
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron siku ya Jumatano amehitimisha ziara yake ya barani Afrika kwa mazungumzo nchini Ethiopia, hasa akizungumzia suala la muda mrefu la uwakilishi wa Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Rais Emmanuel Macron alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na baadaye alikutana na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mahamoud Ali Youssouf na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, na kwa pamoja walijadili utawala jumuishi wa kimataifa.
Viongozi hao “walitambua hitaji la uwakilishi wa Afrika,” kulingana na taarifa iliyosomwa kutoka kwenye mkutano huo.
Rais Macron, ambaye alizuru Misri, Kenya na Ethiopia wakati wa ziara yake barani Afrika, alitaka uwakilishi bora wa Afrika katika taasisi za kimataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wakati wa hotuba yake ya ufunguzi katika Mkutano wa kiuchumi kati ya Afrika na Ufaransa, Africa Forward, ulioandaliwa kwa pamoja na Ufaransa na Kenya na kufanyika kwa mara ya kwanza katika nchi inayozungumza Kiingereza, Macron alitambua hitaji la viti vya kudumu vya Afrika katika baraza hilo.
Tamko la amani na usalama lililotolewa mwishoni mwa mkutano huo pia lilitaka “hitaji la dharura la mageuzi kamili ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kulifanya liwe na ufanisi zaidi na uwakilishi zaidi.”
Utafutaji wa viti vya kudumu wa Afrika umekuwa ukitegemea hitaji la kuakisi hali halisi ya kisasa ya kimataifa, huku mashirika ya bara hilo yakikosoa kutengwa kwa bara lenye watu zaidi ya bilioni 1.4 kutoka kwa nguvu ya kudumu ya kufanya maamuzi.
Siku ya Jumatano Antonio Guterres alisema kwamba dunia ingefaidika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalojumuisha wote.
“Baraza la Usalama ambalo, leo, haliwakilishi hali halisi ya dunia kijiografia. Tuna wanachama watatu wa kudumu kutoka Ulaya, mmoja kutoka Amerika Kaskazini, na mmoja kutoka Asia.” “Amerika ya Kusini, na Afrika hawawakilishwi: hili ni Baraza la Usalama linalokumbwa na tatizo la uhalali, na kwa hivyo, tatizo la ufanisi,” alisema.
Baada ya mkutano kati ya Macron na Abiy, makubaliano mapya ya ufadhili wa mkopo yenye thamani ya dola milioni 63.9 kwa ajili ya uwekezaji wa nishati ya kijani na mpango wa kidijitali wa Ethiopia yalitangazwa.
Wakati wa Mkutano wa Africa Forward, Macron alisema kwamba serikali ya Ufaransa na sekta binafsi zitahamasisha uwekezaji wenye thamani ya dola bilioni 27 ili kuchochea ukuaji jumuishi kote barani.