Mustakabali wa kutokomeza VVU duniani uko njiapanda kutokana na ukata: ByanyimaMustakabali wa kutokomeza VVU duniani uko njiapanda kutokana na ukata: Byanyima

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu UKIMWI wa mwaka 2026, Mkurugenzi Mtendaji huyo Winnie Byanyima, amesema huenda huu ukawa mkutano wa mwisho wa aina hiyo kufanyika.

Akizungumza na waandishi hao wa habari mjini New York Marekani mwishoni mwa wiki amesema kupunguzwa kwa matumizi na mashambulizi dhidi ya haki za binadamu vinaathiri kazi ya wanasayansi wanaotafuta tiba ya ugonjwa huo.

Ufadhili washuka kwa asilimia 30 hadi 40

Hatua za kimataifa dhidi ya VVU zimepungua kwa kiasi kikubwa katika rasilimali zake. Katika mwaka uliopita, amesema fedha zilizotengwa kwa ajili ya kupambana na janga hilo zimepungua kwa kati ya asilimia 30 hadi 40 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023.

Kwa mujibu wa Bi. Byanyima, wafadhili wengi sasa wanaelekeza fedha katika kufadhili vita, na bila msaada wa kimataifa nchi zinazohudumiwa na UNAIDS hazitaweza kuendeleza programu za kinga na matibabu.

Mkutano huo wa Ngazi ya Juu utafanyika tarehe 22 hadi 23 Juni mjini New York ukiwa na kaulimbiu “Kwa Pamoja Kutokomeza UKIMWI.”

Mkutano huo utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, watu wanaoishi waziwazi na VVU pamoja na watu mashuhuri wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya virusi hivyo.

Lengo la mkutano huo ni kuweka ahadi za kisiasa zitakazosaidia kudumisha azma ya kutokomeza VVU/UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.

Mipango ya matumaini

Licha ya mgogoro wa bajeti, baadhi ya hatua zinaonesha maendeleo. Miongoni mwao ni makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Wizara za Afya wakati wa mkutano wa G20 mwaka 2024, kundi la mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani.

Chini ya uenyekiti wa Brazil, muungano wa kimataifa wa kuhakikisha upatikanaji sawa wa teknolojia za afya uliundwa.

Mpango huo umechochea uzalishaji wa ndani wa dawa na chanjo, huku ukisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na janga la VVU.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *