Morogoro. Dereva wa bodaboda aliyefahamika kwa jina la Ally Kambi (24), mkazi wa Kingolwira Manispaa ya Morogoro, anadaiwa ameuawa kisha kuporwa pikipiki na watu ambao bado hawajajulikana waliomkodi eneo la Mkono wa Mara, Wilaya ya Morogoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo amethibitisha kutokeamauaji hayo na amesema wanaendelea na uchunguzi ili kubaini waliohusika kufanya mauaji hayo.
Akisimulia tukio hilo, baba mkubwa wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Shukuru Msonga amesema kijana wake huyo alikodiwa na mtu asiyefahamika Mei 11, 2026 majira ya usiku na hakuweza kurudi tena hadi Mei 13, mwili ulipokutwa porini eneo la Mkono wa Mara ukiwa na majeraha.
“Baada ya kutoonekana nyumbani kwa siku nzima, tulikwenda kutoa taarifa kwa Serikali ya mtaa na kituo cha polisi ambapo kazi ya kumtafuta ilianza. Tulihangaika kumtafuta maeneo mbalimbali, tulifika mpaka hospitali, tulitangaza kwenye vijiwe vyote vya bodaboda, hatimaye jana majira ya asubuhi tukapata taarifa kuwa kuna mwili umeonekana porini,” amesema Msonga.
Amesema baada ya yeye pamoja na ndugu wengine kufika eneo la tukio, waliukuta mwili ambao waliutambua kuwa ni wa kijana wao huyo ukiwa na majeraha na pembeni kulikuwa na fimbo kubwa (gongo) pamoja na fulana iliyoloa damu.
Marehemu Ally Kambi (24) enzi ya uhai wake
Aidha amesema kuwa watu waliofanya mauaji hayo walichukua pikipiki ya marehemu, fedha kiasi ambacho bado hakijafahamika pamoja na simu.
Mjomba wa marehemu, aliyejitambulisha kwa jina la Ahmed Ramadhani amesema alipata taarifa za kupotea kwa mpwa wake Mei 11 na baada ya kupata taarifa hizo alianza jitihada za kumtafuta mpaka jana ndipo walipopata taarifa kuwa mwili umeonekana porini maeneo ya Mkambarani.
“Kifo ni kifo na kila mtu atakufa lakini kifo hicho kilichomkuta mpwa wangu kwa kweli kinatia uchungu na kimetuumiza kwa sababu amedhurumiwa nafsi pamoja na mali yake ambayo ni pikipiki. Mpwa wangu alikuwa kijana makini, mpole na asiyependa ugomvi na mtu. Ameacha pengo na wategemezi ambao ni mke na watoto,” amesema Ramadhani.
Baadhi ya madereva wa bodaboda waliokuwa wakiegesha kijiwe kimoja na marehemu wamesema marehemu enzi za uhai wake hakuwa na kawaida ya kukaa kijiweni mpaka usiku. Alikuwa akirudi nyumbani mapema na ndiyo maana alipotoweka siku ya tukio walipata wasiwasi mapema na kuanza kumtafuta.
Mmoja wa madereva hao wa bodaboda, Fadhil Shabaani amesema siku ya tukio Ally alitoka kwenye kijiwe alichokuwa akiegesha eneo la Kingolwira Stendi akiwa na abiria na baada ya hapo hakuweza tena kurudi. Ilipofika asubuhi walipata taarifa kuwa hata nyumbani kwake pia hakurudi.
“Asubuhi ya Mei 12 ndipo niliposikia kuwa Ally anatafutwa na sisi wote kama madereva, majirani na marafiki tuliungana na familia kuanza kumtafuta. Jana asubuhi ndipo tulipopata taarifa nyingine kuwa mwili wake umeonekana porini na kwamba ameporwa pikipiki. Baba yake pamoja na ndugu walikwenda kuangalia mwili na kweli walituthibitishia kuwa ni wa Ally,” amesema Shabaani.
Mwili wa dereva wa bodaboda Ally Kambi (24) anayedaiwa kuuawa na watu wasiojulika wilaya ya Morogoro ukiingizwa kwenye gari kwenda kuzikwa. Picha Hamida Shariff
Ameongeza kuwa bodaboda aliyokuwa akiendesha marehemu ilikuwa ya mkataba na kwamba marehemu alipewa na rafiki yake ili amfanyie kazi kwa siku kadhaa halafu amrudishie mwenyewe mwenye mkataba.
Amesema matukio ya kuuawa na kuporwa pikipiki madereva wa bodaboda wa Kingolwira kwa muda mrefu yalitoweka na ndiyo maana madereva wengi walijisahau na kumuamini kila abiria anayekuja kukodi boda. Hata hivyo, ameeleza kuwa kwa tukio hilo la leo wamepata hofu na litawafanya waongeze umakini.