Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Mei 25, 2026 Jamhuri itamsomea hoja za awali (Ph) mfanyabiashara Monica Beda (36) anayekabiliwa na shtaka moja la kujipatia Sh60 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Beda, ambaye ni mkazi wa Kimara, anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Agrey Mashanda, kwa madai kuwa atamuagizia gari aina ya Mitsubishi Fighter Fuso, jambo ambalo alijua kuwa ni uongo.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne Mei 19, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo yake.
Hakimu Mshasha alisema kwa kuwa maelezo ya mshtakiwa huyo bado hayajapandishwa katika mfumo wa Mahakama, kesi hiyo anaahirisha mpaka Mei 25, 2026 kwa ajili ya Jamhuri kumsomea hoja za awali.
Mfanyabiashara, Monica Beda (36) anayekabiliwa na shtaka moja la kujipatia Sh60 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Florida Wencelaus alidai maelezo ya awali ya mshtakiwa huyo yapo tayari ila bado hayajapandishwa katika mfumo wa Mahakama.
“Mheshimiwa hakimu, kutoka na sababu hiyo tunaomba mahakama yako itupangie tarehe fupi ili tuweze kumsomea maelezo yake mshtakiwa na kesi hii iweze kuendelea na hatua nyingine,” alisema Wakili Wencelaus.
Kwa mara ya kwanza, Monica alifikishwa Mahakamani hapo Aprili 20, 2026 na kusomewa kesi ya jinai namba 8385 ya mwaka 2026.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 8, 2025 Mtaa wa Samora katika Jiji la Dar es Salaam, ambapo kwa njia ya udanganyifu alijipatia fedha taslimu Sh60 milioni kutoka kwa Agrey Mashanda.
Alijipatia fedha hizo kutoka kwa Mashanda kwa ukijifanya utamuagizia gari aina ya Toyota Mitsubishi Fighter Fuso, wakati ukijua kuwa ni uongo.
Mfanyabiashara, Monica Beda (36) anayekabiliwa na shtaka moja la kujipatia Sh60 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Mshtakiwa huyo bado yupo rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana aliyopewa Aprili 2026.
Masharti hayo yalitolewa na Hakimu Mshasha ambaye alimtaka mshtakiwa awe na wadhamini wawili na mmoja wapo anatakiwa awasilishe nusu ya mali anayodaiwa kuiba ambayo ni Sh30 milioni au awasilishe mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Pia, hakimu Mshasha alisema kama wadhamini wataweka hati ya kiwanja kama dhamana, hati hiyo inatakiwa iwe imefanyiwa tathimini na ripoti yake kuambatanishwa kwa pamoja.
Vilevile wadhamini hao wanatakiwa wawe na barua za utambulisho kutoka taasisi husika kama ni wafanyakazi na kama sio wafanyabiashara basi wanatakiwa wawe na barua kutoka serikali za mitaa.
