Dar es Salaam. Tanzania imeendelea kujijengea nafasi kama moja ya nchi zinazoongoza mageuzi ya kidijitali katika sekta ya afya barani Afrika, baada ya kuunganisha mifumo na kupanua huduma za tiba mtandao katika hospitali mbalimbali nchini.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema hatua hiyo imeiwezesha Tanzania kuondoka katika mifumo iliyokuwa imegawanyika na kuelekea kwenye mfumo mmoja wa kitaifa unaorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza mjini Geneva jana Jumatatu, Mei 18, 2026 katika mkutano uliofanyika pembeni mwa Mkutano Mkuu wa Afya Duniani (World Health Assembly), Mchengerwa amesema mageuzi hayo yanalenga kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote bila kujali eneo wanaloishi au uwezo wao wa kifedha.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akiwa katika mkutano kuhusu uimarishaji wa afya kidijitali, uliofanyika pembeni mwa Mkutano Mkuu wa Afya Duniani (World Health Assembly)
“Kwa Tanzania, afya kidijitali siyo tu teknolojia. Ni kuhusu watu,” amesema.
Amesema katika kipindi cha miaka ya nyuma, Tanzania ilikuwa na mifumo mingi ya kidijitali ambayo haikuweza kuwasiliana, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto katika utoaji wa huduma za afya.
Hata hivyo, amesema chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imeweka mkazo katika kuunganisha mifumo hiyo kitaifa kupitia mfumo wa mawasiliano wa pamoja.
Kwa sasa, zaidi ya vituo 220 vya afya vina uwezo wa kuwasiliana kidijitali, hatua inayorahisisha upatikanaji wa taarifa za wagonjwa na usimamizi wa rufaa kutoka ngazi ya chini hadi hospitali za rufaa.
Kwa mujibu wa waziri huyo, mgonjwa anayehamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kingine hahitaji tena kubeba mafaili ya karatasi kwa sababu madaktari wanaweza kuona historia ya matibabu kwa njia ya kielektroniki.
Amesema mfumo huo umeanza kupunguza urudufu wa vipimo vya maabara, kuboresha uamuzi wa kitabibu na kuimarisha mwendelezo wa huduma kwa wagonjwa.
Katika hatua nyingine, Serikali imeanza kupanua huduma za tiba mtandao (telemedicine) katika hospitali takribani 25 nchini ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa wataalamu wa afya katika maeneo ya vijijini.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akiwa katika mkutano kuhusu uimarishaji wa afya kidijitali, uliofanyika pembeni mwa Mkutano Mkuu wa Afya Duniani (World Health Assembly).
Kupitia mfumo huo, madaktari waliopo katika vituo vya afya vya mbali wanaweza kupata ushauri wa wataalamu bingwa waliopo katika hospitali kubwa kwa wakati halisi.
Mchengerwa amesema huduma hizo zimekuwa msaada mkubwa katika afya ya mama na mtoto, matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza, huduma za radiolojia pamoja na huduma za dharura.
“Mgonjwa aliyepo wilayani kijijini sasa anaweza kupata utaalamu ambao hapo awali ulikuwa unapatikana katika miji mikubwa pekee,” amesema.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutumia teknolojia za simu kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kusajili kaya, kufuatilia afya za wajawazito na watoto pamoja na kutoa rufaa kwa wagonjwa.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, matumizi ya mifumo hiyo yanaisaidia Serikali kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma katika upatikanaji wa huduma za afya.
Amesema Tanzania pia imeanza kuandaa mazingira ya matumizi ya akili unde (AI) katika sekta ya afya kupitia mfumo wa sera wa kitaifa unaolenga kuhakikisha matumizi yake yanakuwa salama, yenye maadili na uwajibikaji.
Baadhi ya maeneo yanayotajwa kunufaika ni pamoja na uchunguzi wa mapema wa milipuko ya magonjwa, kupitia uchambuzi wa takwimu pamoja na kusaidia uchunguzi wa picha za kitabibu.
Hata hivyo, Mchengerwa amesema AI haitachukua nafasi ya wahudumu wa afya bali itatumika kusaidia kazi zao huku faragha na usalama wa taarifa za wagonjwa ukilindwa.
Amesema Serikali pia inaendelea kuimarisha mifumo ya usalama wa mtandao na sheria za ulinzi wa taarifa ili kuongeza imani ya wananchi katika huduma za afya za kidijitali.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akiwa katika mkutano kuhusu uimarishaji wa afya kidijitali, uliofanyika pembeni mwa Mkutano Mkuu wa Afya Duniani (World Health Assembly)
Katika kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu, Serikali imeanza kujumuisha afya ya kidijitali katika bajeti za Taifa huku ikisisitiza umuhimu wa wadau wa maendeleo kuzingatia mifumo inayounganishwa kitaifa badala ya miradi ya muda mfupi isiyowasiliana.
Mchengerwa amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa mengine katika kuendeleza afya ya kidijitali kwa lengo la kujenga mfumo wa afya wenye usawa na unaowafikia wananchi wote.
