Uhondo wa mechi 104 Kombe la Dunia 2026 mbashara Azam TV Uhondo wa mechi 104 Kombe la Dunia 2026 mbashara Azam TV 

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza katika historia, kituo cha luninga cha Azam TV kitaonesha mbashara mechi zote 104 za Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Canada, Marekani na Mexico.

Hii inakuwa mara ya kwanza kwa televisheni ya Tanzania kuonesha mbashara mechi zote za Fainali za Kombe la Dunia tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo makubwa ya dunia mwaka 1930.

Pia, ni mara ya kwanza kwa Azam TV kupata haki ya kuonesha mechi zote za Kombe la Dunia tangu kampuni hiyo ilipoanzishwa mwaka 2013.

Azam TV itaonesha mechi hizo kupitia chaneli za Azam Sports 2HD na Azam Sports 4HD kuanzia mechi ya kwanza kati ya Afrika Kusini na Mexico Juni 11 na kumaliza kwa mchezo wa fainali utakaopigwa Julai 19, mwaka huu.

Wakati wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, mechi ya kwanza ilikuwa kati ya Afrika Kusini na Mexico kama itakavyokuwa mwaka huu.

Utamu ni kwamba mechi zote zitatangazwa na kuchambuliwa kwa lugha adhimu ya Kiswahili zikiwa na ladha maalumu kutoka kwa watangazaji na wachambuzi mahiri wa soka nchini.

Kwa watazamaji wa nje ya Tanzania kama Malawi, Kenya na Uganda watapata uhondo huo kwa lugha ya Kiingereza kutoka kwa watangazaji na wachambuzi kutoka nchi husika.

Takribani nchi zote ambako Azam TV hufikisha matangazo yake watafaidi uhondo huo wa mechi.

Azam TV itakuwa na studio mbili za kisasa kwa ajili ya wachambuzi wa lugha ya Kiswahili na nyingine kwa Kiingereza.

Azam TV imezindua kampeni yake kubwa ya matangazo hayo leo Jumamosi kwa kutumia helikopta maalumu inayozunguka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ikiwa na bango lenye maandishi ya: “Mechi zote 104,

Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitashirikisha idadi ya timu za taifa 48 zilizogawanywa katika makundi 12 yenye timu nne kila moja.

Argentina wanaingia katika fainali za mwaka huu wakiwa mabingwa watetezi wa taji hilo walilolitwaa mwaka 2022 baada ya kuifunga Ufaransa katika mechi ya fainali kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya dakika 120 za mechi hiyo kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Kwa mara ya kwanza katika historia, bara la Afrika litawakilishwa na timu 10 katika fainali hizo ambazo pia kwa mara ya kwanza zinaandaliwa na nchi tatu.

Wawakilishi 10 wa Afrika katika fainali hizo ni Senegal, Morocco, Tunisia, Afrika Kusini, Cape Verde, Misri, Algeria, Ghana, DR Congo na Ivory Coast.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *