Dar es Salaam. Staa wa Bongofleva, Chege ni kati ya wanamuziki wanaounda kundi maarufu nchini la TMK Wanaume Family ambalo alijiunga nalo mwaka 2002, lakini amepata mafanikio makubwa kupitia kazi zake binafsi.
Kazi yake ya kwanza binafsi iliyompatia mafanikio makubwa ni Twenzetu (2005), wimbo uliotayarishwa na Miikka ‘Mwamba’ Kari chini ya MJ Records, huku akiwashirikisha Mhe. Temba, Ferooz na YP.
Hata hivyo, Chege ambaye jina lake limetokana na kitabu cha Ngugi wa Thiong’o, The River Between (I995), baadaye alijenga utamaduni wa kuwashirikisha wasanii wa kike katika nyimbo zake kama ifuatavyo.
Lady Jaydee – Aprili 2010
Kipindi Lamar akiwa juu zaidi kama mtayarishaji muziki, ndipo alipata nafasi ya kutengeneza wimbo wa Chege akimshirikisha Lady Jaydee, Mambo Bado (2010) ambao ulifanya vizuri wakati huo.
Wimbo huu ambao video yake iliongozwa na Director John Kallage, ulitayarishwa studio kwa Lamar, Fishcrab, ikiwa ni baada ya mtayarishaji huyo kuachana na Bongo Records, 41 Records na Sharobaro Records.
Hadi sasa hii ni moja ya kolabo kubwa za Chege kwa kuzingatia ukubwa wa Lady Jaydee ambaye alitoka kimuziki kupitia wimbo wake, Machozi (2000) chini ya MJ Records, na hadi sasa akiwa ameachia albamu 10 huku 11 ikitarajiwa 2027.
Malaika – Februari 2013
Mara baada ya kushirikishwa na Chege katika wimbo wake, Uswazi Take Away (2014), ndipo Malaika alivuma kimuziki kabla ya kuanza kutoa kazi zake binafsi zilizopaisha zaidi jina lake.
Wimbo huo ulitayarishwa na Tudy Thomas pamoja na Dunga, huku video yake ikiongozwa na Director Adam Juma wa Visual Lab: Next Level, ambapo Malaika aliwahi kufanya kazi.
Malaika anatajwa kama msanii wa kwanza wa kike Tanzania kutoka kwenye Bongofleva kufanya muziki aina ya Mchiriku, ni baada ya kutoa wimbo wake, Mwantumu (2014) akiwa na Chande na Tin White.
Nandy – Januari 2017
Takribani miezi saba baada ya Nandy kutoka na wimbo wake, Nagusagusa (2016) chini ya Tanzania House of Talent (THT), Chege tayari akaona wanaweza kufanya kazi pamoja licha ya kutokuwa na jina kubwa.
Mara moja Chege akamshirikisha Nandy katika wake, Kelele za Chura (2017) ambao ulitayarishwa na watayarishaji muziki wawili, Jobanjo na Lazier, huku video yake ikiongozwa na Director Destro.
Na hii ndio kolabo kubwa ya kwanza ya Nandy ambaye kwa sasa ni miongoni mwa wasanii wa kike wanaofanya vizuri Afrika Mashariki akiwa ameshinda tuzo nne za Muziki Tanzania (TMA) kuanzia msimu wa 2021.
Ray C – Julai 2017
Akiendelea kupata mafanikio kupitia kazi binafsi baada ya kulipa kundi mgongo, ndipo Chege alimshirikisha Ray C katika wimbo wake, Najiuliza (2017) uliotayarishwa Wasafi Records.
Ngoma hiyo ambayo Sanapei Tande pia alisikika, ilipita katika mikono ya watayarishaji wawili ambao ni Laizer na Dunga kutokea Kenya, huku video ikisimamiwa na Kwetu Studios.
Haya yalikuwa ni mafanikio mengine kwa Chege kufanya kazi na mwimbaji mkubwa wa kike kama Ray C ambaye alitoka na albamu yake, Mapenzi Yangu (2003) chini ya Smoth Vibes.
Saida Karoli – Februari 2018
Hapa kwa Saida Karoli, tunaweza kusema Chege alitaka kuendelea kuupa heshima kubwa muziki wake kutokana kile ambacho tayari Saida amekifanya hasa kupitia nyimbo zake za asili.
Chini ya utayarishaji wake Mocco Genius, Chege akamshirikisha Saida Karoli katika wimbo wake, Kaitaba (2018), ambao video yake iliongozwa Director Hanscana.
Mashabiki wengi wanamkumbuka Saidi Karoli kupitia wimbo wake, Maria Salome (2001) maarufu kama Chambua kama Karanga, ambao ulitayarishwa FM Studio na Miikka ‘Mwamba’ Kari kutokea Finland.
Vanessa Mdee – Aprili 2019
Mwaka mmoja kabla ya Vanessa Mdee kutangaza kuachana kabisa na muziki wa Bongofleva, ndipo Chege alimpa nafasi katika ngoma yake, Manjegeka chini ya Ziiki Media Productions.
Vanessa a.k.a Vee Money, katika kolabo hiyo na Chege alionyesha uwezo mkubwa wa kuimba pamoja na kucheza kama inavyoonekana katika video yake iliyosimamiwa na Hanscana.
Hadi anaacha muziki, Vanessa alikuwa ameshinda tuzo tatu za TMA, akishinda kipengele cha Wimbo Bora wa RnB (Closer) 2014, kisha Msanii Bora wa Kike na Mtumbuizaji Bora wa Kike 2015.
Phina – Septemba 2021
Takribani miaka mitatu baada ya Phina kuibuka mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2018, ndipo Chege akamshirikisha Phina katika wimbo wake, Kushki (2021).
Haikuishia hapo, miezi michache baadaye Phina alikuja kusikia katika ngoma nyingine ya Chege, Sinsima (2021) iliyotayarishwa na Mr. T Touch, huku video ikisimamiwa na Director Yuzzo.
Phina, mshindi wa TMA mara nne, bado anashikilia rekodi kama mwanamuziki pekee aliyeibuliwa na shindano la BSS ambaye ameshinda tuzo hizo mara nyingi zaidi kwa muda wote.
