
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa kulengwa kwa viwanja vya michezo na miundombinu ya umma na Marekani pamoja na Israel wakati wa vita vya uchokozi kumefichua uadui wa washambuliaji hao dhidi ya heshima, furaha na fahari ya taifa la Iran.
Pezeshkian ametoa kauli hiyo Alhamisi alipokuwa akitembelea ukumbi wa michezo wa Azadi wenye uwezo wa kuchukua watu 12,000 mjini Tehran, ambao ulishambuliwa na Marekani pamoja na Israel tarehe 5 Machi na kuharibiwa kabisa.
Aliwataka maafisa wa michezo na wasimamizi wa uwanja wa Azadi kuharakisha shughuli za ujenzi upya, kurejesha kikamilifu miundombinu iliyoharibiwa, na kusisitiza umuhimu wa kulinda kwa kiwango cha juu maeneo yote ya michezo nchini humo.
Aidha amebainisha masikitiko yake makubwa kufuatia mashambulizi dhidi ya viwanja vya michezo na miundombinu ya umma nchini Iran wakati wa vita vya siku 40 kati ya Marekani na Israel vilivyoanza tarehe 28 Februari.
Rais Pezeshkian amesisitiza kwamba mashambulizi dhidi ya viwanja vya michezo si suala la kuharibu majengo pekee, kwani maeneo hayo ni sehemu ya kumbukumbu ya kihistoria, utambulisho wa taifa, pamoja na alama ya juhudi, matumaini na fahari ya vijana wa Iran.
Akizungumzia nafasi maalum ya uwanja wa Azadi katika historia ya michezo ya Iran, rais amesema kulengwa kwa eneo hilo kunaonyesha wazi kuwa maadui wa taifa la Iran hawana uadui tu dhidi ya uwezo wa nchi hiyo wa kujilinda na maendeleo ya kisayansi, bali pia dhidi ya kila alama ya heshima na hadhi ya taifa hilo.
Katika barua aliyomwandikia Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), Kirsty Coventry, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran Ahmad Donyamali alisema, akitoa ushahidi wa nyaraka mbalimbali, kuwa mashambulizi ya Marekani na Israel yalilenga moja kwa moja miundombinu ya michezo ya Iran
Kwa mujibu wa Donyamali, mashambulizi hayo yalisababisha kuharibiwa kabisa kwa ukumbi wa watu 12,000 wa Azadi pamoja na kuathiri vituo vingine 287 vya michezo kote nchini.
Aidha alisema mashambulizi hayo yalisababisha pia hasara kubwa ya maisha ya watu, ikiwemo vifo vya wanamichezo 203, wakiwemo wanawake 16 na wanaume 187.