
Dar es Salaam. Wasomi, watafiti na wabunifu nchini Tanzania wametakiwa kuhakikisha kazi zao za kitaaluma haziishii katika makaratasi bali zinageuzwa kuwa masuluhisho ya kweli yanayotatua changamoto za kijamii.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu, Mei 18, 2026 na Naibu Katibu Mtendaji anayesimamia Biashara na Ubunifu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Dk Blandina Kilama wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Tafiti na Bunifu 2026 katika Chuo Kikuu Ardhi (ARU) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Kilama amesema Taifa haliwezi kupata maendeleo ya kweli kama maarifa yanayozalishwa vyuoni hayatatumika moja kwa moja kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema tafiti zinapaswa kuwa msingi wa kutengeneza sera, biashara changa (start-ups), na teknolojia zinazozalisha ajira na kuongeza tija katika uchumi wa nchi.
“Hatuwezi kupanga mipango thabiti bila taarifa sahihi kutoka kwenye tafiti zenu pamoja na bunifu zenu za uendelezaji wa miji na ardhi, hivyo basi naomba mtambue kuwa ninyi ni kiungo muhimu kwetu,” amesema Kilama.
Kilama amesema miji inakuwa kwa kasi kubwa huku ukuaji huo ukiambatana na na changamoto za makazi,miundombinu, usafiri, usimamizi wa ardhi, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema kwa sababu hiyo, zinahitajika suluhisho za kisasa na zinazotekelezeka.
“Tunahitaji tafiti zinazoweza kusaidia kujenga miji himilivu, miundombinu salama, na matumizi bora ya ardhi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.
Akitoa mfano wa umuhimu wa tafiti hizo, Dk Kilama alikumbusha tukio la hivi karibuni ambapo eneo la makazi katika mji unaokua kwa kasi nchini lilikumbwa na mafuriko makubwa, nyumba kupasuka na barabara kukatika baada ya mvua chache.
Amebainisha, changamoto hiyo haikutokana na ukosefu wa fedha pekee, bali ukosefu wa mipango sahihi, matumizi hafifu ya tafiti na kutokuwepo kwa ubunifu wa kuona changamoto kabla hazijatokea.
“Maendeleo ya Taifa hayawezi kujengwa kwa saruji na ramani pekee; yanajengwa kwa maarifa, tafiti, bunifu na uwezo wa kuona kesho kabla haijafika,” amesema Dk Kilama huku akihimiza Chuo Kikuu Ardhi kuendelea kuwa nguzo ya maendeleo kupitia taaluma zao za upangaji miji, ujenzi salama na usimamizi wa ardhi.
Amesisitiza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka bayana kuwa sekta ya ardhi, milki na ujenzi ni miongoni mwa sekta zitakazoendesha mageuzi ya uchumi wa Tanzania.
“Dira hiyo inahitaji kuona huduma za ardhi zikihama kuelekea mifumo ya kidijitali, uwazi, na matumizi ya akili unde (AI) katika usimamizi wa rasilimali hizo,” amesema.
“Tume ya Taifa ya Mipango kuwa iko tayari kupokea mawazo na tafiti zote zinazoweza kusaidia ujenzi wa miji himilivu na miundombinu salama dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Profesa Evarist Liwa amesema maendeleo ya Taifa lolote duniani yanategemea sana uwezo wake wa kuzalisha maarifa, kufanya tafiti na kugeuza bunifu kuwa suluhisho la changamoto za jamii.
Amesema kwa kutambua hili Chuo Kikuu Ardhi kina kitengo maalumu kinachosimamia masuala ya tafiti na machapisho ambacho kinaendelea kuratibu juhudi za watafiti kwenye chuo hicho katika kujibu changamoto za jamii na na miradi yenye athari chanya kwa jamii.
Pia ushirikiano wa kitafiti kutoka ndani na nje ya nchi ambao umefungua milango mingi ya mafunzo, tafiti, ubadilishanaji wa uzoefu na fursa za kimataifa kwa wanafunzi na wahadhiri wetu.
“Wiki hii ya utafiti na ubunifu ni sehemu ya mchango wetu katika kujenga Tanzania yenye wataalamu wabunifu, wenye uwezo wa kutatua changamoto za maendeleo kwa kutumia maarifa na teknolojia,” amesema.
