
Hatimaye baada ya miaka 22 ya ukame, Arsenal au ukipenda waite The Gunners wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu wa 2025-26 baada ya Man City kulazimishwa sare ya bao moja kwa moja na The Cherries ambao nao walikuwa wanafukuzia angalau alama moja ili wafaulu kushiriki kombe la Uefa Conference Cup msimu ujao.
Man City walikuwa nyuma ya Arsenal kwa alama tano wakienda ugani Vitality baada ya vijana wa kocha Mikel Arteta kutekeleza jukumu lao kwa kuinyuka Burnley bao moja kwa nunge siku ya Jumatatu.
Sare ya 1-1 baina ya City na Bournemouth ina maana kwamba wakiwa na alama 78 dhidi ya 82 za Arsenal, alama za juu zaidi wanazoweza kupata ni 81 kwenye mechi ya funga msimu, hata kama Arsenal watapoteza mchezo wao dhidi ya Crystal Palace, Jumapili ijayo.
Mafanikio hayo ya Arsenal yanahitimisha ukame wa miaka 22 bila taji la EPL na kurejesha kombe hilo kaskazini mwa jiji la London.
Baada ya kubeba taji la nyumbani, swali linabaki: Je, Arsenal itaweza kufanya hivyo hivyo itakapomenyana na Paris Saint-Germain katika fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya huko Budapest?
Fainali ya Ligi ya Mabingwa ya UEFA ya 2025/26 kati ya Paris Saint-Germain na Arsenal itafanyika tarehe 30 mwezi huu wa Mei katika Uwanja wa Puskás Aréna mjini Budapest nchini Hungary.
