
Dar es Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetangaza wateule 18 wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2026 huku mwandishi wa Mwananchi Devotha Kihwelo akiwa ni miongoni mwa wateule hao.
Akizungumza katika halfa ya kutangaza wateulie hao wa msimu wa 16 iliyofanyika ofisi za Uwezo Tanzania leo Jumanne, Mei 19, 2026, Katibu Mtendaji wa MCT, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Ernest Sungura amesema vimetumika vigezo vya msingi takribani kumi katika kuchuja kazi 594 za waandishi walizozikisanya.
Vigezo hizo ni fikra asilia ya mwandishi, ni kuzingatia misingi ya uandishi wa habari, ripoti ya kina na utafiti, vyanzo vingi tofauti vyenye uhusiano na wakati na mashiko kwa maana habari inahusu jambo ambalo lipo na wakati huu.
Kigezo kingine ni ubora wa kazi ikihusisha ubunifu na uwasilishaji, ufahamu wa kina wa mada na stadi za kuhoji, kutoa taarifa mpya, namna nzuri ya uwasilishaji ikiwamo kufuata kwa hoja na mwisho ni athari kwa umma, kwa kuandika kwake mwandishi umma umepata faida gani.
Katika mchakato huo Sungura ameweka bayana kuwa jopo la majaji 12 waliohusika kujivunia matumizi ya dijitali katika uchakataji wa kazi za waandishi.
“Wateule hao 18 ni Shaban Hamisi wa Nipashe, Simon Mkina wa Pambazuko Oline, Daniel Samson wa Nukta Africa, Diki Kanyika Sahara Media, Mackriner Siyovelwa Crown Digital.
“Esau Ng’umbi wa Nukta Africa, Sanula Athanas wa Nipashe, Abel Kilumbu EATV, Francis Kajubi wa The Guardian, Devotha Kihwelo wa Mwananchi, Vitus Medard wa The Guardian.”
Wengine ni Anthony Rwekaza wa Watetezi Online Tv, Neema Abel wa The Guardian, Isack Lukumay wa Orkonerei FM, Joseph Kirati wa The Chanzo, Kelvin Makwinya wa Nukta Africa, Abdallah Kurwa wa ITV na Huwaida Moh’d wa Assalaam FM.
Sungura amesema kazi hizo ziliingizwa kwenye mfumo wa kidijitali uliotengenezwa ambao ulitoa kazi 60 za waandishi ambazo hazikukidhi vigezo.
“Majaji wamefanyia kazi kila mmoja na sehemu alipokuwa si kama zamani walikuwa wanakutana kwa pamoja. Wamekuja wateule 18 kwa kukidhi viwango vya ubora ambao tunautaka,” amesema.
Aidha kati ya waandishi hao 18 zitapunguzwa na mwisho washindi watatangazwa katika hafla ya Mei 29, 2026 jijini Dar es Salaam.
Tuzo za mwaka huu zinahusu kazi za mwaka 2024 na mwaka 2025 ambapo washindi watapata kiwango cha pesa kilekile cha miaka yote.
“Tuzo hizi si kwa ajili ya pesa na hatuko hapa kushindana, EJAT inaendelea kuheshimu utaaluma na weledi kwa habari zinazoleta mabadilikko kwenye jamii,” amesema.
Kwa upande wake, Jaji Beatrice Bandawe amesema mfumo mpya wa kidijitali wa kuchakata kazi za washiriki ni mabadiliko makubwa katika historia ya tuzo hizo zinazowakutanisha wanahabari kutoka vyombo mbalimbali nchini.
Aidha, mfumo huo mpya wa umeleta mabadiliko katika uchujaji wa kidijitali kabla ya majaji, tathimini bila upendeleo na kigezo cha ushahidi wa athari.
