Ni wiki ya madaraja na malipo kwa makandarasiNi wiki ya madaraja na malipo kwa makandarasi

Dodoma. Wakati Bunge likitarajia kuhitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara Maliasili na Utalii leo Jumatatu, Mei 17, 2026, wizara tatu zitawasilisha mapendekezo ya kuomba bajeti zao kwa mwaka wa fedha 2026/27 wiki hii.

Wizara zitakazowasilisha bajeti zao ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliyopangiwa siku moja kama Wizara ya Viwanda na Biashara, huku Wizara ya Ujenzi ikipewa siku mbili za uwasilishaji wa mjadala wa bajeti hiyo.

Hata hivyo, Jumatano na Alhamisi ndizo siku zinazotarajiwa kuwa na mvutano mkali kutoka kwa wabunge, kwani ndipo itakapojadiliwa Hotuba ya Wizara ya Ujenzi ya Waziri Abdallah Ulega ambayo kwa namna yoyote haitajitenga na miundombinu ya barabara, madaraja na masuala ya malipo ya makandarasi.

Tangu kuanza kwa mkutano wa tatu wa Bunge la bajeti, hotuba iliyopita kwenye misukosuko mingi ni Wizara ya Maliasili na Utalii iliyosomwa mwisho mwa juma na hitimisho lake linatarajia kuwa leo.

Kwenye michango ya wabunge, wengi wameonyeshwa kutoridhishwa na namna Serikali inavyoshughulikia mipaka kati ya makazi ya watu na hifadhi, ongezeko la wanyama kama tembo na mamba namna linavyoshughulikiwa na ulipaji wa kifuta machozi kwa waliojeruhiwa na wanyama.

Lingine lililojadiliwa zaidi ni uharibifu wa mazao kutokana na wanyama, uonevu wa askari wa wanyama kwa binadamu, lakini wakagusia pia weledi wa watumishi kwenye maeneo mengi hadi kusababisha migogoro na wananchi.

Mbunge wa Katavi, Thomas Kampala, alisema Wizara hiyo imekosa mwelekeo katika suala la uwekaji mipaka kwani kila sehemu imeweka vigingi mkoani Katavi, lakini kila wakati wamekuwa ni watu wa kusogeza na kuanzisha migogoro na wananchi.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo, alisema hakuna mwananchi anayeanzisha migogoro ya ardhi bali Wizara ya Maliasili na Utalii ndiyo imekuwa chanzo kwa kusogeza mipaka bila utaratibu, huku Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, akitaka hatua kuhusu mauaji yanayosababishwa na askari wa hifadhi.

Kwa maana hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji atakuwa na kazi ya kujibu hoja za wabunge ili kuwashawishi waipitishe bajeti yake.

Wizara ya Ujenzi

Kwa upande wa Wizara ya Ujenzi, dalili za mapema zilianza kujionyesha wakati wa kuchangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu ambapo wabunge wengi walilalamikia kutokulipwa kwa makandarasi wanaotekeleza ujenzi wa miundombinu maeneo mbalimbali nchini.

Mbali na michango kwenye hotuba hiyo, lakini kipindi cha maswali, hoja ya kutolipwa kwa makandarasi imekuwa ikiibuliwa mara nyingi hata kwenye maswali ya nyongeza jambo linaloonyesha kutakuwa na mvutano kwenye wizara hiyo.

Hivi karibuni Mbunge wa Mpwapwa, George Malima, alihoji kuondoka kwa mkandarasi Estim Construction Ltd anayejenga barabara ya kutoka njiapanda ya Kongwa hadi Idilo (kilomita 32) akihusisha na kutolipwa na badala yake akaanza kujihusisha na ubomoaji wa milima akiponda kokote mradi ambao haukuwepo kwenye mkataba.

Hoja ya Mbunge huyo iliwainua wabunge wengi wakataja namna makandarasi walivyoikimbia miradi kwa kisingizio cha fedha licha ya Waziri wa Ujenzi kunukuliwa mara kadhaa akisema fedha siyo tatizo bali makandarasi wanatakiwa kuendelea na kazi.

Kingine kitakachojadiliwa zaidi ni uharibifu wa barabara uliotokana na mvua kubwa za mwaka huu ingawa jambo hilo limegawanyika katika maeneo mawili kwani miundombinu mingine inahudumiwa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

“Waziri huwa anasema lakini siyo kweli, mimi nimedai fedha kwa muda mrefu sana na mwisho mtu unaamua kusimama maana unajikuta una madeni kila mlango, namshukuru Mungu kuna vijisenti wamenilipa majuzi na nimepanga kurudi saiti,” amesema mmoja wa makandarasi aliyeomba asitajwe jina.

Mjenzi huyo katika moja ya miradi ya barabara mkoani Dodoma, amesema kada yao inapitia wakati mgumu kwani mara nyingi wanakosa kujitetea lakini anayekwamisha au kuchelewesha kazi huwa ni Serikali yenyewe.

Wizara ya Ulinzi

Kwa upande wa Wizara ya Ulinzi, uzoefu unaonyesha huwa inapita bila misukosuko ingawa suala la ulipaji wa fidia kwa maeneo yanayotwaliwa na jeshi huwa ni kipengere chenye kelele nyingi na wakati mwingine utaratibu wa vijana kujiunga na jeshi.

Wizara ya Viwanda pia huenda isiwe na mjadala mkubwa, kwani ni jambo lililo wazi kwenye uwekezaji kwa wenye uwezo ili kutengeneza ajira na kukuza uchumi.

Viwanda vilivyobinafsishwa kwa watu wengine lakini haviendelezwi huenda ukawa moja ya hoja zitakazojadiliwa.

Mara nyingi wabunge wamekuwa na mapendekezo ya kutaka Serikali ivirudishe mikononi mwaka au kuwakabidhi wawekezaji wenye nia ya kuviendeleza, badala ya ambao wamevichukua na kuweka kama sehemu ya maghala ya kuhifadhia bidhaa zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *