Gradine Toto: Kutimuliwa jeshini hadi kutoa wimbo ‘Mayday Rachel’Gradine Toto: Kutimuliwa jeshini hadi kutoa wimbo ‘Mayday Rachel’

Dar es Salaam. ‘Mayday Rachel’ ni jina la wimbo wa mwanamuziki Gradine Dulo ‘Gradine Toto’ ambaye ameuteka ulimwengu kutokana na wimbo huo wa mapenzi kugusa hisia za watu wengi duniani.

Licha ya kuwa si watu wote wanaelewa maana ya maneno yaliyotamkwa kwenye wimbo huo. Lakini melodi  na sauti tamu imewafanya waweze kuupenda huku ukipigwa katika sehemu mbalimbali za burudani.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, msanii huyo ameeleza safari yake ya muziki huku akifichua kilichomo nyuma ya wimbo huo unaozungumzia hisia za kuumizwa za mwanaume kwenda kwa mpenzi wake aitwaye Rachel.

Akisimulia kuhusu safari yake Gradine amesema yeye ni mzaliwa wa moja ya nchi iliyopo Afrika ya Kati. Huku akificha kuitaja nchi hiyo.

“Sitaki kusema hasa nilizaliwa wapi, lakini nilizaliwa Afrika ya Kati. Sehemu kubwa ya utoto niliitumia nikiwa Kinshasa, Kongo,” amesema Gradine.

Gradine amesema safari yake katika muziki ilianza tangu akiwa mtoto, huku akimtaja mama yake kama mtu aliyemvutia.

“Mama yangu alikuwa mwimbaji mzuri sana kanisani. Alikuwa akiimba muda wote hata akiwa jikoni, akipiga deki nilikuwa naona. Kwa hiyo naweza kusema kuimba nilivutiwa na mama yangu. Kisha baadaye kipaji changu kikaboreshwa na wakufunzi wengine,” amesema.

Licha ya kuwa alipenda kuimba tangu akiwa mtoto amesema aligundua kuwa na  uwezo mkubwa wa kuimba alipokuwa shule ya sekondari kati ya mwaka 2016 hadi 2019.

Gradine Toto msanii aliyeimba wimbo unaotamba Mayday Rachel

“Nilipokuwa high school ndipo niligundua kweli ninaweza kuimba. Hapo ndipo nilianza kuamini kuwa nina kipaji. Unajua shule kulikuwa na festival sasa kwaya masta akawa ananichagua kama muongozaji

“Lakini nilianza kuimba rasmi kwa kurekodi nyimbo zangu baada ya kufutwa kazini. Nilikuwa nafanya kazi jeshini hapo ndipo niliamua kujaribu kwenye kipaji changu ilikuwa mwaka 2025,”amesema.

Alivyofutwa kazi jeshini

Hata hivyo, Gradine ameeleza kuwa kabla ya kuingia rasmi kwenye muziki, aliwahi kujiunga na jeshi. Lakini alifukuzwa kazini baada ya muda mfupi kutokana na suala ya nidhamu.

“Nilikuwa napitia kipindi cha kuumizwa moyo baada ya kuachana kati yangu na Rachel. Ilikuwa inaniumiza hadi ikaathiri kazi yangu nikawa siendi kazini.

“Nilikuwa sifanyi chochote, siku zilikuwa zinaenda sasa hadi narudi kwenye akili yangu timamu nikagundua nimechelewa nilifukuzwa jeshini rasmi kwa sababu jeshi linahitaji nidhamu kali sana,”alisema.

Hadithi nyuma ya Rachel

Moja ya mambo yaliyowavutia watu wengi ni tungo  iliyopo nyuma ya wimbo wa Mayday Rachel. 

Gradine alisema wimbo huo ulitokana na uhusiano wake wa kimapenzi na mwanamke aliyeitwa Rachel. Kwa mujibu wake, uhusiano wao uliharibika baada ya mpenzi wake wa zamani kuingilia kati.

