
Nyota wa Real Madrid, Kylian Mbappe na staa wa PSG, Ousmane Dembele ni majina makubwa ambayo yatakiongoza kikosi cha Ufaransa kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu huko Marekani, Canada na Mexico.
Wawili hao ni miongoni mwa majina 26 yanayounda kikosi ambacho kimetangazwa leo na Meneja wa timu hiyo Didier Deschamps kikiwa na nyota wanaotamba katika klabu mbalimbali barani Ulaya.
Kiwango bora msimu cha nyota wa Manchester City, Rayan Cherki kimemlipa mchezaji huyo kwa kupata uteuzi katika kikosi hicho cha Ufaransa ambacho ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.
Kocha Deschamps amefanya uamuzi uliotegemewa na wengi wa kumjumuisha kikosini kipa wa Lens, Robin Risser ambaye amekuwa na msimu wa kihistoria katika Ligi Kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’.
Akicheza kwa mara ya kwanza katika Ligi hiyo, Risser amefanikiwa kutwaa tuzo ya Kipa Bora msimu huu na Deschamps amemuongezea wasifu kwa kumjumuisha katika kundi la makipa watatu atakaopanda nao ndege kwenda Kombe la Dunia.
Imekuwa ni siku ngumu kwa mshambualiaji wa Tottenham Hotspur, Randal Kolo Muani na kiungo wa Real Madrid, Eduardo Camavinga ambao wametoswa na Deschamps.
Kolo Muani ndiye alifunga moja kati ya mabao ya Ufaransa katika ushindi wa mabao 2-0 ambao iliupata katika nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022 dhidi ya Morocco.
Ni kikosi kinachotegemewa kuwa cha mwisho kuitwa na Deschamps kwani baada ya Kombe la Dunia 2026, Kocha huyo hatoendelea kuifundisha timu hiyo na nafasi yake itachukuliwa na Zinedine Zidane.
Makipa wanaounda kikosi hicho ni Mike Maignan, Brice Samba na Robin Risser huku mabeki wakiwa ni Lucas Digne, Malo Gusto, Lucas Hernandez, Theo Hernandez, Ibrahima Konate, Jules Kounde, Maxence Lacroix, William Saliba na Dayot Upamecano.
Viungo wanaounda kikosi hicho ni N’Golo Kante, Manu Kone, Adrien Rabiot, Aurelien Tchouameni na Warren Zaire-Emery.
Washambuliaji ni Maghnes Akliouche, Bradley Barcola, Rayan Cherki, Ousmane Dembele, Desire Doue, Jean-Philippe Mateta, Kylian Mbappe, Michael Olise na Marcus Thuram.
Ufaransa katika Fainali za Kombe Dunia 2026 imepangwa katika kundi I na timu za Senegal, Norway na Iraq.
Itafungua dimba dhidi ya Senegal, Juni 16 kisha itacheza na Iraq, Juni 23 na itamaliza hatua ya makundi kwa kucheza na Norway, Juni 26.