Njombe. Watumishi 10 wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, waliokuwa wakielekea Wilaya ya Makete, wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wamepanda kuacha njia na kupinduka kutokana na mteremko mkali na kona.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana Mei 16, 2026, ambapo amesema imetokea Mei 16, 2026, saa 3:40 asubuhi katika kata ya Tandala wilayani Makete.
Amesema eneo hilo lina kona na mteremko mkali, hali iliyosababisha dereva kushindwa kumudu gari hilo lililobeba watumishi hao ambao walikuwa wakielekea Chuo cha Ualimu Tandala kwa ajili ya Bonanza la mwenge.
Banga amesema dereva wa gari hilo, Robert Malekela (46), mkazi wa Ilembula, amekamatwa na anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano kwa sababu hakuwa na kibali.
Baadhi ya wananchi wakiangalia ajali hiyo iliyotokea maeneo ya kijiji cha Tandala kilichopo wilayani Makete ambapo watumishi 10 kati ya 43 waliokuwepo kwenye basi walijeruhiwa.
“Gari hili aina ya Fuso, halikuwa na kibali cha kusafiri kwenda njia hiyo, limekuwa likifanya safari zake kati ya Njombe na Igwachanya, hivyo lilikodiwa na dereva akaenda kwenye njia ambayo hana uzoefu nayo,” amesema Banga.
Ametoa wito kwa madereva mkoani Njombe kuwa makini wanapoendesha magari kufuata taratibu za kuomba vibali wanapobadilisha njia pamoja na kuwa waangalifu katika maeneo yenye kona na miteremko.
Mkuu wa Wilaya ya Makete, Kissa Kasongwa ametoa pole kwa majeruhi wa ajali iliyotokana na basi hilo huku akitoa shukurani kwa wauguzi na madaktari wa Hospitali ya Ikonda kwa kuwahudumia watumishi hao.
“Nawapa pole majeruhi wote waliopata ajali, pia, nawashukuru wauguzi na madaktari kwa kuwahudumia watumishi hawa,” amesema Kasongwa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Jerry Mwaga amesema kuwa watahakikisha wanasimamia huduma muhimu kwa ajili ya majeruhi hao ikiwemo kuwarudisha makwao.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Consolata Ikonda, Agnes Mlawa amesema majeruhi 10 kati ya 43 walikuwepo kwenye gari hilo na kupokewa kwenye hospitali hiyo.
“Hakuna aliyepoteza maisha katika majeruhi hawa, tuliowapokea bali wanahitaji tu huduma ya karibu,” amesema Mlawa.
