
Arusha. Waonyeshaji Zaidi ya 500 wanatarajiwa kushiriki maonyesho ya kimataifa ya utalii ya Karibu-Kilifair 2026, yanayolenga kukuza biashara ya utalii kimataifa kwa kutangaza vivutio vya vilivyopo nchini.
Aidha, wanunuzi wa kimataifa wasiopungua 1,000 kutoka zaidi ya nchi 40 wanatarajiwa kuhudhuria maonyesho hayo makubwa ya utalii Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa leo Mei 14, 2026 na Mkurugenzi wa kampuni ya Kilifair Promotion, Dominic Shoo wakati akizungumzia maandalizi ya maonyesho hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 4 hadi 6, 2026 katika viwanja vya Magereza jijini Arusha.
Amesema maandalizi ya maonyesho hayo yamekamilika na kwamba mwaka huu yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika tangu kuanzishwa kwake.
Shoo amesema lengo kuu la maonyesho hayo ni kuwakutanisha wadau wa sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania chini ya jukwaa moja ili kujenga mtandao wa biashara na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vyake vya utalii.
Amesema kupitia maonyesho hayo, washiriki watapata nafasi ya kufanya mikutano ya kibiashara, kubadilishana uzoefu pamoja na kutangaza bidhaa mbalimbali za utalii, zinazopatikana Tanzania na nchi nyingine zinazoshiriki.
“Mwaka huu tuna waonyeshaji wasiopungua 546 kutoka nchi 13 na wanunuzi wa kigeni wasiopungua 1,000 kutoka zaidi ya nchi 40. Katika siku hizi nne, watu watafanya networking kubwa na kujenga uhusiano mpya wa kibiashara,” amesema Shoo.
Ametaja nchi 14 zinazoshiriki kuwa ni Tanzania, Ujerumani, Zanzibar, Uganda, Nigeria, Afrika Kusini, Uturuki, Kenya, Zimbabwe, Rwanda, Ethiopia, Zambia na Ghana.
Shoo amesema maonyesho hayo yatafunguliwa rasmi Juni 5, 2026 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji na kuwa miongoni mwa mambo yatakayofanya maonyesho ya mwaka huu kuwa ya kipekee ni uwepo wa vivutio vipya, ikiwemo uzoefu wa kupanda Mlima Kilimanjaro ndani ya viwanja vya maonyesho.
Kwa mujibu wa Shoo, washiriki watapata nafasi ya kushiriki shindano maalumu la kupanda Mlima Kilimanjaro, litakalompa mshindi safari ya kupanda mlima huo au zawadi ya fedha taslimu Sh1 milioni.
Amesema hatua hiyo inalenga kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro huku ikiibua hamasa mpya kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi huyo amesema siku ya kwanza ya maonyesho itahusisha zaidi waonyeshaji pamoja na wanahabari huku siku zinazofuata zikitarajiwa kuwa na mikutano ya biashara, mawasiliano ya wadau wa utalii pamoja na shughuli mbalimbali za kutangaza vivutio vya utalii.
“Tunaamini ongezeko la watalii wanaokuja Tanzania linachangiwa kwa kiwango kikubwa na maonyesho haya kwa sababu tunawakutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali na kuwapa nafasi ya kuiona Tanzania kama kituo muhimu cha utalii,” amesema Shoo.
Mbali na sekta ya utalii, Shoo amesema maonyesho hayo pia yatakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Arusha kutokana na ongezeko la wageni wanaohudhuria kila mwaka.
Katika hatua nyingine, Shoo amesema mwaka huu waandaaji wameanzisha rasmi kipengele cha utalii wa michezo kwa kushirikiana na mwanariadha maarufu wa Tanzania, Alphonce Simbu.
Amesema Simbu atatumika kama balozi wa kuhamasisha utalii wa michezo nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupanua aina za bidhaa za utalii zinazotangazwa kupitia maonyesho hayo.
Kwa upande wake, mdau wa utalii nchini, Timothy Mdinka amesema maonyesho hayo yana manufaa makubwa kwa wadau wa ndani kwa sababu yanawapa nafasi ya kukutana na wanunuzi wa kimataifa bila kutumia gharama kubwa za kusafiri nje ya nchi.
Mdinka amesema wadau wa utalii kutoka Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wanapaswa kutumia vizuri maonyesho hayo kutangaza bidhaa zao na kujenga ushirikiano wa kibiashara.
Amesema hatua ya kuanzishwa kwa vipengele vipya kama utalii wa michezo na utalii wa utamaduni itaongeza thamani ya maonyesho hayo na kusaidia Tanzania kuvutia watalii wengi zaidi kutoka mataifa mbalimbali duniani.