
Uganda imeanzisha udhibiti wa mipaka kutokana na mlipuko wa virusi vya Ebola. Wafanyakazi wa afya nchini humo tayari wameanza kupima halijoto ya watu huku wakiwasaidia kunawa mikono yao karibu na Bundibugyo magharibi mwa Uganda.
Mlipuko wa virusi hivyo, unaoaminika kuua makumi ya watu, umetangazwa kuwa ni dharura ya afya ya umma inayotia wasiwasi kimataifa.
“Tuliposikia habari za Ebola, ilitubidi kwanza tuwaambie wahudumu waliokuwa katika kituo cha afya jinsi wanavyoweza kujizuia kuwasiliana na watu ambao wanaweza kuwa na Ebola au wale wanaowashuku kuwa na Ebola,” amesema Clovis Bwambale, mfanyakazi wa afya wa Uganda.
Janga hili la sasa linasababishwa na aina ya Bundibugyo ambayo si ya kawaida sana, ambayo haina chanjo au matibabu maalumu.
Awali, Waziri wa Afya wa Kongo, Samuel Roger Kamba Mulamba alikuwa amesema kwamba aina mpya ya virusi vya Ebola vinavyoenea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni “vikali sana na hakuna chanjo au matibabu maalumu ya kuvidhibiti.”
Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Afrika (Africa CDC) vimetangaza mlipuko wa Ebola nchini DR Congo na Uganda kuwa Dharura ya Afya ya Umma ya Bara.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imerekodi vifo 131 kutokana na visa 513 vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola, na kumekuwa na kifo kimoja katika nchi jirani ya Uganda.
