
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetoa maagizo na hatua 10 za dharura za kuimarisha ulinzi dhidi ya ugonjwa wa Ebola kufuatia mlipuko ulioripotiwa katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Hofu ya kusambaa kwa ugonjwa huo imeongezeka katika ukanda wa Afrika Mashariki baada ya mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuthibitisha kuwa watu wasiopungua 131 wamefariki dunia kutokana na mlipuko mpya wa ugonjwa huo huku zaidi ya 500 wakiambukizwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma jana Mei 18, 2026, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe Tanzania bado ipo salama na haina mgonjwa yeyote wa Ebola, lakini Serikali imeongeza tahadhari kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu na shughuli za kiuchumi kati ya Tanzania na nchi zilizoathirika.
Taarifa hiyo imekuja siku chache baada ya nchi hizo mbili kutangaza uwepo wa mlipuko wa Ebola, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likitangaza ugonjwa huo kuwa dharura ya kiafya ya kimataifa.
Dk Magembe amesema Serikali imeanza kutekeleza hatua mbalimbali za kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini, ikiwemo kuimarisha uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia kupitia mipaka, bandari na viwanja vya ndege.
“Serikali imeendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo kupitia afua mbalimbali za kinga, ufuatiliaji na utoaji wa elimu kwa umma,” imeeleza taarifa hiyo.
Miongoni mwa maagizo hayo 10 ni kuimarisha ufuatiliaji wa tetesi katika jamii, kupeleka timu za wataalamu wa kitaifa katika mikoa yenye hatari kubwa, kuimarisha vituo vya afya na kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa kinga pamoja na tiba muhimu.
Hatua nyingine ni kuendelea kutoa elimu ya afya kupitia televisheni, redio na mitandao ya kijamii, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa afya mipakani na nchi jirani kwa ajili ya kubadilishana taarifa za tahadhari.
Aidha, Serikali imewaelekeza waganga wakuu wa mikoa kuamsha timu za wataalamu wa afya na kubainisha vituo maalumu vya kuhudumia wagonjwa endapo kutatokea maambukizi.
Pia, mwongozo mpya wa wasafiri (Travel Advisory) utaanza kutumika leo Mei 19, 2026 ili kusaidia utekelezaji wa hatua za kinga kwa mujibu wa Kanuni za Afya za Kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ebola husababishwa na virusi vinavyoenea kutoka kwa popo na wanyama jamii ya sokwe kwenda kwa binadamu, na baadaye kusambaa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kupitia kugusa majimaji ya mwili wa mgonjwa au mtu aliyefariki kutokana na ugonjwa huo.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa, maumivu ya misuli, uchovu mkali, kuumwa kichwa, kutapika na kuharisha. Baadhi ya wagonjwa wanaweza kupata vipele au kutokwa damu katika sehemu mbalimbali za mwili kama macho, pua na mdomo.
Serikali imewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya watu wenye dalili za Ebola pamoja na kuepuka kula mizoga ya wanyama.
Wananchi pia wametakiwa kuwahi katika vituo vya afya wanapoona dalili zinazofanana na Ebola na kutoa taarifa kupitia namba ya dharura 199 iwapo watabaini mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
“Wananchi waendelee kupata taarifa kutoka kwenye vyanzo rasmi vya Serikali ili kuepuka upotoshaji,” imeeleza taarifa hiyo ya Dk Magembe.
Wakati huohuo, watumishi wa afya wamekumbushwa kuzingatia kanuni za kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa.
