Mayele kuijaza mamilioni Pyramids FC Kombe la DuniaMayele kuijaza mamilioni Pyramids FC Kombe la Dunia

Dar es Salaam. Kuteuliwa kwa Fiston Mayele katika kikosi cha timu ya Taifa ya DR Congo kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Dunia 2026 huko Marekani, Canada na Mexico, kutaifanya klabu ya Pyramid ya Misri kuvuna kiasi kisichopungua Dola 198,000 (Sh514 milioni) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Pyramids FC inaweza kuvuna fedha zaidi kutoka FIFA iwapo DR Congo itafanikiwa kuingia hatua za mtoano za mashindano hayo.

Fedha hizo ambazo Pyramids FC itavuna kupitia Mayele, zinatokana na gawio ambalo FIFA inalitoa kwa klabu ambazo wachezaji wao wameitwa katika vikosi vya timu za taifa vinavyoshiriki Kombe la Dunia ambapo kwa kila mchezaji, FIFA inalipa kiasi cha Dola 11,000 (Sh29 milioni) kwa kila siku ambayo anakuwepo katika fainali hizo.

Kanuni za mashindano hayo zinalazimisha kila timu kuwasili katika nchi ambayo fainali hizo zinachezwa siku tano kabla ya kuanza kwake hivyo DR Congo kuanzia inawasili hadi itakapomaliza hatua ya makundi itatumia siku 18.

Katika kila siku moja ambayo Mayele atakuwepo na DR Congo kwenye Kombe la Dunia, Pyramids FC itapata Dola 11,000 hivyo kwa siku 18, itapata Dola 198,000.

Mayele ni miongoni mwa washambuliaji wanne walioitwa na kocha Sébastien Desabre kwa ajili ya mashindano hayo makubwa duniani.

DR Congo imerejea kwenye Kombe la Dunia baada ya miaka 50 tangu iliposhiriki kwa mara ya mwisho mwaka 1974 ilipokuwa ikijulikana kama Zaire.

Kocha Desabre amesema anaendelea kuwaamini wachezaji ambao wamekuwa sehemu ya timu hiyo kwa miaka kadhaa huku akisisitiza kuwa Kombe la Dunia sio sehemu ya kufanya majaribio ya kikosi.

Katika kikosi hicho pia amerejea kiungo mkongwe Gael Kakuta ambaye hakuitwa kwenye baadhi ya mechi za hivi karibuni za DR Congo.

Katika hatua ya makundi, DR Congo imepangwa kundi K pamoja na Ureno, Colombia na Uzbekistan.

KIKOSI CHA DR CONGO KOMBE LA DUNIA 2026

Makipa: Matthieu Epolo (Standard Liege), Timothy Fayulu (Noah) na Lionel Mpasi (Le Havre)

Mabeki: Dylan Batubinsika (Larisa), Rocky Bushiri (Hibernian), Gedeon ‌Kalulu (Aris Limassol), Steve Kapuadi (Widzew Lodz), Joris Kayembe (Racing Genk), Arthur Masuaku (Racing Lens), Chancel Mbemba (Lille), Axel Tuanzebe (Burnley) na Aaron Wan-Bissaka (West Ham United)

Viungo: Theo Bongonda (Spartak Moscow), Brian Cipenga (Castellon), Elia Meshack (Alanyaspor), Gael Kakuta (Larissa), Edo Kayembe (Watford), Nathanael Mbuku (Montpellier), Samuel Moutoussamy (Atromitos), Ngalayel Mukau (Lille), Charles Pickel (Espanyol) na Noah ⁠Sadiki (Sunderland)

Washambuliaji: Cedric Bakambu (Real Betis), ⁠Simon Banza (Al Jazira), Fiston Mayele (Pyramids) na Yoane Wissa (Newcastle United)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *