Chadema yamjibu Msajili, CCM yaingia mtegoniChadema yamjibu Msajili, CCM yaingia mtegoni

Dar es Salaam. Uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kisimamishiwe usajili wake, kitozwe faini au kiruke kiunzi, umebaki mikononi mwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Hiyo ni baada ya Chadema, kukamilisha matakwa ya barua ya Ofisi ya Msajili ya Mei 7, 2026, iliyokitaka chama hicho kujieleza kwa nini kisisimamishiwe usajili au kutozwa faini kwa kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Usajili.

Chadema, imesema imeijibu barua hiyo kwa tarehe isiyozidi Mei 20 2026 kama ilivyoelekeza na majibu hayo yamewasilishwa kwa Ofisi ya Msajili.

Mei 7, 2026 Ofisi ya Msajili, iliiandikia Chadema barua yenye kumbukumbu namba HA.322/362/16A/22 iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, ikiituhumu kwa ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, hivyo ijieleze kwanini isisimamishiwe usajili au kutozwa faini.

Katika hatua nyingine, Chama cha Mapinduzi (CCM) nacho, kimekutana na ‘mkono’ wa ofisi ya msajili, baada ya kuandikiwa barua, kikitakiwa kutoa maelezo kujibu tuhuma za ukiukaji wa sheria ya vyama vya siasa.

Hatua ya msajili kuiandikia barua CCM, imetokana na kauli ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT), Mary Chatanda aliyesema Rais Samia Suluhu Hassan, angemwachia nchi kwa dakika moja, wale aliowaita wanaoichafua nchi kutoka nje, hajui kama wangekuwepo.

“Nasema, kama ningekabidhiwa nchi hii hata kwa dakika moja tu! Mama Samia, sijui kama wale watu wangekuwepo. Wamemkuta ndugu yetu mpendwa, Dk Samia, akiwa mpole, mnyenyekevu na msikivu,” alisema Chatanda Mei 18, 2026 akiwa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge, Isimani mkoani Iringa.

Chadema: Tumejibu

Mwananchi imeiona barua ya majibu ya Chadema iliyosainiwa na Katibu mkuu wake, John Mnyika kwenda Ofisi ya Msajili, ikikanusha tuhuma zote, huku kikidai hakijakiuka sheria yoyote ya vyama vya siasa.

Pia, Chadema imesema hata kama kungekuwa na ukiukwaji wa Katiba, madai hayo yanayohusu makosa ya jinai yanaweza kuamuliwa na Mahakama pekee iwapo yamethibitishwa au la na si Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Chama chetu hakijakiuka Sheria ya Vyama vya Siasa kama inavyodaiwa. Kilichofanyika ni utekelezaji wa haki za kisiasa na Kikatiba zilizoainishwa katika Katiba ya nchi,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Chama hicho pia kimeitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia kikamilifu Katiba ya Tanzania na misingi ya demokrasia ya vyama vingi.

“Kufanya hivyo, kutaifanya Ofisi ya Msajili kutekeleza kazi zake kwa ufanisi na kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi ya demokrasia ya vyama vingi kama inavyotamkwa katika Ibara ya 3(1) ya Katiba ya Tanzania,” imeeleza barua hiyo.

Katika maelezo yake, Chadema imeahidi kuendelea kutekeleza shughuli zake za kisiasa kwa mujibu wa Katiba, sheria za nchi na misingi ya kidemokrasia bila kuyumbishwa.

Pia, imesisitiza kuwa, haijatenda kosa lolote linalostahili adhabu ya kusimamishwa usajili au kutozwa faini, huku ikidai kifungu cha 19(2)(f) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ni kinyume cha Katiba.

“Chadema haitasita kutumia njia zote halali za kisheria, Kikatiba na kidemokrasia kulinda haki zake za kisiasa, uhuru wa chama na haki za wanachama wake,” imeeleza sehemu nyingine ya barua hiyo.

Imeeleza kuwa, chama hicho kimejieleza kuwa, kinaamini katika utawala wa sheria na hakiko tayari kuona maisha ya watu yanapotea halafu kukafanyika uchunguzi unaodaiwa kuwa wa kimaigizo.

Msajili akiri kupokea barua

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 20, 2026, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Nyahoza amethibitisha kupokea barua ya maelezo kutoka Chadema, lakini amesema bado hajaipitia wala kutoa uamuzi kwa kuwa yuko kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa kinachoendelea Morogoro.

“Tupo katika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa, Morogoro, kinachoendelea leo, hivyo bado sijaisoma na kutoa uamuzi,” amesema Nyahoza.

Katika barua ya Msajili kwenda Chadema, baadhi ya matukio yaliyotajwa ni pamoja na kauli zinazodaiwa kutolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, kuhusu mpango wa kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kuachiwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na kesi mahakamani.

Nyahoza amesema kauli hizo zinaweza kutafsiriwa kama shinikizo kwa mhimili wa Mahakama na zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama wa nchi, jambo linalokatazwa chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Barua ya msajili kwa Chadema

Katika barua yake, Msajili pia alinukuu kauli zinazodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Korogwe, Oliver Kisaka akizitaja kuwa za uchochezi na zinazoweza kuhamasisha vurugu za kisiasa, hasa kutokana na rejea zake kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025 pamoja na kauli mbiu ya “No Reform, No Election.”

Kwa mujibu wa kifungu cha 19(2)(f) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, chama hakipaswi kuruhusu viongozi au wanachama wake kutumia lugha ya matusi, kashfa, kisasi au uchochezi inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama wa nchi.

“Kesi ya Tundu Lissu ipo mahakamani. Kushinikiza au kuhamasisha watu washinikize aachiwe ni sawa na kuishinikiza Mahakama kutoa uamuzi wa kupendelea upande fulani, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi,” inaeleza sehemu ya barua ya Msajili.

Maoni ya wadau

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa George Kahangwa amesema umuazi utategemea na namna ambavyo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itakaposoma maelezo yao.

“Litakuwa jambo la busara iwapo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wataielewa barua ya Chadema, ikiwa ngumu basi ikiwezekana wafanye mazungumzo na Chadema iachwe ifanye shughuli zake za kisiasa,”amesema.

Kuhusu CCM

Akizungumzia sakata la CCM, Nyahoza amesema ofisi yake imezipokea video na taarifa za matamshi hayo na tayari imechukua hatua.

“Kuhusu suala la mheshimiwa Chatanda, na sisi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tumetumiwa video na picha hizo, tumekwisha iandikia CCM barua ili wawasilishe maelezo kuhusu suala hilo,” amesema Nyahoza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *