
Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imeziondoa baadhi ya mali katika orodha ya mali za mbunge wa zamani wa viti maalum (CCM), Askofu Getrude Rwakatare kwa kuwa hazikuwa mali binafsi bali za St. Mary’s International Academy Limited.
Uamuzi huo umetolewa jana Jumatatu, Mei 18, 2026 na majaji watatu wa Mahakama hiyo iliyoketi Dar es Salaam ambao ni Augustine Mwarija, Pantrine Kente na Zainab Muruke, wakati wakitoa uamuzi wa maombi ya mapitio namba 1591 ya 2024.
Maombi ya mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam, Kituo Jumuishi Temeke yaliotolewa Desemba 6, 2024 na Jaji Glady’s Barthy, yalifunguliwa na mtoto wa marehemu, Kellen Rwakatare na St. Mary’s International Academy Limited.
Mchungaji Rwakatare alikuwa mbunge kupitia Mkoa wa Morogoro na mwanzilishi wa Kanisa la Mlima wa Moto lililopo Mikocheni jijini Dar es Salaam na pia mwanzilishi wa shule za St. Mary’s International Academy zilizopo maeneo mbalimbali nchini.
Hata hivyo, Aprili 20, 2020 alifariki dunia jijini Dar es Salaam pasipo kuacha wosia wowote ndipo watoto wake, Kellen Rwakatare, Tibe Rwakatare, Humphrey Keneth na Mutta Rwakatare, walipoomba na kuteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi yake.
Baada ya kupewa barua ya usimamizi wa mirathi, wasimamizi hao kwa pamoja, walitakiwa kuwasilisha, ndani ya miezi sita, orodha na hesabu za mali alizoacha mama yao na baadaye kuwasilisha kortini hesabu za mwisho za mirathi.
Wasimamizi hao waliwasilisha hesabu za mwisho za mali za marehemu zenye vitu (item) 38 ambavyo vilihusu mgawanyo wa hisa na mali katika taasisi saba zinazofanya kazi katika viwanja vilivyopo jijini Dar es Salaam na mkoani Mbeya.
Orodha ya mali ilisainiwa na wasimamizi watatu pekee, Tibe, Humphrey na Mutta ambao walikuwa wajibu maombi katika maombi ya mapitio (revision) namba 1591 ya 2024 yaliyofunguliwa na St. Mary’s Internatonal Academy Limited na Kellen.
Kellen ambaye hakusaini orodha hiyo, aliwasilisha pingamizi kwa maelezo kuwa baadhi ya mali hazimilikiwa na marehemu na St. Mary’s International Academy Limited ambayo haikuwa sehemu ya shauri hilo lililokuwa Mahakama Kuu.
Lakini alikwenda mbali na kueleza moja ya mali hizo, kiwanja namba 701 Kitalu 46 eneo la Kijitonyama, Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam ambayo ni mali halali ya marehemu Rwakatare, haikujumuishwa kama sehemu ya mali zake.
Baada ya kusikiliza mawakili wa pande zote mbili, Jaji alitupilia mbali pingamizi la Kellen kwa maelezo kuwa madai ya Kellen kuwa mali alizozitaja zinamilikiwa na St. Mary’s International Academy Limited na sio marehemu, hayakuthibitishwa.
Kuhusiana na malalamiko yake kuhusu mgawanyo mali kwa wajibu maombi, mali ambazo Kellen alikuwa na hisa nyingi, Mahakama iliona kuwa, mgawanyo uliooneshwa chini ya kipengele cha 38 cha orodha ya mali hizo ulikuwa sahihi.
Maombi ya marejeo
Kutokana na kutoridhishwa na uamuzi huo, dhidi ya uamuzi huo, mwombaji wa kwanza (St. Mary’s International Academy), ambaye hakuwa katika kesi ya Mahakama Kuu na Kellen, waliwasilisha ombi la mapitio ya hukumu hiyo.
Maombi hayo yaliwasilishwa Mahakama ya Rufani Tanzania yakiwa yameambatanishwa na kiapo cha pamoja cha waombaji cha Desemba 20,2024 pamoja na kiapo cha wakili wao, Respicius Didade cha Desemba 30,2024.
Katika maombi hayo, waliegemea sababu saba, kwamba Jaji alikosea kwamba baada ya kujulishwa kuwa baadhi ya mali zilizoorodheshwa zilikuwa ni za St. Mary’s International Academy, alijielekeza vibaya na kuikubali orodha hiyo.
Pia, walisema Jaji alimhukumu mwombaji wa kwanza bila kumsikiliza kwa kuamuru mali zake zipelekwe kwenye mirathi ya Mchungaji Rwakatare bila kumpa mwombaji fursa ya kusikilizwa jambo ambalo ni uvunjaji wa wazi wa kanuni za haki asilia.
Kwamba Mahakama Kuu ya Tanzania ilimchukulia kuwa mwombaji kama taasisi au mali binafsi ya marehemu Mchungaji Rwakatare kinyume na sheria.