“Kwanza unatakiwa kujua ni stori ya kweli. Mayday Rachel imezaliwa kutoka kwenye hisia kali na maisha yangu ya uhalisia. Nilitaka ielezee maumivu upweke. Nadhani nimeimba kwa niaba ya wanaume wengi kwa sababu kuna watu wanapitia vitu lakini hawawezi kuvisema .

“Kipindi niko kwenye mahusiano na Rachel nilikuwa ex wangu  pia liitwa Rachel. Sasa huyo ex alikuja nyumbani kwangu bila taarifa kwa sababu alikuwa anapajua. Sababu sipendi drama alivyokuja sikumfukuza.

“Nilimkaribisha kama mtu ambaye simfahamu alitengeneza chai kisha akasema anasikia usingizi. Niliacha simu yangu ndani nikawa nafua baadhi ya nguo zangu chafu,”amesema.
Amesema wakati ameenda kufua Rachel ambaye ni mpenzi wake wa zamani alichukua namba ya Rachel ambaye alikuwa mpenzi wake mpya.

“Nikiwa nimeenda kufua alichukua simu yangu na kuiba namba ya Rachel. Kisha akampigia simu na kujitambulisha kama mke wangu. Baadaye Rachel alinipigia akasema umempa namba mke wako anipigie nilishindwa kujitetea,”amesema

Tukio hilo lilisababisha Rachel kuamini kuwa Gradine alikuwa bado kwenye uhusiano mwingine. jambo lililofanya waachane.

Kufananishwa na Fally

Amesema alipotoa wimbo na watu kudhani umefanywa na Fally Ipupa ilifanya ajisikie vibaya.

“Nilihisi kama watu hawathamini juhudi zangu  badala yake wanamsifu mtu mwingine. Nilikuwa napitia kila mahali watu wanasema Fally ametoa wimbo mpya.

“Lakini pia nikaichukua kama sifa kwa sababu Fally ni msanii mkubwa na anayefanya vizuri. Kwahiyo kama wananilinganisha na yeye inaonesha nipo vizuri nilitaka tu utambulisho,”amesema.

Mjadala kuhusu AI

Baada ya wimbo ‘Mayday Rachel’ kusambaa kwa kasi, baadhi ya watu mitandaoni walidai kuwa umetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba (AI).

Hata hivyo msanii huyo amesema teknolojia imesaidia  katika baadhi ya vitu lakini sio kwenye kila kitu.

“Kuna sehemu za sauti kama kelele za umati wa watu wanasikia kwenye wimbo hizo ni computer sound effects. Lakini sauti yangu, hisia na uandishi wa wimbo ni halisi.

“Mwanzo walisema ni Fally Ipupa kwa hiyo kama ni Fally sio AI .  Lakini kwa sababu wamejua nimeimba mimi wanasema ni AI nadhani hapo watu wanakuwa wachaguaji sana. 

“Watu hawajazoea kusikia kitu kizuri kilicho kamilika. Kwa hiyo wakisikia wanahisi ni AI wanadhani binadamu hawezi kufanya. Siku hizi kila kitu kizuri ni AI. Ukisikiliza Mayday utagundua imetokana na hisia za binadamu na sio mashine,”amesema. 

Aliongeza kuwa Akili Mnemba haiwezi kutengeneza  hisia kama za binadamu.

Amesema wimbo huo umefungua milango mingi ya mafanikio ikiwemo kumtambulisha kwa hadhira mpya kimataifa na kupata usikivu kutoka kwa vyombo mbalimbali vya habari.

Kolabo na Kiba

Amesema yupo kwenye maandalizi ya kushirikiana na msanii Alikiba kutoa muendelezo wa wimbo huo yaani Mayday Rachel Remix.

“Tunafanya kazi ya wimbo Mayday Rachel 2, kwa kushirikiana na Alikiba ambapo mwezi huu nitakuja Tanzania kwa ajili ya kolabo ,” alisema.

Aidha amesema msanii namba moja anayempenda Tanzania ni Alikiba kutokana na vocal zake, kisha anafuata Mbosso. 
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *