KUMEIBUKA mjadala kwa baadhi ya wadau wa soka wakiona kama wamedanganywa hatua za kuanza kwa ujenzi wa Uwanja wa Yanga, sasa kigogo mmoja wa timu hiyo ameibuka na kutuliza presha.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Munir Said, amesema watu hawatakiwi kuwa na presha juu ya kuanza kwa hatua ya ujenzi akisema mradi huo kuanza sio lazima kuona nondo na mchanga.
Munir amesema katika hatua za ujenzi wa uwanja mkubwa kama huo unaoihusisha klabu kubwa kama Yanga, lazima uanze kwa hatua za kiofisi ikiwemo kusajili mradi kwa mamlaka za kiserikali.
Bosi huyo alisema baada ya hatua hizo za awali ambazo zinatafsiri kuanza kwa ujenzi, mamlaka za serikali zitatoa vibali maalum ambapo baada ya hapo ndio mchakato wa ujenzi kuanza eneo la mradi.
“Unajua tumekuwa tukipokea simu nyingi sana wakiona kama alichokisema Rais (Hersi Said) ni kama amewadanganya aliposema ujenzi ungeanza jana, naona watu walitarajia kuona pale kuna vifaa vinashushwa, nondo na saruji,” amesema Munir.
“Watu watambue huu ni mradi mkubwa lazima zifanyike taratibu za kisheria, zikiwemo kuusajili kwa mamlaka za serikali na baada ya hapo vitatoka vibali ambavyo sasa ndio vitakwenda kuruhusu tatartibu zingine za kiujenzi eneo la mradi.
“Sisi ndio wajumbe tuliosimamia mchakato huu kuanzia mwanzo mpaka sasa, tuna imani kubwa kwamba uwanja utajengwa na mashabiki wa klabu yetu wasiyumbishwe na wale wa upande wa pili, watulie wataona uwanja wao.”
Mapema Hersi mara baada ya kusainishana makubaliano ya mradi huo na kampuni ya GSM ambayo ndio itakwenda kusimamia ujenzi huo, alisema ujenzi ungeanza Jumamosi Mei 17, 2026 na kukamilika kwake ndani ya miezi 18 hadi 24.
Yanga imetangaza kuanza kwa mchakato huo wa ujenzi wa uwanja eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 20,000.
