Changamoto za afya duniani hazijawahi kuwa kubwa kiasi hiki – Guterres kwa Baraza la Afya la DuniaChangamoto za afya duniani hazijawahi kuwa kubwa kiasi hiki – Guterres kwa Baraza la Afya la Dunia

Bwana Guterres punde tu baada ya salamu akaanza kwa kuwakumbusha wahudhuriaji umuhimu wa mkutano huu akisema mkutano huu wa kila mwaka ni fursa muhimu kwa Mataifa Wanachama kuoanisha na kuharakisha juhudi za kukabiliana na changamoto za afya duniani kisha akatahadharisha kuwa kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa kuanzia mwaka jana kunaendelea kuathiri vibaya mifumo ya afya duniani, “Kliniki zimefungwa. Wahudumu wa afya wamepoteza ajira zao. Huduma za kinga, ufuatiliaji na matibabu zimedhoofika. Maisha yamekatizwa mapema.”

Pamoja na changamoto hizo, Katibu Mkuu Guterres amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO kwa kuendelea kutoa uongozi wa kitaalamu na msaada wa dharura kwa nchi zinazokabiliwa na majanga mbalimbali ya kibinadamu.

Amesema WHO imelazimika kupanga upya vipaumbele vyake huku ikiendelea kukabiliana na vitisho vipya vya afya duniani na akasisitiza umuhimu wa kupanua huduma za afya kwa wote pamoja na kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa afya ya binadamu na kwamba, “WHO iko katikati ya mfumo wa afya duniani. Ni lazima ibaki imara na huru, ikiwa na ufadhili wa kutosha na endelevu.”

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kazi ya mkutano huo unaokutanisha wanachama 194 wa WHO ni muhimu kwa usalama wa afya duniani na kwa kufanikisha lengo la afya kwa wote sasa na siku zijazo.

Ameyashukuru mataifa wanachama kwa uongozi, mshikamano na ushirikiano wao katika kujenga dunia yenye afya bora, usalama na usawa zaidi.

Mwisho akawatakia mkutano wenye mafanikio na bila shaka huu ukiwa ni mkutano wake wa mwisho katika uongozi wake unaoelekea ukingoni hadi mwishoni mwa mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *