Hatari ya kupanda malori ya mizigoHatari ya kupanda malori ya mizigo

Dar es Salaam. Safari ya matumaini ya kijana Shukurani Kigodi kutoka Morogoro kwenda Iringa kwa ajili ya msiba iliishia kwenye majonzi baada ya lori alilopanda kupata ajali njiani huku yeye na wenzake wakibaki bila msaada wowote wa fidia kutokana na mazingira ya safari yao.

Kijana huyo aliamua kupanda lori la mizigo mwishoni mwa mwezi uliopita lililokuwa likielekea Iringa baada ya kukosa nauli ya basi.

Kwa mujibu wa ndugu zake, lori hilo lilikuwa limebeba saruji, wakiwa njiani eneo la Mikumi, lilipinduka baada ya dereva kushindwa kulimudu, hali iliyosababisha baadhi ya watu waliokuwamo kwenye gari hilo kupoteza maisha.

Kisa hicho kinafanana na matukio mengi yanayoendelea nchini, wananchi hupanda magari ya mizigo kama malori, Fuso, Canter na magari ya mchanga kwa ajili ya safari au kazi.

Hatari ya magari ya mizigo

Mtaalamu wa masuala ya bima, Dk Anselmi Anselmi anasema watu wanaopanda magari ya mizigo kama abiria wanajiweka katika hatari ya kukosa fidia pindi ajali inapotokea, kutokana na matumizi hayo kuwa kinyume cha sheria na masharti ya bima.

Anasema huduma za bima huongozwa na sheria pamoja na miongozo maalumu inayobainisha mazingira ambayo fidia inaweza kutolewa au kukataliwa.

Dk Anselmi anasema moja ya misingi ya bima ni kutolipa fidia pale hasara inapotokana na kitendo kilichofanywa kinyume cha sheria au masilahi ya umma.

“Mtu amekata bima halafu akapata hasara akiwa anafanya jambo ambalo ni kinyume cha sheria au masilahi ya umma, basi hapo bima hailipi fidia,” anasema Dk Anselmi.

Anasema magari ya mizigo hayajasajiliwa kwa ajili ya kubeba abiria, hivyo yanapotumika kubeba watu yanakuwa yanakiuka sheria za usalama barabarani pamoja na masharti ya bima.

“Gari la mizigo linapotumika kubeba abiria tayari linakuwa linakwenda kinyume cha sheria. Ndiyo maana mara nyingi trafiki wanayakamata na kuyatoza faini,” anasema.

Anasema endapo ajali itatokea kwa mtu aliyepanda kwenye gari la mizigo kama abiria, kampuni ya bima inaweza kukataa kulipa fidia kwa sababu mazingira ya safari hiyo yalikuwa nje ya matumizi halali ya gari husika.

“Aliyepanda pamoja na mwenye gari wote wanakuwa wamekiuka sheria, hivyo inakuwa vigumu kupata fidia ya bima, hata hatua za kisheria dhidi ya mwenye gari zinaweza kuwa ngumu kutokana na kutokuwepo kwa mkataba rasmi wa usafirishaji kama ilivyo kwa mabasi au vyombo vingine vya usafiri wa abiria.”

Anasema ili mtu aweze kudai fidia mara nyingi kunakuwa na ushahidi wa huduma ya usafiri kama tiketi kwenye gari la mizigo hakuna tiketi ya aina yoyote.

Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani, Wilayani ya Kiteto, Raphael Karani akitoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa malori na canter barabara ya Arusha- Lobosiret ya kuacha kupakia abiria kwenye vyombo vya moto visivyoruhusiwa kwa kuwa ni kosa kisheria. Picha na Jeshi la Polisi

Akizungumzia watu wanaosafiri kwenye magari ya mizigo wakidai wanafuatana na mali zao au mzigo wao, Dk Anselmi anasema hata katika mazingira hayo sheria hairuhusu mtu kuwa ndani ya chombo kinachobeba mzigo.

“Katika utaratibu wa ‘cargo escort’, mwenye mzigo anatakiwa kufuata mzigo wake kwa kutumia gari tofauti na si kukaa ndani ya lori linalobeba bidhaa,” anasema.

Muundo wa sheria

Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani sura 168 ya mwaka 1973 na marekebisho yake ya mwaka 2023, magari ya mizigo yanatakiwa kutumika kubeba mizigo na si abiria isipokuwa kwa ruhusa maalumu.

Sheria hiyo inaeleza matumizi ya gari nje ya usajili wake ni kosa na yanaweza kuondoa uhalali wa madai ya bima pale ajali inapotokea.

Sheria hiyo pia inaweka wajibu kwa wamiliki wa magari kuhakikisha vyombo vyao vinatumika kwa madhumuni yaliyoidhinishwa kisheria, huku kanuni za usalama barabarani zikikataza kubeba abiria kwenye magari ya mizigo bila kibali maalumu.

Wakili Haron Sanga anasema kampuni nyingi za bima hulipa fidia kwa kuzingatia masharti ya matumizi ya gari yaliyopo kwenye mkataba wa bima.

“Ikiwa gari limekata bima ya kubeba mizigo pekee, basi watu waliopandishwa kama abiria wanaweza kutotambuliwa katika fidia,” anasema Sanga.

Anasema changamoto kubwa ni wananchi wengi kutofahamu tofauti kati ya gari la mizigo na gari la abiria katika sheria za usafiri na bima.

“Watu wanaamini bima inalinda kila aliyepo ndani ya gari, lakini kisheria matumizi ya gari ndiyo msingi wa madai ya fidia,” anasema.

Kwa mujibu wa Sheria ya Leseni za Usafirishaji ya mwaka 1973 sura 317, magari yanayotumika kubeba abiria yanapaswa kuwa na leseni maalumu ya usafirishaji wa abiria na kutimiza masharti ya usalama kwa wasafiri.

Taasisi za malori

Naibu Katibu wa Chama cha Madereva wa Malori Tanzania (Chamamata), Muhidini Sangoti anasema kitendo hicho ni kinyume cha sheria za usafirishaji na ndani ya magari hayo hawapaswi kuwepo watu zaidi ya wawili ambao ni dereva na msaidizi wake.

“Ukikuta kuna mtu wa tatu ndani ya lori lazima utoe maelezo, inaweza kuwa ni fundi au dereva mwenzako anayefata gari lililoharibika, lakini kisheria bado ni kosa,” anasema Sangoti.

Anasema mara nyingi polisi wanapokamata lori lenye watu zaidi ya wawili huchukulia kuwa ni abiria waliopandishwa, jambo ambalo huleta changamoto kwa madereva hata pale wanapombeba mfanyakazi mwenzao kwa msaada wa usafiri.

Sangoti ametoa mfano wa dereva anayesafiri kwenda Morogoro akiwa na dereva mwenzake anayefanya kazi kampuni moja, polisi wanaweza kuona ni kosa licha ya kuwa si abiria wa biashara.

“Ni kosa kisheria, lakini wakati mwingine ni hali ya kusaidiana tu miongoni mwa madereva,” anasema.

Abiria waliokuwa wanakwenda mnadani  na gulioni wilayani Simanjiro wakishushwa kwenye Fuso la kubebea mizigo.

Aidha, anasema tatizo hilo linaonekana pia kwa baadhi ya magari ya kubeba mchanga, baadhi ya watu hupandishwa kwa madai ya kusaidia kuelekeza maeneo ya kushusha mchanga au kusaidia kazi ndani ya gari.

Kutokana na changamoto hizo, anasema wameitwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani jijini Dodoma kwa ajili ya kikao cha kujadili namna ya kukabiliana na tatizo hilo na changamoto nyingine zinazowakabili madereva.

“Tumeitwa na viongozi wa usalama barabarani Dodoma ili tukajadili changamoto hizi na kutafuta suluhisho,” anasema.

Anasema taasisi yao inalenga kusimamia taaluma ya udereva, kutoa elimu kwa madereva na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili barabarani.

“Zipo changamoto nyingi ambazo tunapaswa kuzisimamia kama taasisi ya taaluma ya madereva Tanzania,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo (Tamstoa), Chuki Shabani anasema sheria hairuhusu madereva kubeba abiria kwenye malori, akieleza kitendo hicho ni hatari na kinaweza kusababisha matatizo makubwa pindi ajali zinapotokea.

Anasema kwa kawaida dereva wa lori anatakiwa kuwa peke yake au kuwa na msaidizi maalumu anayejulikana na mwajiri, hivyo si rahisi kwa tajiri kujua kila kinachoendelea njiani.

“Dereva anakuwa peke yake akiwa safarini. Tajiri ni ngumu kujua kila kinachoendelea kwa sababu hayupo ndani ya gari,” anasema.

Anasema hata suala la kuwa na kondakta au msaidizi ndani ya lori nalo limewekewa masharti maalumu, si kila lori linapaswa kuwa na msaidizi.

“Hata kondakta wengine hawaruhusiwi kuna magari dereva anatakiwa kuwa peke yake kwa sababu anapata muda mrefu wa kupumzika akiwa safarini,” anasema.

Anafafanua kuwa katika safari ndefu, dereva hulazimika kupaki gari na kupumzika anapochoka, hivyo uwepo wa watu wasiokuwa rasmi ndani ya lori unaweza kuongeza changamoto na hatari barabarani.

Aidha, anawataka madereva kuacha tabia ya kubeba watu bila utaratibu kwa kuwa, ni kinyume cha sheria na taratibu za kazi.

Anasema chama hicho kitaendelea kutoa elimu kwa madereva na wamiliki wa malori ili kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa.

Jeshi la polisi

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Polisi Wilaya ya Kiteto, Raphael Karani, Mei 01, 2026 alikagua na kutoa elimu ya Usalama Barabarani kwa madereva wa Malori na Canter Barabara ya Arusha – Lobosiret kupitia Sukuro.

Aliwataka kuacha tabia ya kupakia abiria kwenye vyombo vya moto visivyoruhusiwa kwani ni kosa kisheria na huweza kusababisha ajali barabarani
Alisema hayo alipozungumza na madereva na abiria wafanyabiashara wa Mnadani na Gulioni wilayani Simanjiro huku akihimiza utii wa sheria na kanuni za usalama barabarani bila ya shuruti ili kuepuka ajali.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, William Mkonda anasema wanaendelea kufanya operesheni dhidi ya makosa hatarishi barabarani, ikiwamo tabia ya kupakia abiria kwenye magari ya mizigo, ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara unaimarika.

Mkuu huyo anasema pamoja na kusimamia sheria, jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani.

“Hii inaonesha namna tunavyosimamia sheria kwa kufanya operesheni endelevu dhidi ya makosa hatarishi ya usalama barabarani katika kuhakikisha barabara zetu zinaendelea kuwa salama,” anasema Mkonda.

Anasema Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua dhidi ya madereva wanaokiuka sheria, huku akitoa rai kwa wananchi kushirikiana na mamlaka husika ili kupunguza ajali na kufanya barabara kuwa salama kwa wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *