
Dar/mikoani. Kila kitu kinapanda bei! ni maneno yanayoakisi manung’uniko ya baadhi ya wananchi, kuhusu mabadiliko ya bei za bidhaa mbalimbali, kulikosababishwa na ongezeko la bei za mafuta nchini na duniani.
Kwa mujibu wa wananchi, ongezeko la bei halikuishia kwenye mafuta pekee, limegusa bidhaa nyingine muhimu vikiwemo vyakula, vifaa vya ujenzi, gharama za usafiri ukiwemo wa baiskeli, ambao uendeshaji wake unategemea jasho la mwendeshaji badala ya mafuta.
Hali hiyo imejitokeza kuanza kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati, unaoyahusisha mataifa ya Marekani, Israel dhidi ya Iran, na kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz unaopitisha asilimia 20 ya mafuta yote ya Afrika.
Hatua hiyo, imeathiri mnyororo wa ugavi wa mafuta, uliosababisha kuadimika kwa nishati hiyo, hivyo kupatikana kwa gharama kubwa. Hali hiyo imepandisha bei ya bidhaa nyingine na kuacha maumivu kwa wananchi.
Ongezeko lilianza na nauli za mabasi ya mikoani na daladala Mei 1, mwaka huu. Taratibu likahamia kwenye bidhaa nyingine zinazotumika katika maisha ya kila siku ya wananchi kama gezi, vyakula na vifaa vya ujenzi.
Aidha, hata waendesha baiskeli wanaotoa huduma ya kusafirisha abiria mikoa ya Tabora, Shinyanga, Simiyu na Geita inatajwa kupanda, ambapo maeneo yaliyotumia Sh500 awali sasa yanadaiwa kutumia Sh1,000.
Makali hayo pia yamegusa huduma za usafiri wa wanafunzi unaotolewa na shule binafsi ambapo wamiliki wa shule hizo wameanza kupandisha michango ya usafiri.
Vilio vya bei
Akizungumza na Mwananchi, Mzazi wa watoto watatu wanaosoma katika moja ya shule mkoani Morogoro, Gift Joakim amesema Sh60,000 zilizotosha kugharimia usafiri wa wanawe kupelekwa shule na kurudishwa nyumbani, hazitoshi tena, kwa sasa anahitaji kuwa na Sh90,000 kwa mwezi.
Mmiliki wa shule hiyo, Selestine Mbilinyi amesema tangu kupanda kwa bei ya mafuta shule imejikuta ikiendesha mabasi kwa gharama kubwa inayoingiza hasara katika uwekezaji wake.
“Fedha tunayotumia kununua mafuta imeongezeka mara mbili huku wazazi wakilipa kiwango kilekile. Kupitia vikao na wazazi tutakubaliana kiwango kitakachofaa ili shule isipate hasara,” amesema.
Ukiacha gharama hizo za nauli ya mabasi ya shule ambazo zimeongezeka maeneo mengi, bei ya mfuko mmoja wa saruji imeongezeka kwa Sh700 hadi Sh1,000 kwa mujibu wa taarifa rasmi ya wazalishaji wa bidhaa hiyo.
Hiyo, imefanya bei ya mfuko mmoja wa saruji ufikie Sh18,000 hadi Sh19,000 mkoani Iringa, kutoka Sh15,000 na Sh16,000.
Mabadiliko ya bei pia, yameshuhudiwa katika bei za vyakula katika migahawa ya baba na mamalishe. Sahani yenye chakula iliyouzwa kwa Sh2,000 kwa sasa imefika Sh2,500 katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam.
Si chakula tu, hata soda iliyouzwa kwa Sh600 hadi Sh700, sasa inauzwa kwa Sh800 hadi Sh1,000 katika baadhi ya maeneo.
Ongezeko la bei za bidhaa halikuishia Tanzania Bara pekee, hadi Zanzibar wananchi wanakabiliwa na hali hiyo na eneo mojawapo lililoguswa ni la vifaa vya ujenzi.
Kwa mfano, boksi moja la vigae linauzwa Sh23, 000 hadi Sh30, 000 likiwa limepanda kutoka Sh20, 000.
Akizungumza na Mwananchi muuzaji wa vifaa vya Ujenzi visiwani Zanzibar, Yafas Khamis amesema bei imepanda kutokana na gharama za uchukuzi kwani hutegemea usafiri wa magari kuleta bidhaa hizo.
“Bei ya mafuta imepanda kwa hivyo hakuna mtu wa usafiri wa gari atakuletea bidhaa yako kwa bei ya awali, ndio maana imetulazimu kuongeza bei,” amesema
Hata hivyo, mfanyabiashara mwingine, Swaleh Juma amesema hadi vifaa vingine vya ujenzi kama vile saruji, nondo na misumamari havijapanda bei.
Mkoani Iringa, mabati ya kawaida, yameongezeka bei hadi Sh35, 000 kutoka Sh28, 000 za awali huku mbao zilizokuwa zinauzwa Sh1,800 sasa zinauzwa Sh2,000 hadi Sh2,500.
“Watu wengi wanakuja kuulizia bei lakini wanashindwa kununua kama zamani kwa sababu gharama zimeongezeka karibu kwenye kila bidhaa,” amesema mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi mkoani Iringa, Juma Mwaka.
Sababu za kupaa gharama
Watoa huduma na wauzaji wa bidhaa wanasema wamefikia hatua ya kupandisha gharama za huduma na bidhaa zao kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, usafirishaji na manunuzi yao.
Kwa vifaa vya ujenzi, Kampuni ya Dangote Cement ilitangaza ongezeko la Sh700 kwa aina zote za saruji wanazozalisha. Uamuzi huo, imesema unatokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji.
“Kutokana na kuendelea kupanda kwa gharama za usafirishaji, pembejeo na gharama za uendeshaji kwa ujumla, Dangote Cement Limited Tanzania (DCLT) itafanya marekebisho ya bei za saruji zake kuanzia tarehe 12 Mei 2026… itaongezwa kwa Sh700 kwa kila mfuko wa kilo 50 (bila VAT) katika masoko yote,” imeeleza taarifa hiyo.
Wakati Dangote wakisema hayo, baadhi ya maofisa waliozungumza na Mwananchi kutoka kiwanda cha Mbeya Cement na JK White Cement nao wamekiri kuwapo kwa ongezeko la hadi Sh1,000.
“Ni kweli bei imeongezeka tangu Mei 7, mwaka huu. Hii imetokana na ongezeko la bei ya mafuta iliyopandisha gharama za usafirishaji. Hali hii ndiyo iliyochochea mawakala wetu kupandisha bei,” amesema.
Kutokana na kupaa huko kwa bidhaa hiyo, sasa mfuko uliokuwa ukiuzwa Sh16, 500 sasa unauzwa hadi Sh18,000, huku ule wa Sh17,500 sasa unafikia Sh19,000.
kwa upande wa chakula, muuzaji wa chakula, Lulu John wa Tabata jijini Dar es Salaam, anasema amepandisha bei ya sahani ya wali, ugali, vitafunwa na vinywaji kutokana na gharama za manunuzi anazokutana nazo kwenye mahemezi.
“Gharama zimepanda sana sokoni sisi huku tunauza kwa hasara, ndiyo maana tumepandisha ili na sisi tusipate hasara. Watu wanakuja baadhi wanalalamika lakini hivyohivyo biashara imekuwa ngumu sana,” anasema.
Bei ya mayai nayo imepanda ambapo maeneo ya Magomeni jijini Dr es Salaam, imefikia Sh400 kwa yai moja tofauti na Sh300 ya awali.
Shambani nako hakupoi
Kupanda kwa chakula huku kunaonekana pia kuathiriwa moja kwa moja na bei ya mazao kwa wazalishaji mashambani, ambapo inaelezwa kuwa bei za mahindi na mpunga zimeendelea kuwa juu kwenye maeneo ya uzalishaji kabla hazijaunganishwa gharama za usafirishaji.
“Miaka mingine msimu kama huu wa mavuno mahindi na mchele huuzwa kwa wastani wa Sh5,000 kwa debe (ndoo ya lita 20), lakini mwaka huu tunashangaa, hadi sasa mahindi na mpunga vinauzwa zaidi ya Sh10,000 kwa debe moja,” anasema Salu Weja mkulima kutoka Ulyankulu mkoani Tabora.
Anaeleza katika eneo hilo, unga wa ngano ambao ulikuwa ukipatikana kwa wastani wa Sh1, 200 hadi Sh1,500 kwa kilo, sasa unauzwa Sh2,500 katika maduka mengi ya rejareja.
Wachumi washauri
Akizungumzia suala hilo, mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk Goodhope Mkaro anasema kupanda kwa gharama za ujenzi kunaweza kufanya sekta ya ujenzi idorore.
Hiyo ni kwa sababu itapunguza uwezo wa watu kununua bidhaa, akitoa mfano, kuwa kama walikuwa wanapata mifuko 10 kwa Sh200,000, sasa itakuwa pungufu.
“Kinachoweza kuwasaidia kwa sasa ni kuwa na vipaumbele, kupunguza vitu ambavyo havina umuhimu ili waweze kuendelea na ujenzi,” amesema.
Amesema kuwekwa kwa ruzuku ya Sh259 kwa lita ya dizeli huenda kumesaidia kwa kiasi Fulani kuzuia ongezeko kubwa la bei, akisema kama isingekuwapo hali ingekuwa mbaya zaidi.
“Ushauri wangu kwa Serikali, vita ikiisha wahakikishe wanasimamia bei za bidhaa, ikiwemo saruji, zirudi katika bei zake za zamani, kwani mara zote bei zimekuwa zikipanda wakati kama huu, kushuka inakuwa ni vigumu,” amesema.
Kwa upande wake Profesa Abel Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema kinachotokea kwa sasa ni mfumuko wa bei na ni jambo la kawaida kutegemewa kwa kipindi hiki.
Anasema katika kipindi hiki ambapo bei zinaendelea kubadilika, wananchi wanapaswa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ili kuendana na gharama za maisha zinazopanda.
Anasema, kwa Serikali ni wakati wa kuona namna ya kupitia kodi na tozo kwenye bidhaa muhimu ili kupunguza makali ya maisha kwa wananchi.
“Katika suluhu ya kudumu, Serikali na wadau waone namna ya kuongeza uwekezaji kwenye matumizi ya bidhaa za ndani ikiwemo nishati ya makaa ya mawe na umeme wa jua, ili kuepuka matumizi ya bidhaa ambazo bei zake hatuna mamlaka nazo, zinaamliwa kutoka nje,” anasema.
Imeandikwa na Pawa Lufunga na Bakari Kiango (Dar es Salaam), Zuleikha Fatawi (Zanzibar) na Christina Thobias (Iringa).