Mbali na hivyo, walidai Mahakama kuu ilivuka mipaka yake kwa kushughulika na mali ambazo sio sehemu ya mali za Mchungaji Rwakatare kinyume cha sheria na pia alikubali orodha ya mwisho wakati Kellen hakuwa ameshirikishwa.
Halikadhalika walisema Mahakama ilijielekeza vibaya kwa kukubali orodha na hesabu iliyorekebishwa za mirathi ambazo hazikuwa zimeandikwa kwa pamoja na kuidhinishwa na mawakili wao, Armando Swenya na Respicius Didace.
Katika usikilizwaji wa maombi, mawakili Didace na Swenya waliwawakilisha waombaji wakati mjibu maombi wa kwanza aliwakilishwa na wakili Shehzada Walli, wakati wa pili na tatu waliwakilishwa na Fredrick Massawe na Ditto Amri.
Mawakili wa waombaji walijenga hoja kuwa ingawa Dk Rwakatare alikuwa mwanahisa katika St. Mary’s International Academy Limited, hiyo haikumfanya awe mmiliki wa mali za taasisi hiyo, bali zingekuwa ni sehemu ya mali zake.
Walisema ni hisa zake pekee ndio zilipaswa kuorodheshwa kama mali zake.
Akijibu hoja hizo, wakili Walli alisema orodha na hesabu iliyowasilishwa mahakamani ilikuwa halali na hakuna kifungu cha sheria kinachozuia orodha hiyo kuwasilishwa na mmoja wa wasimamizi kama wasimamizi ni zaidi ya mmoja.
Wakili huyo alisema Jaji alikuwa sahihi alipoamua madai ya muombaji wa pili, Kellen kuwa hakuweza kuthibitisha kuwa St. Mary’s International Academy Limited ilikuwa haimilikiwi na Dk Rwakatare bali St. Mary’s International Academy.
Kwa upande wake, wakili Augusti alisema kuhusu mali zinazobishaniwa, aliunga mkono wasilisho la wakili Walli kwamba kulikuwa hakuna uthibitisho uliotolewa mahakamani kuthibitisha kuwa mali hizo ni ya muombaji wa kwanza.
Uamuzi wa majaji
Katika uamuzi wao baada ya kupitia na kupima mawasilisho ya mawakili wa pande zote mbili, majaji walisema ni jambo lililo wazi katika kumbukumbu kwamba mleta maombi wa pili, Kellen hakushirikishwa katika uandaaji wa hesabu za mwisho.
Hii ni kwa sababu wakati wa kusaini orodha na hesabu hizo za mwisho (inventory) alikuwa amelazwa hospitali ya Aga Khan Jijini Dar es Salaam.
“Uwasilishaji wa wakili wa wajibu maombi kwamba mwombaji wa pili alifanya majadiliano pamoja na wajibu maombi na kukubaliana na yaliyomo kwenye orodha ya rasimu, ni kwa maoni yetu hakuna uthibitisho huo,” walisema.
“Kutokana na ukweli kuwa hakukubaliana (na wasimamizi wenzake wa mirathi) kuhusu mgawanyo wa baadhi ya mali za marehemu na kusababisha kupinga uamuzi wa Mahakama ya chini inaunga mkono msimamo wake,”walieleza.
Majaji hao walisema Jaji alikosea alipotumia kifungu namba 104 cha sheria ya Mirathi wakati katika mazingira ya suala hilo, muombaji wa kwanza hakuwa sehemu ya mwenendo wa shauri lililokuwepo mahakama kuu Dar es Salaam.
Kuhusu kiwanja namba 107 kitalu 46 Kijitonyama kujumuishwa katika mali za marehemu, majaji walisema madai ni kuwa kiwanja hicho ni mali ya muombaji wa kwanza, lakini kimejumuishwa kama sehemu ya mali za marehemu.
Majaji hao walisema ukisoma hukumu, inaonekana kwamba Jaji alikuwa anafahamu kuwa, kwa kanuni kwamba anapokufa mwanahisa katika kampuni, kile kinachopaswa kurithiwa na warithi wao ni hisa zake, si mali ya kampuni.
“Hakuna ubishi kuwa ukiacha viwanja vya Kijitonyama, viwanja vingine vyote vipo kwa jina la St Mary’s International, ikifuatiwa na eneo vilipo. Hakuna hata kimoja chenye jina la marehemu,”walieleza majaji katika hukumu yao hiyo.
“Kwa jumla, kwa Jaji wa Mahakama Kuu kushikilia kuwa mali zinazogombaniwa ni mali ya marehemu kulikuwa na makosa,”walisisitiza.
“Malalamiko yalikuwa tu juu ya mali hizo. Kwa sababu hii, suluhisho sahihi ni kubadilisha uamuzi huo kwa kuondoa mali ya mwombaji wa kwanza kutoka katika mirathi ya marehemu hisa alizo nazo katika kampuni ya mwombaji”
“Uamuzi huu unabadilisha kwa kujumuisha katika mirathi ya marehemu, kiwanja namba 701, Kitalu namba 46, eneo la Kijitonyama, Kinondoni Dar es Salaam,” walihitimisha majaji na kusema kila upande utabeba gharama za kesi.
