo.
“Sina shida na Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) wala Mchengerwa (Waziri wa Afya), wala mtu mwingine yeyote binafsi. Tatizo letu ni mfumo wa uongozi unaotumika. Tunataka kujenga nchi ambayo mtu atapata nafasi kwa uwezo wake, elimu yake na kazi yake, si kwa upendeleo,” amesema Heche.
Ameongeza kuwa kuna haja ya vijana kuunganisha nguvu katika kupigania mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini.
“Tuna sababu ya kuunganisha nguvu ili kuleta mabadiliko katika nchi hii. Hatuwezi kuendelea kupambana kwa ajili yenu wakati wengine wanabaki watazamaji. Vijana, hatima ya maisha yenu ipo mikononi mwenu,” amesema.
Heche pia amewataka vijana kutokubali kuongozwa na viongozi wasiowajibika pamoja na kupinga matumizi mabaya ya fedha za Serikali.
“Mwanafunzi wa chuo kikuu anatakiwa kuwa mtetezi wa maslahi ya wanafunzi na jamii, si kuwa sehemu ya kusifia kila jambo bila kuhoji. Ili tubadilishe nchi hii, lazima tubadilishe mfumo uliopo,” amesema.
Makamu mwenyekiti wa chama hicho, John Heche akizungumza na wasomi kwenye kongamano la wasomi jijini Mwanza. PraiseGod Mgumba.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Salma Kasanzu, ameitaka Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kuhakikisha wanafunzi wote wa vyuo vikuu wanapatiwa mikopo kwa asilimia 100 bila ubaguzi.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu na kuondoa changamoto zinazowafanya baadhi yao kushindwa kuendelea na masomo.
“Bodi ya mikopo ihakikishe wanafunzi wote wa vyuo vikuu wanapata mikopo kwa asilimia 100 ili vijana wasome kwa utulivu na kuendelea kujenga taifa la kesho,” amesema Kasanzu.