
Chato. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewarejesha wagombea udiwani watano kutoka kata ya Bwongera, Jimbo la Chato Kaskazini, waliokuwa wamekata rufaa wakipinga msimamizi msaidizi kutowateua kugombea kwenye kata hiyo.
Uchaguzi wa udiwani kata ya Bwongera, unafanyika baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Batholomeo Manunga kufutwa uanachama na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa makosa ya kinidhamu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Mei 18, 2026 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima, Tume ilipokea rufaa za wagombea watano ambapo katika kikao chake cha awali kilichofanyika Ijumaa Mei 15, 2026, rufaa mbili zilikubaliwa.
“Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 65(7) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea rufaa tano za wagombea udiwani wanaopinga uamuzi wa msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kata ya Bwongera wa kutowateua kuwa wagombea,” inaeleza taarifa hiyo.
Aidha, katika kikao chake kilichofanyika leo Mei 18, 2026, INEC imepitia na kuridhia rufaa tatu zilizokuwa zimesalia na kuwarejesha wagombea hao kuendelea na mchakato wa uchaguzi. Wagombea waliokata rufaa na kurejeshwa ni Anastazia Bampiga (UPDP), Ramrath Abdul (NLD), Magreth Masasi (Makini), Zena Said (TLP) na Hanifa Mohamed (UMD).
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Chato Kaskazini, Geriad Mgoba amesema katika uchaguzi huo, wagombea tisa kutoka vyama tofauti walijitokeza kuwania nafasi hiyo ambapo baada ya kupitia vielelezo vyao, wagombea wanane walibainika kukosa sifa.
Mgoba amesema wagombea wanane kati ya tisa walienguliwa baada ya kushindwa kuwasilisha vielelezo vinavyothibitisha kuwa ni wakazi wa kata hiyo ambapo wagombea watano walikata rufaa, huku wengine watatu wakishindwa kuwasilisha rufaa zao.
“Mimi kazi yangu ilikuwa ni moja tu kupokea vielelezo na kuvipeleka Tume, baada ya kuvipeleka Tume imewarejesha. Wagombea watano walikata rufaa na watatu hawakukata rufaa, kwa hiyo waliridhika na zile sababu kama hawajaridhika wangefanya kama ambavyo wamefanya wenzao na sheria inawaruhusu kwamba kama hawajaridhika wanakata rufaa,” amesema.
Wagombea waliorejeshwa wanatarajiwa kukabidhiwa barua za uteuzi kesho na kuendelea na kampeni zilizoanza Mei 11, 2026 ambazo zinatarajiwa kufungwa Mei 30, 2026 huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Juni 1, 2026.
