Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Afrika inahitaji mifumo ya nishati iliyo ya uhakika, nafuu na endelevu ili kuendana na kasi ya maendeleo ya uchumi, viwanda na teknolojia ya kidijitali.
Amesema upatikanaji wa umeme wa kutosha utakuwa nguzo muhimu katika kuimarisha ushindani wa kiuchumi wa nchi za bara hilo katika miaka ijayo.
Rais Samia ameyasema hayo leo Mei 19, 2026 wakati akihutubia mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia Barani Afrika (NEISA), uliofanyika nchini Rwanda chini ya uenyeji wa Rais Paul Kagame.
Neisa ni jukwaa maalumu la ngazi ya juu barani Afrika linalolenga kuendeleza matumizi ya nishati ya nyuklia kama nyenzo muhimu kuchochea maendeleo endelevu, ukuaji wa viwanda na usalama wa nishati.
Amesema ongezeko la shughuli za uzalishaji, uchimbaji wa madini pamoja na ukuaji wa miji, linaongeza mahitaji ya vyanzo vya umeme vya uhakika vinavyoweza kuzalisha nishati kwa muda wote, hali inayozifanya nchi za Afrika kutafuta suluhisho la muda mrefu katika sekta ya nishati.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipotembelea maonyesho wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), Kigali nchini Rwanda Mei 19, 2026.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Rais wa Togo, Faure Essozimna Gnassingbé, pamoja na viongozi wengine wa Afrika wanaojadili mustakabali wa nishati na maendeleo ya viwanda barani humo.
Katika hotuba yake, Rais Samia amesema nishati ya nyuklia haipaswi kutazamwa kama mshindani wa nishati mbadala, bali kama sehemu ya mkakati mpana wa kujenga mfumo imara wa nishati utakaosaidia ukuaji wa viwanda na uchumi wa muda mrefu.
Amesema Afrika inapaswa kuwekeza katika mchanganyiko wa vyanzo vya nishati ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika unaoweza kuhimili ongezeko la mahitaji ya maendeleo ya kisasa.
Rais Samia ametaja maeneo matatu muhimu yanayoonekana kuwa msingi wa mafanikio ya programu za nishati ya nyuklia barani Afrika, ikiwemo changamoto ya ufadhili wa miradi, usalama wa matumizi ya teknolojia hiyo pamoja na umuhimu wa ushirikiano wa kikanda.
Kuhusu suala la ufadhili, amesema nchi nyingi za Afrika bado zinakabiliwa na ugumu wa kupata fedha za kutekeleza miradi mikubwa ya nishati ya nyuklia kutokana na gharama zake kuwa kubwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipotembelea maonyesho wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), Kigali nchini Rwanda Mei 19, 2026.
Amesisitiza haja ya taasisi za kifedha za kimataifa pamoja na washirika wa maendeleo kushirikiana na nchi za Afrika ili kuwezesha upatikanaji wa fedha na teknolojia zitakazosaidia bara hilo kufanikisha malengo yake ya nishati na maendeleo ya viwanda.
“Ni vyema tutakawa na mifumo ya kibunifu ya kifedha na mikopo inayozingatia mazingira ya Afrika ili kuwezesha miradi hiyo kupata wawekezaji na mikopo kwa urahisi zaidi.
Ushirikiano wa kikanda ni nguzo muhimu katika kufanikisha ajenda ya nishati ya nyuklia Afrika. Katika hili nimpongeze kaka yangu Paul Kagame kwa mchango wake katika kuratibu mjadala wa maendeleo ya nishati ya nyuklia,”
Amesema ushirikiano huo utawezesha kutafuta fursa za uwekezaji na kubadilishana uzoefu katika matumizi ya nishati ya nyuklia kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Rais Samia pia amesisitiza kuwa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia yanahitaji uwepo wa mifumo madhubuti ya udhibiti pamoja na wataalamu wenye ujuzi wa kutosha kusimamia sekta hiyo.
“Tunaamini uwekezaji katika sekta ya nishati ya nyuklia unaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, hasa wakati mahitaji ya nishati yakiendelea kuongezeka kutokana na ukuaji wa viwanda, miji na shughuli za uzalishaji,” amesema Rais Samia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati la atomiki (IAEA), Rafael Mariano Grossi pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), Kigali nchini Rwanda Mei 19, 2026.
Katika hatua hiyo, amepongeza mchango wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) kwa kusaidia nchi mbalimbali za Afrika kuimarisha uwezo wa kisheria na kiufundi katika matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani na maendeleo.
Kwa upande wake Rais Kagame amesema kwa bara la Afrika nishati sio tu suala la maendeleo bali ni chanzo cha msingi wa ukuaji wa viwanda.
“Hii ndio sababu tunaona nishati ya nyuklia kama nguzo muhimu kwa mipango ya muda mrefu ya bara la Afrika na mafanikio yake,” amesema Kagame.
Akizunguma kwenye mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa IAEA na Mkurugenzi Mtendaji wa International Atomic Energy Agency (IAEA) Rafael Mariano amesema taasisi hiyo inafahamu changamoto ya mitaji na iko tayari kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufadhili miradi ya nyuklia.
