Dodoma. Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) imesitisha shahada zinazoandaa walimu wanasihi. Kwa mujibu wa mwongozo wa uandaaji na ufundishaji wa mitalaa kwa shahada za ualimu uliotolewa na tume hiyo Februari 2024, shahada za ualimu zinazopewa uzito katika vyuo vikuu kwa sasa ni Shahada ya Sayansi na Elimu na Shahada ya Sanaa na Ualimu.
Hatua hiyo inalenga kuwaimarisha walimu katika masomo mawili ya kufundishia kama alivyoeleza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda Julai 2025”
“Maana yake dozi ya sayansi sasa ndio itakuwa kubwa, wanafunzi watatumia muda mwingi kusoma masomo watakayokwenda kuyafundisha huko wanakoenda kuliko njia za kufundisha.”
Mwongozo huo unajielekeza zaidi katika maudhui ya somo la kufundishia, mbinu za kutawala darasa na mbinu za kufundisha na tathmini. Hakuna kokote mwongozo umetambua haja ya unasihi katika mafunzo ya ualimu.
Ingawa nafasi ya vyuo kuwa na somo la saikolojia ya ualimu ingalipo, somo hili hata hivyo hujikita zaidi kwenye sayansi ya ujifunzaji na si kujenga uelewa mpana wa mwanafunzi kama mtu mwenye hisia, changamoto na mahitaji ya kihemko.
Sera ya Elimu inasemaje?
Hatua hiyo ya kutotambua moja kwa moja huduma ya unasihi kama sehemu ya mafunzo ya ualimu inakinzana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023) iliyotamka bayana kuwa huduma ya malezi na unasihi ni sehemu muhimu ya ujifunzaji.
Kipengele 3.8 cha sera kinachozungumzia mazingira salama na rafiki katika utoaji wa elimu na mafunzo, kina sehemu ya 3.8.3 inayosema:
“Serikali, kwa kushirikiana na wadau, itaongeza utoaji wa huduma stahiki za unasihi na ushauri nasaha katika viwango vyote vya elimu na mafunzo.”
Takwa hili la kisera lilianza mwaka 2002 wakati Wizara ya Elimu na Utamaduni (wakati huo) ilipotoa Waraka Na. 11 wa Mwaka 2002 (Waraka wa Malezi na Ushauri Nasaha) ulioagiza wazi kuwa kila shule/chuo kitakuwa na kamati ya malezi na mwalimu wa malezi na ushauri.
Waraka huo ulitaka kila shule iwe na mwalimu mlezi anayechaguliwa na wanafunzi wenyewe na kamati ya malezi na ushauri nasaha, ili kushughulikia matatizo ya wanafunzi yanayohusiana na ukuaji, maadili, afya na maisha yao ya kila siku.
Umuhimu wa unasihi
Utafiti unaonesha wazi kuwa ufanisi katika elimu hauwezi kutenganishwa na unasihi na kwamba unasihi ni sehemu muhimu ya mafunzo ya ualimu. Huduma za unasihi zinapoimarishwa shuleni, kwa mfano, zinaongeza hali ya wanafunzi kujitambua, kujiamini, kufanya uamuzi unaoongozwa na uelewa, na hivyo kupunguza mdondoko, mimba za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia na kuongeza kufaulu.
Serikali kwa kutambua umuhimu huo, mwaka 2020 ilitoa mwongozo wa malezi, unasihi na ulinzi wa mtoto unaolenga kumsaidia mwalimu mnasihi kutekeleza vyema Waraka wa Elimu na 11 wa 2002. Mwongozo huu unaeleza kwa kina dhana ya unasihi, hatua za kufuata katika kutoa unasihi, mbinu za usikilizaji unaolenga kumuelewa mwanafunzi, na jukumu la mwalimu mlezi katika kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji na kuwapa msaada wa kisaikolojia.
Uelewa wa walimu
Pamoja na umuhimu wake, uelewa wa dhana na misingi ya unasihi umeendelea kuwa changamoto miongoni mwa walimu na viongozi wa shule.
Kwa wengi kwa mfano, “unasihi” unachanganywa na huduma ya kutoa ushauri au kumuelekeza mtoto afanye nini.
Unasihi unatazamwa kama mazungumzo ya kawaida na maoni yanayoweza kutolewa na mtu yeyote badala ya uhusiano wa kitaalamu unaolenga kumsaidia mwanafunzi kuelewa nafsi yake, kutatua matatizo yake mwenyewe na kufanya uamuzi unaoongozwa na uelewa.
Ingawa pamekuwepo mafunzo mengi ya unasihi nchini, hususani kwa walimu/wakufunzi wa vyuo vya ualimu, utafiti mwingi unaonyesha kuwa uelewa wa dhana za msingi za unasihi bado ni mdogo.
Nkuba Mabula, kwa mfano, mwaka 2015 katika utafiti wake uliochunguza hali ya mafunzo, maarifa na stadi za walimu wanasihi katika shule za sekondari za Tanzania, kiwango cha utayari wao kupokea mafunzo zaidi ili kuimarisha stadi zao.
Alibaini upungufu mkubwa wa stadi na maarifa ya unasihi miongoni mwa walimu wanasihi shuleni. Pamoja na uwepo wa mafunzo kadhaa, walimu bado hawana uwezo wa kushughulikia matatizo ya ndani na nje ya mwanafunzi yanayoathiri kujifunza. Hali bado haijabadilika sana.
Matokeo yake ni kwamba huduma ya unasihi imekuwa na utekelezaji wa kusuasua. Bado imani ya wanafunzi kwa walezi wao hairidhishi na hivyo wanafunzi wengi huona ni afadhali kuonana na marafiki zao na watu wengine wasioaminika kuliko kupeleka matatizo yao kwa walezi.
Mpango wa Shule Salama
Uamuzi huu wa kisera kufuta masomo ya unasihi, unatokea katika wakati muhimu ambapo serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza mpango wa Shule Salama ulioanzishwa mwaka 2022.
Mpango huu, pamoja na mambo mengine, unalenga kusaidia kukabiliana na ongezeko kubwa la matukio ya watoto kunyanyaswa kingono, ambapo utafiti unasema wanafunzi wengi hukumbana na hali hizi nyumbani, wakiwa njiani kwenda shule na wakati mwingine shuleni kwenyewe.
Lengo la pili la mpango huu ni kuhakikisha mtoto analindwa dhidi ya tishio la usalama wake na kwamba mifumo ya ulinzi wa mtoto inaimarishwa. Kwa ufupi, mpango huo unasisitiza kuimarisha huduma za unasihi ili kuwalinda wanafunzi dhidi ya unyanyasaji, mimba za utotoni na kuwapa nafasi ya kujieleza kwa usalama.
Katika mazingira ambayo walimu hawana uelewa mzuri wa misingi ya unasihi, ni wazi utekelezaji wa mpango wa shule salama, utakabiliwa na changamoto kubwa kwa sababu kuu mbili. Kwanza, mifumo ya kuripoti na kushughulikia matukio ya unyanyasaji inakuwa dhaifu. Lakini pili hata pale ambapo wanafunzi wanahitaji kupata msaada wa kisaikolojia, uelewa wa walimu katika kutoa huduma hii moja kwa moja au kuwapa rufaa ya huduma za kibobezi, unakuwa changamoto.
Utekelezaji wa mtalaa mpya
Kadhalika, mtalaa ulioboreshwa ulioanza kutumika kwa awamu kama alivyopata kueleza mara kwa mara Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, unamtaka mwanafunzi kufanya uamuzi muhimu wa masomo mara tu anapoingia kidato cha kwanza.
Hapo kabla, mwanafunzi alifanya uamuzi huo akiwa kidato cha tatu, baada ya kupata uzoefu wa masomo ya sekondari kwa miaka miwili.
Mabadiliko haya yenye nia njema yanaonesha haja kubwa ya msaada wa kitaalamu wa unasihi wa masomo, ili mwanafunzi asichague masomo kwa shinikizo la wazazi, marafiki au watu wanaomzunguka.
Aidha, utekelezaji wa mtalaa huu pia unamhitaji mwalimu anayejua mbinu bora za kuupata moyo wa mwanafunzi, kabla hajampakia maarifa. Mwanafalsafa Aristotle aliwahi kusema: “Elimu inayoelimisha kichwa cha mwanafunzi bila kubadilisha moyo wake, hiyo haiwezi kuwa elimu iliyokamilika.” Je, mwalimu asiyejifunza unasihi kwa kina, anaweza kweli kugusa moyo wa mwanafunzi?
Tufanyeje?
Nchi yetu inapitia wakati muhimu katika utekelezaji wa mtalaa mpya na Sera ya Elimu 2014 (toleo la 2023).
Sambamba na mtalaa huu, Serikali ina mipango kadhaa inayohitaji walimu wenye mahiri za unasihi katika kuitekeleza.
Ipo haja ya kutazama upya umuhimu wa unasihi kwa kuitazama kama taaluma isiyoweza kutolewa na mtu yeyote bila mafunzo maalum.
Aidha, mamlaka zinazohusika zione haja ya kupitia upya mwongozo wa uandaaji na utoaji wa shahada za ualimu na kurejesha umahiri wa unasihi kama sifa moja wapo ya ualimu.
Mwisho, tuone uwezekano wa kuimarisha mafunzo ya muda mfupi kwa walimu wa malezi ili kuwajengea mahiri za unasihi zinazowawezesha kutoa huduma ya unasihi kitaalam kuliko ilivyo sasa ambapo wengi wanatoa ushauri wakiamini ni unasihi.
Tuone haja ya kuutazama unasihi kama nguzo muhimu ya elimu kamilifu inayoanza na kumfanya mwanafunzi ajisikie salama kuwa kwenye mikono ya mwalimu.
Mwandishi ni mhadhiri, mtafiti na mshauri elekezi wa sayansi ya ujifunzaji katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
