Marekani. Vita vya maneno kati ya Jay-Z na Nas vimeendelea kutajwa kama moja ya migogoro mikubwa zaidi kuwahi kutokea kwenye muziki wa hip-hop duniani.
Chanzo cha ugomvi huo kinatajwa kuanzia studio, baada ya Nas kushindwa kufika kurekodi kwenye albamu ya kwanza ya Jay-Z, Reasonable Doubt iliyotoka mwaka 1996.
Inaelezwa Jay-Z alikuwa amepanga kufanya kazi na Nas kwenye moja ya nyimbo za albamu hiyo. Huku baadhi wakidai ilikuwa “Bring It On” na wengine wakitaja “Can I Live”.
Hata hivyo, siku ya kurekodi ilipowadia, Nas hakutokea studio jambo lililoanza kuvuruga uhusiano wao taratibu.
Mwanzilishi mwenza wa Roc-A-Fella Records, Dame Dash amesema Nas pamoja na rapper AZ walikuwa wamepangwa kushiriki kwenye “Bring It On”. Lakini walichelewesha vipindi vya kurekodi hadi Jay-Z akaamua kutumia rappers wengine kukamilisha wimbo huo.
Aidha mtayarishaji maarufu Irv Gotti naye alikumbuka tukio hilo na kusisitiza kuwa Nas hakufika studio kama ilivyotarajiwa.
Miaka michache baadaye, hali hiyo iligeuka kuwa vita kwenye muziki huku Jay-Z na Nas wakirushiana vijembe kupitia nyimbo za diss, mahojiano na majukwaa mbalimbali ya burudani.
Wachambuzi pia waliwaona wawili hao kama wachanaji bora wa kizazi chao. Jambo lililofanya ushindani wao kuvuta hisia kubwa kutoka kwa mashabiki wa hip hop duniani.
Kabla ya mgogoro huo, wawili hao walikuwa tayari wanafahamiana tangu miaka ya 1990 kupitia mtayarishaji Large Professor aliyemsaidia Nas kupata nafasi kwenye muziki.
Katika moja ya ziara zao mjini Washington, Large Professor aliwahi kudai walikutana na mazingira hatari na ndipo Jay-Z aliyekuwa bado anachipukia kwenye rap alitoa bastola ili kuwatuliza wenzake.
Baadaye Jay-Z alirejea tukio hilo kupitia wimbo wake maarufu “Takeover”, akidai ndiye aliyemuonyesha Nas silaha kwa mara ya kwanza.
Wakati huo Nas alikuwa tayari ametikisa muziki wa New York kupitia albamu yake Illmatic ya mwaka 1994, huku The Notorious B.I.G. naye akifanya mapinduzi kupitia albamu Ready to Die.
Jay-Z aliingia rasmi kwenye ushindani huo baada ya kuachia Reasonable Doubt mwaka 1996, huku sauti ya Nas ikisikika kupitia sampuli ya wimbo “The World Is Yours” kwenye “Dead Presidents II”.
Wiki moja baadaye, Nas aliachia It Was Written iliyofanya vizuri zaidi kibiashara kuliko Illmatic. Huku “If I Ruled the World” ikiwa moja ya nyimbo zilizotikisa kipindi hicho.
Kadri miaka ilivyokwenda, ushindani huo uliendelea kukua na kugeuka moja ya beef kubwa zaidi katika historia ya hip hop, ukizaa nyimbo kali na mijadala ambayo hadi leo bado inatajwa duniani.
