Mambo magumu, mhadhiri akwaa kisiki kupangua uamuzi wa RaisMambo magumu, mhadhiri akwaa kisiki kupangua uamuzi wa Rais

Dar es Salaam. Mambo bado magumu, ndiyo maneno unayoweza kuyatumia kuelezea safari ya aliyekuwa mhadhiri msaidizi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Jonas Tilya, anayepinga uamuzi wa Rais wa kubariki kufutwa kwake kazi.

Hii ni baada ya rufaa yake aliyoiwasilisha Mahakama ya Rufani Tanzania kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, kutupa maombi yake ya mapitio ya mahakama aliyotaka kurejeshwa kazini, kukwaa kisiki kortini.

Rufaa hiyo namba 409 ya 2023, iliyotolewa uamuzi Mei 15, 2026 na jopo la majaji watatu, aliifungua dhidi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Bodi ya Magavana ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Hata hivyo, baada ya kufungua rufaa hiyo, ilikutana na kizingiti kuwa ilifunguliwa nje ya muda wa kisheria, hoja ambayo majaji- Dk Mary Levira, Lilian Mashaka na Paul Ngwembe walikubaliana nayo na kuitupa rufaa hiyo.

“Kwa upande wetu, tunathamini hoja za pande mbili, na baada ya kupitia kumbukumbu za hukumu inayopingwa, ni dhahiri kwamba ilitolewa na Jaji Mfawidhi Mei 15, 2023,” walisema majaji hao na kuongeza:

“Kutokana na mrufani kwa kutoridhishwa, aliwasilisha notisi ya rufaa tarehe Mei 24, 2023 na tarehe hiyo hiyo aliomba nakala zilizoidhinishwa, ambazo zilijibiwa na msajili Juni 19, 2023. Yote hapo juu yalifanyika vizuri ndani ya wakati.”

“Hata hivyo, mrufani hakuwahi kuomba cheti cha kuchelewa, ambacho kingeondoa kipindi cha kuanzia tarehe Mei 24, 2023 wakati mrufani aliomba nakala hadi Juni 19, 2023 alipojulishwa kuwa rekodi zilikuwa tayari kukusanywa.”

“Wakati mrufani anaamini muda ni kuanzia Juni 19, 2023 alipoarifiwa juu ya utayari wa nyaraka, AG alishikilia kuwa bila kuwepo kwa cheti cha kuchelewa, muda ulianza kukimbia kutoka Mei 24, 2023 wakati notisi ya rufaa ilipowasilishwa.”

“Kwa upande wetu, hatuoni ubishi kwa sababu maswali yote yanatakiwa kutatuliwa kwa sheria. Kanuni ya 90 (1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani Tanzania, 2009, inataka kuwepo kwa cheti cha kuchelewa kutoka kwa msajili,” walisisitiza majaji hao.

“Ni msimamo wa sheria kwamba mrufani analazimika kupata kutoka kwa msajili nyaraka zote muhimu, ikiwa ni pamoja na cheti cha kuchelewa ikiwa rufaa imepitwa na wakati,” walieleza majaji katika hukumu yao waliyoitoa Mei 15, 2026.

“Kwa maneno mengine, hakuna nafasi ya kumlaumu msajili ikiwa mrufani ameshindwa kuomba. Tunasisitiza kwamba ni lazima kuwe na uzingatiaji kamili wa sheria na kanuni za mahakama,” walisisitiza na kuhitimisha.

Majaji hao walisema mrufani alikuwa na siku 60 za kuwasilisha rufaa yake, na hii ni kati ya Mei 24, 2023 hadi Julai 23, 2023, na hakuna ubishi kuwa Julai 23, 2023 ilikuwa ni siku ya mapumziko, na siku iliyofuata Jumatatu ilikuwa Julai 24, 2023.

“Hiyo tarehe (Julai 24, 2023) ndiyo ilipaswa kuwa tarehe ya mwisho kwa mrufani kuwasilisha rufaa yake, lakini badala yake rufaa hii iliwasilishwa Agosti mosi, 2023, sawa na siku tisa baada ya siku 60 zinazotakiwa na sheria kupita,” walisema majaji.

Majaji hao walisema baada ya kugundua kuwa rufaa iliwasilishwa nje ya wakati, hawana la kufanya zaidi ya kuipiga nje rufaa hiyo kutokana na sababu hiyo.

Safari ya kutuhumiwa, kushushwa daraja

Kulingana na hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufani iliyowekwa katika tovuti, kumbukumbu zinaonesha kuwa Tilya alikuwa mwajiriwa wa mjibu rufaa wa pili, ambaye ni Bodi ya Magavana ya Chuo cha Ustawi wa Jamii, kuanzia Julai mosi, 2014.

Ilipofika Agosti 2015, alithibitishwa kama mhadhiri msaidizi na kuingizwa katika ajira ya kudumu na kuingizwa katika masharti ya pensheni.

Akiwa kazini, alituhumiwa kulazimisha uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi wa kike wa kozi aliyokuwa akifundisha, na ili kushawishi akubaliwe, alimtisha mwanafunzi kuwa angesahihisha mitihani yake isivyo sawa ikiwa atakataa.

Tilya alifunguliwa makosa manne ya kinidhamu, moja likiwa kushindwa kutekeleza majukumu ya kuridhisha, kinyume na Kanuni ya 42 na aya ya 8 ya Sehemu A ya Jedwali la Kwanza la Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.

Shtaka la pili lilikuwa ni unyanyasaji wa kingono kinyume na Kanuni ya 65 (1) na aya ya 6 ya Sehemu ya II ya Jedwali la Tatu la Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, na la tatu ni utovu wa nidhamu kinyume na kanuni za utumishi.

Katika shtaka la nne, ilikuwa ni ukiukaji wa Kanuni za Maadili kwa Utumishi wa Umma, Kanuni za Maadili za Kitaalamu na Maadili ya Uongozi wa Umma, kinyume na Kanuni ya 42 na aya ya 14 za Utumishi wa Umma.

Baada ya kupewa mashtaka hayo na kamati ya nidhamu, aliyakanusha yote na kamati iliketi Januari 18, 2020, na baada ya shauri lake kusikilizwa, alipatikana na hatia katika kosa la kwanza la kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kuridhisha.

Baada ya kumtia hatiani, kamati ilipendekeza adhabu ya kumshusha cheo chake kutoka mhadhiri msaidizi hadi mkufunzi msaidizi mafunzo kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia Januari 18, 2020.

Anakata rufaa na kukutana na kigingi

Mrufani hakuridhika na akakata rufaa kwa Tume ya Utumishi wa Umma kwa misingi kadhaa, ikijumuisha kunyimwa haki ya kusikilizwa na haki ya uwakilishi, uwepo wa upendeleo na muundo wa wajumbe wa kamati ya uchunguzi.

Baada ya rufaa kusikilizwa, alishindwa na tume haikutupa tu zile sababu za rufaa, bali ilienda mbali na kubaini kuwa mrufani alikuwa na hatia si tu kwenye lile kosa la kwanza lililomshusha cheo, bali pia kwa makosa mengine.

Hukumu ya tume ilikuwa kuweka kando adhabu ya awali ya kupunguzwa cheo, badala yake ikatoa uamuzi kuwa afukuzwe kazi. Akakata rufaa kwa Rais, lakini Agosti 4, 2022 Rais alitupa rufaa hiyo na kubariki uamuzi wa Tume ya Utumishi.

Hapo ndipo alipoamua kufungua maombi ya mapitio ya mahakama (judicial review) mbele ya Mahakama Kuu, ambapo mahakama iliona tume ilikosea kwa kuunda mashtaka mapya ambayo hayakuwa sehemu ya taratibu za kinidhamu.

Malalamiko mengine yalitupiliwa mbali, ambayo yalifanya maombi yote ya mapitio ya mahakama kutupwa, ndipo akakimbilia Mahakama ya Rufani, lakini nako akagonga mwamba kwa kigezo cha kufungua rufaa nje ya muda.

Kabla ya majaji kusikiliza rufaa hiyo, walisema ni vyema wajiridhishe juu ya uhalali wa rufaa hiyo na wakili Isaac Tasinga alimwakilisha mrufani, na wakili wa Serikali Mkuu, Grina Aden, akisaidiana na mawakili Hosana Mgeni na Victor Mhana waliwakilisha wajibu rufaa.

Hapo ndipo suala la ukomo wa muda liliibuka katika mawasilisho ya mawakili wa pande mbili, na majaji kukubali hoja za wajibu rufaa juu ya kuwa nje ya muda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *