Bei ya mafuta ilivyopandisha mahitaji ya kufunga gesi kwenye magariBei ya mafuta ilivyopandisha mahitaji ya kufunga gesi kwenye magari

Dar es Salaam. Kupanda kwa bei ya mafuta nchini kumegeuza biashara ya ubadilishaji wa magari kutumia gesi kuwa moja ya huduma zinazotafutwa zaidi kwa sasa huku kampuni nyingi zikizidiwa na idadi ya wateja wanaohitaji huduma hiyo.

Uhitaji huo ulioongezeka umefanya baadhi ya kampuni kuwapa kipaumbele wale wanaokwenda na fedha taslimu na kuacha kutoa kwa muda mikopo kwa wale waliokuwa wakilipia kidogokidogo hali inyochochewa na uhaba wa vifaa.

Hilo limeenda sambamba na kuongezeka kwa bei ya ufungaji mifumo hiyo huku mtungi wa kilo 11 ambao unatumiwa na wengi, sasa umefika hadi Sh2.1 milioni, Sh1.9 milioni na Sh1.8 milioni ikiwa ni ongezeko kutoka Sh1.5 milioni hadi Sh1.65 milioni iliyokuwa ikitozwa na baadhi ya kampuni kabla ya hali hii.

Hali hii sasa imefanya baadhi ya kampuni kuwa na oda hadi za watu 300 wanaosubiri huduma huku kuchelewa kwa meli kukitajwa kuwa kitu kinachochelewesha huduma hiyo inayoonekana kama mkombozi kwa sasa.

Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazoshuhudia athari hasi kupitia ongezeko la bei za mafuta kufuatia vita inayoendelea mashariki mwa kati ambayo imesababisha mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu ya uzalishaji, uhifadhi na usafishaji wa mafuta ikiwamo visima vya uzalishaji, maghala ya kuhifadhi na viwanda vya kusafisha mafuta na hivyo kuathiri uwezo wa uzalishaji.

Hali hii imefanya sasa wakazi wa Jiji Dar es Salaam ambao ndiyo wanufaika wa uwepo wa vituo vya kujaza gesi kununua lita moja ya petroli kwa Sh4,115, dizeli kwa Sh4,248 na mafuta ya taa kwa Sh4,677.

Ikilinganishwa na gesi ambayo inauzwa kwa Sh1,550 kwa kilo, inakuwa ni pungufu ya Sh2,565 kwa watumiaji wa petroli na Sh2,698 kwa watumiaji wa dizeli.

“Tofauti ni kubwa sana kwa sasa, mahitaji yameongezeka ukilinganisha na siku za nyuma kwa sababu kila mtu anatafuta namna ya kupata ahueni ila changamoto iliyopo sasa ni upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya kuhudumia wateja hao,” amesema Ofisa Masoko Aron Dosha kutoka Kampuni ya Exogas Green Solution Limited.

Amesema hivi sasa kwa siku wanapata zaidi ya simu 100 za watu wanaoulizia gharama za kubadili mifumo yao kwenda kwenye gesi wakati ambao watu zaidi ya 300 wapo wanasubiri huduma.

“Vifaa ndiyo changamoto kubwa kwa sasa, tuliagiza mzigo meli ikachelewa. Hali hii imefanya tusitishe huduma kwa wale wanaohitaji kulipa kidogo kidogo yaani mkopo na tuwape kipaumbele wale wanaolipia fedha taslimu kwa vifaa kidogo tulivyonavyo,” amesema.

Amesema hali hiyo sasa imefanya mtungi wa kilo 11 ambao unafungwa na watu wengi kulipiwa Sh1.8 milioni kutoka Sh1.65 milioni waliyokuwa wakitoza kabla ya mapigano haya.

“Mtu akiwa na vifaa vichache, huwezi kuuza kwa Sh1.5 milioni au Sh1.65 milioni, lazima aongeze kwa sababu mahitaji ni makubwa na kila kitu kimeongezeka,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya EAM Autogas Garage, Emmanuel Mwakaje amesema licha ya gharama za ufungaji kurudi kule zilipokuwa awali lakini uhitaji wa watu umekuwa mkubwa zaidi.

Amesema kabla ya mapigano katika nchi za mashariki ya kati, watu waliokuwa wakibadili mifumo hiyo kwenda kwenye gesi walikuwa wachache, lakini pia hata wateja walikuwa hawapatikani tofauti na sasa wafungaji wako wengi na wateja ni wengi zaidi.

“Mahitaji yanapoongezeka bei lazima iongezeke kidogo na asilimia kubwa ya watu wanaokuja kufunga wanataka mitungi ya kilo 11 ambayo ndiyo inakaa kwenye magari madogo,” amesema.

Amesema mitungi hiyo kabla ya hali inayoendelea sasa duniani, ilikuwa ikifungwa hadi kwa kati ya Sh1.6 milioni hadi Sh1.6 milioni na mazungumzo yakawepo, lakini sasa bila Sh1.8 mtu hawezi kufungiwa na hakuna mazungumzo.

“Kipindi cha nyuma biashara ilikuwa ngumu, tulifanya kila kitu ili kumvutia mteja kwa sababu watu walikuwa hawana motisha ya kufunga hivyo wateja wakawa wachache, vifaa vilikuwa havijapanda bei lakini sasa wanaohitaji kufunga mfumo huo wameongezeka ili kukwepa gharama za mafuta wakati ambao vifaa hakuna,” amesema.

Akitaja bei za kubadili mifumo amesema mtungi wa kilo 4.5 sasa unafungwa kwa Sh1 milioni, kilo 6 (Sh1.2 milioni), kilo 11 Sh(1.8 milioni), Kilo 15 (Sh2.2 milioni) kilo 17 (Sh2.5 milioni) bila mazungumzo.

Bei hizi za sasa, kabla ya mapigano ya Mashariki ya kati, kampuni zililazimika kuweka bei zinazowavutia wateja kwa wengine kupunguza Sh200,000 hadi Sh250,000 ili kupata wateja.

Mkurugenzi kutoka Nk CNG Auto Limited, Nurdin Kombo ambao pia wamelazimika kusitisha huduma ya mkopo kwenye ufungaji wa mifumo ya gesi, amesema kwa sasa bei ya mtungi wa kilo 11 umefikia kati ya Sh1.9 milioni hadi Sh2 milioni.

“Unajua hii changamoto ya vifaa imeongezeka kutokana na mahitaji kukua kwa kasi, hii imefanya tasnia kuzidiwa na watu wengi kulazimika kuagiza vifaa kwa haraka. Hivyo baada ya muda fulani nadhani bei itarudi kule ilipokuwa,” amesema.

Akitolea mfano wa kampuni yake, amesema wanatarajia vifaa vingine kufika Juni au Julai hususani mitungi ambayo haiwezi kusafirishwa kwa meli huku wakilazimika kutumia ndege kuleta vifaa vidogo vidogo.

“Kila mtu aliyeagiza vifaa vyake vikiingia, mali zitagongana sokoni kwa wakati mmoja, hivyo bei itashuka ila kwa sasa kuna watu tumewaambia wasubiri kwanza wakati tukisubiri vifaa ili wapewe huduma,” amesema.

Hali ilivyo DIT

Wakati kampuni binafsi zikilalamika kuzidiwa na wateja na kukosa vifaa, Meneja wa mradi wa kuunganisha mfumo wa gesi asili katika magari (CNG) katika Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Dk Esebi Nyari amesema bado wanavyo vifaa vya kutosha.

“Kweli, idadi ya wateja imeongezeka tofauti na hapo nyuma tulikuwa tunapata shida kuwapata ila sasa kila siku wateja wanapiga simu na kuja kubadili mifumo. Kwa siku tunahudumia gari nne kulingana na uwezo wetu,” amesema.

Akizungumza mmoja wa madereva, Victor Mashaka alilalamikia kuongezeka kwa bei za kufunga mifumo hiyo akitaka ifanyike namna kuzipunguza.

“Kama hukuweza wakati ule kulipokuwa na nafasi ya kufanya mazungumzo, sasa hivi huwezi, wanataja bei wanaangalia na pembeni, bila Sh2 milioni, wengine Sh1.9 milioni hutoboi,” amesema.

Hayo yanaelezwa wakati ambao bajeti ya Wizara ya Nishati ya mwaka 2026/2027 inaeleza hadi sasa vyombo vya usafiri na usafirishaji zaidi ya 20,000 vinavyotumia gesi asilia.

Vilevile, hadi Machi 2026, kampuni binafsi 86 za ndani na nje ya nchi zilikuwa zimepewa idhini ya kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa gesi asilia nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *