Morogoro. Serikali mkoani Morogoro, imeanza utekelezaji wa mkakati wa kupanda miti milioni mbili ya viungo na matunda ifikapo mwaka 2030, ili kufungua fursa ya biashara ya kaboni, uhifadhi wa mazingira na ongezeko la kipato kwa wananchi.
Mpango huo unaotekelezwa kupitia ushirikiano wa Serikali, Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), ambapo hadi sasa zaidi ya miche 200,000 ya mikarafuu, kokoa, parachichi, michikichi, korosho na mdalasini imepandwa Kilosa, Kilombero, Mvomero na Mlimba.
Akizungumza katika mafunzo ya kilimo msitu yaliyofanyika leo Mei 19, 2026 mjini Morogoro, Ofisa Kilimo Mshauri wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Peter Gama, amesema Serikali imeamua kuwekeza katika kilimo msitu ili kuunganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya uchumi wa wananchi.
“Kilimo msitu kina faida kubwa kwa sababu mkulima anaweza kuendelea kuvuna mazao kama mahindi, hiliki na kokoa huku miti ikiendelea kukua na kuhifadhi mazingira,” amesema.
Gama, amesema Serikali pia imesambaza miche ya mikarafuu, mdalasini na kokoa kwa wakulima na wanafunzi kupitia kampeni ya Jisomeshe na Mkarafuu inayowahamasisha wanafunzi wa kidato cha kwanza kupanda miti kwenye mashamba ya familia zao.
Mkazi wa kijiji cha Nakatimbu Wilaya ya Kilombero, Zakaria Kayombo akizungumza jambo wakati wa mafunzo ya kilimo msitu yanayoshirikisha wakulima, wafugaji na wajumbe wa kamati za mazingira yanayofanyika kwa kipindi cha wiki moja, Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda
Amesema kilimo msitu kina mchango mkubwa katika kupunguza ukataji miti hovyo, uchomaji moto na ongezeko la hewa ya kaboni inayochangia mabadiliko ya tabianchi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Wadau wa Uwezeshaji wa Jamii na Ustawi wa Mazingira, Victoria John, amesema wakulima wengi tayari wanafanya kilimo msitu bila kufahamu faida yake, ikiwemo biashara ya kaboni na masoko ya kimataifa.
Amesema kupitia mradi huo, wananchi wa Wilaya ya Kilombero wameanza kupewa elimu kuhusu matumizi endelevu ya ardhi, usawa wa kijinsia na namna ya kunufaika na masoko ya kaboni.
“Kilimo msitu kinaongeza kipato cha mkulima lakini pia kinatunza mazingira na kusaidia kukabiliana na athari za tabianchi,” amesema Victoria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Agra, Dk Rachel Zakayo, amesema Morogoro ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha miradi ya kaboni kutokana na mazingira yake na utegemezi mkubwa wa sekta ya kilimo.
Amesema mfumo huo husaidia kufyonza hewa ya kaboni, kurejesha uoto wa asili na kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunataka kuona wananchi, hasa wanawake na vijana wakinufaika moja kwa moja na uchumi wa kijani kupitia miradi ya mazingira,” amesema Dk Rachel.
