Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, amesisitiza uungaji mkono wa nchi yake kwa haki ya Wapalestina ya kuanzisha nchi yao wenyewe, akitoa maoni yake kuhusu utata uliosababishwa na hatua ya nyoka wa timu ya soka ya Barcelona, Lamine Yamal, wakati timu yake ilipokuwa ikisherehekea taji la ubingwa wa ligi ya Uhispania.
Yamal alionekana katika video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, akipeperusha bendera ya Palestina ndani ya basi la wazi. Picha hizo zimevutia mazingatio makubwa ya duru za kisiasa na vyombo vya habari ndani na nje ya Uhispania.
Akizungumzia suala hilo katika mkutano wa waandishi wa habari akiwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Pedro Sanchez amesema: “Palestina ina haki zote za kuwepo,” na amekumbusha kwamba nchi yake tayari imeitambua rasmi Nchi ya Palestina.
Sanchez amelaani “mauaji ya kimbari” yanayofanywa na jeshi la Israel na serikali ya kivamizi inayoongozwa na Benjamin Netanyahu katika Ukanda wa Gaza. Pia amepinga shughuli za kuwapa walozi wa Kizayuni makazi katika Ukingo wa Magharibi, akilielezea jambo hilo kuwa ni “uvamizi haramu.”
Waziri Mkuu wa Uhispania amesisitiza kwamba “kuendelea kwa vita huko Gaza sio tu kwamba kunatishia usalama wa Mashariki ya Kati lakini pia kuna athari mbaya kwa jamii ya Israel.” Vilevile ametoa wito wa kuheshimiwa sheria za kimataifa na kukomeshwa kwa vita.

Pedro Sanchez ametoa wito kwa Netanyahu kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Ukanda wa Gaza na kufanya kazi ili kukomesha mtindo wa kukwepa adhabu.
Picha ya Lamine Jamal akiwa na bendera ya Palestina imefungua tena mjadala kuhusu nafasi ya wanariadha katika masuala ya kisiasa na kijamii, hasa wale wenye ushawishi wa vyombo vya habari unaofikia hadhira kubwa duniani.
Lamine Jamal ana wafuasi milioni 42 kwenye Instagram na ana ushawishi mkubwa kwa mamilioni ya watu kote duniani hususan tabaka la vijana na washabiki wa soka.
Miongoni mwa watu wa kwanza kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii kuhusu tukio hilo ni mwanasiasa wa Uhispania, Gabriel Ruffian, ambaye amesifu kitendo cha mchezaji huyo wa soka wa kimataifa wa mpira wa miguu.
El Mundo imeripoti kuwa, si kawaida kwa wanasoka wa Uhispania, hasa vijana, kuchukua msimamo wa kisiasa kuhusu masuala nyeti kama vile kadhia ya Palestina, na kwa sababu hii, hatua ya ujasiri ya Yamal imepewa mazingatio makubwa.