KOCHA Mkuu wa KenGold, Jumanne Challe amesema ni ngumu kwa timu hiyo kushika nafasi nne za juu zitakazoiwezesha kucheza mechi za ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao, kutokana na ushindani wa wapinzani wao na mwenendo wa kikosi hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Challe amesema malengo ya timu hiyo mwanzoni yalikuwa ni kumaliza nafasi nne za juu, ingawa, kwa hali ilivyo na mwenendo wao ni ngumu kufikia kile walichokusudia, licha ya kubakia mechi sita kabla ya msimu kuisha.
“Ushindani na wapinzani wetu ni mkubwa sana na gepu lililopo la pointi ni ngumu kuwafikia, hii inatokana na kutokuwa na mwenendo mzuri hasa tunapocheza viwanja vya nyumbani ambavyo ni muhimu sana kwa Ligi ya Championship,” amesema Challe.
Kocha huyo amesema hali hiyo imechangia kurudisha nyuma maendeleo ya kikosi hicho msimu huu, ingawa anaendelea kupambana kwa mechi zilizobakia, hususani kutengeneza balansi nzuri kwenye eneo la kujilinda ambalo ndilo limekuwa na changamoto.
Baada ya msimu bora wa 2023-2024, mashabiki na wapenzi wa soka hususani wa jijini Mbeya walitarajia KenGold ingeendeleza ilichokifanya katika Ligi ya Championship, japo baada ya kupanda daraja mambo yalikuwa ni tofauti na kurejea ilipotoka.
Msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya jijini Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, ikirejea Ligi Kuu baada ya miaka 21 tangu iliposhuka mwaka 2001.
Licha ya kiwango bora, ila KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu, ambapo msimu wa 2024-2025, iliburuza mkiani na pointi 16, ikishinda mechi tatu tu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza ya 15 na pointi 23.
Msimu huu wa 2025-2026, KenGold imeshinda mechi nane, ikitoka sare sita na kupoteza 10 kati ya 24, ikiwa nafasi ya saba na pointi 30, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 25 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa pia mara 29.