
Mamia ya wanachama wa Muungano wa Kimataifa wa Wanasayansi Duniani wameandika barua ya wazi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UNESCO, na Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wakitaka kulindwa taasisi za kisayansi nchini Iran, na pande vamizi yaani Marekani na Israel ziwajibishwe.
Barua hiyo imeanza kwa kusema: “Sisi, wasomi, watafiti, wanafunzi na wanachama wa jamii ya wasomi duniani tunaeleza wasiwasi wetu kuhusu mashambulizi yasiyopungua 21 ambayo yameharibu maabara, vyuo vikuu, hospitali na taasisi nyingine za kisayansi wakati wa mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Barua hiyo ya wanasayansi zaidi ya 1,000 imeeleza kuwa: Mashambulizi ya Marekani na Israel yamekilenga Chuo Kikuu cha Ufundi cha Isfahan, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amirkabir.
Barua hiyo imeongeza kuwa: Taasisi za kisayansi na elimu ni maeneo ya kiraia ambayo ni muhimu kwa afya ya umma, maarifa na maisha ya binadamu, na kwamba uharibifu wa hujuma za Marekani na Israel ni hatari kwa watafiti, wanafunzi, wafanyakazi wa sekta ya afya na umma kwa ujumla na unaacha madhara ya kudumu kwa sayansi na jamii.