Mwelekeo mpya bei ya CocoaMwelekeo mpya bei ya Cocoa

Mbeya. Wakati matumaini yakirejea kwa wakulima wilayani Kyela kufuatia bei ya cocoa kupanda, wadau na Serikali wametaja mikakati na mipango kuhakikisha zao hilo linaendelea kupaa, huku wakitoa angalizo.

Kwa takribani miaka miwili nyuma, bei ya cocoa ilifikia Sh32,000 kwa kilo lakini kwa cha miezi mitatu nyuma mwaka huu ilishuka hadi Sh5,540 na kufanya wakulima kuhofia kilimo hicho kwa mustakabali wao.

Kutokana na mdororo huo, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Copra), ilikutana na wadau jijini Mbeya kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kwa maendeleo endelevu kwa tasnia ya cocoa.

Kikao hicho ambacho kilifanyika Machi 7 mwaka huu, kilihusisha mikoa minne inayolima zao hilo ikiwa ni Mbeya, Songwe, Morogoro na Tanga, huku Kagera ikitajwa kuwa na uzalishaji mdogo.

Hata hivyo, katika mnada uliofanyika Mei 11, mwaka huu kwenye ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Kyela (Kyecu) bei ilipanda hadi Sh10,380 kwa kilo moja,  huku kilo 238,420 zikiuzwa.

Sababu ya anguko la bei

Katika kikao hicho cha kwanza kilichofanyika Mbeya, sababu kadhaa zilitajwa kushuka kwa bei ya zao hilo na mikakati maalumu ya kurejesha uhai kwa wakulima.

Miongoni mwa sababu zilizotajwa ni kushuka kwa bei ya soko la dunia, wazalishaji wakubwa kama Ivory Coast wanaozalisha tani milioni mbili na Ghana tani 700,000 walikumbwa na hali mbaya ya hewa na magonjwa katika zao hilo.

Sababu nyingine ni mlipuko wa magonjwa ulioathiri kwa kiwango cha asilimia 40 ilifanya kampuni kubwa duniani zinazonunua zao hilo walianza kununua bidhaa za ziada kwa muda wa mbeleni.

Mikakati ya Serikali

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Copra, Irene Mlola anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau wameweka mipango ili kuhakikisha zao hilo linarejea kwenye hali yake na kuinua uchumi wa mkulima na Taifa kwa jumla.

Anasema mkakati wa kwanza ni uhakika wa kuongeza uzalishaji kutoka tani 17,000 na ili kufikia malengo hayo lazima kuwapo uhakika wa upatikanaji wa miche.

Anasema lazima kufahamu kanuni za kilimo bora kwa kuwafundisha wakulima ili tija inayopatikana iwanufaishe kuanzia wadau hadi wakulima wenyewe.

Mkakati wa pili anasema ni kuongeza ubora, akibainisha kuwa ili kufikia malengo lazima wawe na uzalishaji wenye ubora ili kujitofautisha na washindani licha ya kutokuwa na kiwango kikubwa ikilinganishwa na vinara Ivory coast na Ghana.

“Sisi Copra tumepanga kuwa na makaushio saba kwa mwaka huu kabla ya Juni ila mwaka ujao wa fedha tumejipanga kuweka bajeti kuongeza hadi 20 ili kuweza kufikia malengo, lakini tuzingatie kanuni za umoja wa Ulaya juu ya uharibifu wa mazingira (UDI),” amesema.

Amesema mkakati mwingine ni kilimo cha mkataba kitakachomuwezesha mkulima na mchakataji kujihakikishia malighafi na kuuza kwa madaraja kama ilivyo kwenye kahawa.

“Mkakati mwingine ni kuongeza thamani ndani ya nchi, hata kama hatutafika asilimia 100 kwa muda mfupi, lazima tuwe na juhudi za makusudi tunaendeleza zao katika viwanda vyetu,” amesema.

Meneja Mkuu wa Kyecu, Aman Hankungwe amesema kupanda kwa bei hiyo ni mwelekeo mzuri katika kufikia malengo yao na wakulima kwa jumla.

Amesema ili kuhakikisha bei inaendelea kupanda, Kyecu inaendelea kuhimiza wakulima na kuvuna kwa ubora zao hilo ili kulipa thamani na kuvutia wanunuzi zaidi kwa mafanikio.

“Mpango wetu ni kuzitembelea Amcos na kukutana na wakulima angalau asilimia 80 ili tuweze kuzungumza nao, kuwapa elimu ya kuandaa, kulima na kuvuna kwa ubora, tukifanya hivi tutawavutia wanunuzi wengi na bei itakuwa shindani.

“Malengo ni kuona bei angalau inafikia Sh15,000 kwa kilo ukizingatia bei elekezi ya Serikali ni Sh10,000 na tulishuka hadi Sh5,440, hivyo tunashauri wakulima kuliongezea thamani zao hili,” amesema Hankungwe.

Mkulima wa zao hilo wilayani Kyela, Isaya Mwakimo amesema kushuka kwa bei ya awali, licha ya hofu haikuwapa wakati mgumu sana kutokana na hali ya hewa kwa Machi na Aprili.

“Kampuni nyingi kipindi kama hicho zinasimama kutokana na mvua nyingi zinazokuwa zinanyesha, sisi wakulima tuna matarajio kwamba, katika mnada ujao bei itapanda tena kutoka hapa ilipofikia,” amesema Mwakimo.

Unice Mwakiswaswa amesema wakulima na Serikali wanategemeana, hivyo mafanikio au anguko la mmoja wapo linawagusa wote ikiwamo Taifa, akipongeza juhudi zinazofanywa na mamlaka.

“Sisi wakulima hatuna soko, wateja wote wanaokuja wanaletwa na Serikali, hivyo utaona msukumo mkubwa ni pande zote, kwa kuwa tunalipambania Taifa moja, tunashukuru na kupongeza Serikali,” amesema Unice.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *