
Polisi wa San Diego huko California nchini Marekani wametangaza kwamba watu watano wameuawa katika shambulio lililolenga kituo cha Kiislamu cha mji huo, wakiwemo washambuliaji wawili.
Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo kama uhalifu uliotokana na chuki.
Mkuu wa Polisi wa San Diego, Scott Wall amesema miongoni mwa waliouawa ni mlinzi wa msikiti, akibainisha kuwa washambuliaji wawili walikuwa vijana waliowaua watu watatu, kisha wakajiua wenyewe kwa kujipiga risasi.
Polisi wameeleza kwamba timu za dharura zimepata miili ya waathiriwa ndani ya kituo kikubwa cha Kiislamu huko San Diego, kabla ya ya kupata miili ya washambuliaji hao wawili, waliokuwa na umri wa miaka 19 na 17.
Katika tukio lenye uhusiano na kadhia hii, mwandishi wa habari wa NBC News amewanukuu maafisa wa kutekeleza sheria wakisema kwamba wapelelezi wanachunguza maandishi yanayochochea chuki dhidi ya Uislamu yaliyopatikana ndani ya gari ambalo polisi wamepata miili ya washukiwa hao wawili wakiwa wamekufa.
Akisisitiza habri ya tukio hilo, Meya wa San Diego, Todd Gloria amesema kwamba Kituo cha Kiislamu katika kitongoji cha Claremont cha jiji hilo, ambacho kina msikiti mkubwa zaidi, kimeshambuliwa kwa risasi.
Polisi wameripoti kwamba mmoja wa walinzi wa usalama katika Kituo cha Kiislamu alikuwa miongoni mwa watu watatu waliouawa, huku utambulisho wa waathiriwa wengine wawili ukiwa bado haujulikani.
Mkurugenzi wa Kituo cha Kiislamu cha San Diego, Imam Taha Hassan, amethibitisha katika ujumbe wake usalama wa “watoto wote wanaosoma katika kituo hicho, wafanyakazi na walimu”.
Amesema: “Hatujawahi kushuhudia maafa kama haya hapo awali. Kwa sasa, ninachoweza kusema ni kwamba tunaomba na kusimama kwa ajili ya kuonesha mshikamano na familia zote za waathiriwa katika jamii yetu.”
Kituo cha Kiislamu cha San Diego ndicho kikubwa zaidi katika kaunti hiyo na kina msikiti mkubwa zaidi. Kwa mujibu wa tovuti yake, pia kinajumuisha taasisi za elimu, ikiwamo Shule ya Al-Rashid, ambayo hutoa masomo ya Kiislamu na Kiiarabu, na kuhifadhi Qur’ani.
