Geita. Wakazi wa Halmashauri ya Nyang’hwale wameendelea kunufaika na miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) baada ya kampuni ya Barrick kupitia mgodi wa Bulyanhulu kutoa shilingi milioni 401 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika Shule ya Sekondari ya Nyang’hwale.

Fedha hizo zitatekeleza mradi wa Barrick-Twiga Future Forward Education Programme unaohusisha ujenzi wa mabweni mawili, madarasa matano na matundu ya vyoo manane kwa ajili ya wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita katika shule hiyo ya serikali mkoani Geita.

Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi imefanyika shuleni hapo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Meneja Mkazi wa Barrick Gold Corporation nchini, Dk Melkiory Ngido, ikihudhuriwa na viongozi wa serikali, wananchi na wanafunzi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Ngido alisema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuchochea maendeleo ya jamii kupitia sekta mbalimbali, hususan elimu, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Alisema elimu ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya elimu unachangia kujenga maarifa, fursa na mustakabali bora wa vijana wa Kitanzania.

Katika hatua nyingine, Dk Ngido alisema Barrick kupitia mpango huo wa elimu uliyozinduliwa mwaka 2023, umeahidi kutoa Dola milioni 30 za Marekani kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule nchini, ambapo lengo ni kujenga madarasa 1,090, mabweni 270 na matundu ya vyoo 1,640 katika shule 161.

Alifafanua kuwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo, shule 64 zilinufaika, huku awamu ya pili ikiwa imefikia zaidi ya asilimia 83 ya utekelezaji, na tayari Shule ya Nyang’hwale imeshalipwa zaidi ya shilingi milioni 304, ikiwa ni asilimia 76 ya fedha za mradi wake.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Kaunga Amani, aliishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wanaochangia maendeleo ya wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Husna Toni, aliishukuru kampuni ya Barrick kwa mchango wake, akisema utasaidia kuboresha ufaulu na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *