Mwanafunzi adaiwa kujifungua, kumtupa mtoto chooniMwanafunzi adaiwa kujifungua, kumtupa mtoto chooni

Bagamoyo. Mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari Kibindu wilayani Bagamoyo mkoani Pwani anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujifungua mtoto na kumtupa kwenye shimo la choo cha mabweni ya wanafunzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 20, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase tukio hilo liligundulika Mei 19, 2026 saa 4:00 asubuhi katika shule hiyo iliyopo Kata ya Kibindu.

“Mwanafunzi huyo alikuwa na ujauzito ambao haukubainika katika kipindi chote cha miezi tisa hadi alipohisi maumivu makali ya tumbo na kwenda chooni, ambapo alijifungua mtoto huyo na kumtupa chooni,” imedai taarifa hiyo. 

Taarifa hiyo imeendelea kueleza   kuwa baada ya tukio hilo, mwanafunzi mwingine aliingia chooni na kuona matone ya damu karibu na tundu la choo.

Alipomwaga maji alisikia sauti ya mtoto ndipo alipoutaarifu uongozi wa shule na kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji pamoja na Polisi Kata, jitihada za kumuokoa mtoto huyo zilifanyika na baadaye kuwahishwa katika Kituo cha Afya Kibindu kwa matibabu.

Polisi wamesema mama pamoja na mtoto wanaendelea kupatiwa matibabu huku hatua nyingine za kisheria zikisubiri kukamilika kwa matibabu hayo.

Katika hatua nyingine, Jeshi hilo linamshikilia Kesi Ibrahim mkazi wa Kifuleta, Chalinze kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa miaka sita.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo tukio hilo lilitokea Mei 17, 2026 saa 7:00 mchana katika kijiji cha Kifuleta, Kata ya Kimange ambapo mtuhumiwa anadaiwa kumlaghai mtoto huyo na kumuingiza chumbani kwake kabla ya kumfanyia kitendo hicho.

Baada ya wazazi wa mtoto kubaini tukio hilo walitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mbwewe na juhudi za kumkamata mtuhumiwa zikafanikiwa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi wa matukio yote mawili na   watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *