Dodoma. Kauli ya gharama za kumuona daktari kwa wagonjwa, imewaibua madaktari na kueleza kinachoendelea huku wakionya siasa zisiingizwe kwenye afya za watu.

Tozo za wagonjwa kuwaona madaktari ziliibuliwa mwanzoni mwa wiki wakati wa kuchangia hotuba ya Wizara ya Afya ambapo walilalamikia kuwa tozo hizo zinawaongezea gharama na mzigo mkubwa wagonjwa.

Wabunge walioibua hoja hiyo ni Mwita Waitara na Mwita Getere waliosema gharama za kuwaona madaktari ni kilio cha maumivu na mzigo mkubwa kwa wenye kipato cha chini.

Akizungumza leo, Rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema kauli hiyo ni ya kuwavunja moyo madaktari na inawarudisha nyuma katika kazi hiyo ya wito.

Dk Nkoronko amesema hakuna ukweli wala uthibitisho wa namna yoyote kwamba gharama hizo zimekuwa zikipelekwa kwa moja kwa moja kwa madaktari badala yake ni tozo za Serikali katika matibabu.

Rais huyo amesema hakuna daktari wa kituo au hospitali ya umma ambaye anaweza kupokea mkononi mwake tozo za namna yoyote bali kila kitu kinalipwa serikalini kwa kutumia namba za malipo na fedha hiyo inafanya huduma katika hospitali na vituo vya afya.

“Kauli ile ilileta mjadala mkubwa kwa MAT na hasa ilipochagizwa kwenye mitandao ya kijamii, kwa hakika inatuvunja moyo kwenye utumishi wetu, lakini wanasahau kuwa ni wao watunga sera ndiyo waliweka hilo halafu leo wanatutupia sisi,” amesema Dk Nkoronko.

Hata hivyo, ameonya wanasiasa kuacha kulinganisha taaluma ya udaktari na alichokisema ni bei ya nyanya badala yake waendelee kuheshimu na kuthamini kama ambavyo Serikali imekuwa ikiwaheshimu na kutumia gharama kubwa kuwaandaa.

Kwa mujibu wa daktari huyo, kazi kubwa waliyonayo kwa sasa ni kuendelea kuhudumia wananchi na kusaidia kurudisha uhai na afya zao na kwamba hadi sasa daktari mmoja bingwa anaona wagonjwa kati ya 35 hadi 40 kwa siku kiwango ambacho ni cha juu ukilinganisha na mataifa mengine.

“Kubwa mimi nawapa lawama viongozi wetu wa siasa, wao wameweka afya kuwa kipaumbele cha chini wakatanguliza vingine, wangeweka kiwe cha kwanza haya yasingeweza kujitokeza, nawasihi madiwani na wabunge watupe nafasi tuwahudumie Watanzania,” amesema.

Kuhusu nini kifanyike kupunguza gharama hizo, amesema Bima ya afya kwa wote ndiyo suluhisho la moja kwa moja kwani litakwenda kufuta kila kero ambayo inalalamikiwa na pande zote watakuwa kwenye mstari mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *