Taraji P. Henson ampa maua bibi yake wa miaka 102Taraji P. Henson ampa maua bibi yake wa miaka 102

Marekani. Mwigizaji wa Marekani, Taraji P. Henson (55), ameeleza jinsi bibi yake mwenye umri wa miaka (102), Patsie Ballard, alivyochangia kwa kiasi kikubwa kuamini kuwa anaweza kuitimiza ndoto yake ya kuwa mwigizaji mkubwa.

Taraji, mkali wa filamu ya Acrimony (2018), amefunguka hayo katika mahojiano yake mpya wiki hii wakati akizungumzia tamthilia yake mpya, Joe Turner’s Come and Gone.

Amesema bibi yake huyo ambaye alizaliwa mwaka 1924, naye anatarajiwa kwenda kuitazama tamthilia hiyo ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi.

Ilizinduliwa rasmi Aprili 25, 2026 na inatarajiwa kuendelea kuoneshwa hadi hapo Julai 26, jijini New York katika ukumbi wa Ethel Barrymore Theatre.

“Bibi yangu ametimiza umri wa miaka 102 na anakuja kutazama tamthilia hii. Alizaliwa mwaka 1924, jambo ambalo linanishangaza sana,” alisema Taraji.

Mwigizaji huyo alieleza kuwa watu wa kizazi cha bibi yake hawakuwa na nafasi kubwa ya kujichagulia ndoto ya kuzifikia kama ilivyo kwa watoto wa leo.

Lakini licha ya hali hiyo, Ballard alimpa uhuru wa kuonesha ubunifu wake alipokuwa akikaa kwa babu na bibi zake huko North Carolina wakati wa likizo.

“Hakuniruhusu tu kuwa na ndoto ya kuja kuwa mwigizaji, bali pia aliniruhusu kuigiza wahusika mbalimbali, kuimba mbele ya kioo na kuamini kipaji changu,” alisema.

Taraji alisema upweke aliokuwa nao kipindi hicho ulimsaidia kukuza kipaji chake cha uigizaji kwani muda mwingi aliutumia kubuni wahusika tofauti tofauti.

Kutokana na mchango mkubwa wa bibi yake katika maisha yake, Taraji amesema alimpeleka kwenye hafla ya tuzo za Oscars 2009, ambapo aliteuliwa kuwania tuzo kupitia filamu, The Curious Case of Benjamin Button.

Tamthilia ya Joe Turner’s Come ambayo imeongozwa na Debbie, ndani yake Taraji amecheza nafasi ya Bertha Holly sambamba na Cedric the Entertainer.

Ikumbukwe baada ya kusomea uigizaji Chuo Kikuu cha Howard, Taraji alicheza filamu yake ya kwanza, Streetwise (1998), na tangu wakati huo amekuwa akifanya vizuri akishinda tuzo 38 na kutajwa katika orodha ya watu 100 wenye nguvu ya ushawishi duniani.

Baadhi filamu zake maarufu ni pamoja na Baby Boy (2001), The Karate Kid (2010), Think Like a Man (2012), Acrimony (2018), What Men Want (2019), The Best of Enemies (2019).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *